Serikali yapinga wazo la kuchapisha Nida ZanzibarSerikali yapinga wazo la kuchapisha Nida Zanzibar

Dar es Salaam. Serikali imesema haina mpango wa kuanza kuchapisha vitambulisho vya Taifa vya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) Zanzibar kwa mfumo unaotumika katika utoaji wa pasi za kusafiria, ikieleza mfumo wa sasa wa uchapishaji wa pamoja unaimarisha usalama na kudhibiti udanganyifu.

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Alhamisi, Mei 21, 2026 na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Ayoub Mohammed Mahmoud alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Mtoni, Abubakar Mohammed Mussa, aliyehoji ni lini Serikali itaanza kuchapisha vitambulisho vya Nida Zanzibar ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi.

Katika majibu ameeleza uzalishaji wa vitambulisho vya Taifa nchini hufanyika katika Kituo Kikuu cha Uchakataji wa Taarifa (Data Centre), ambako taarifa zote za usajili na utambuzi wa wananchi huchakatwa kabla ya kuzalishwa kwa Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIN) na vitambulisho vyenyewe.

Naibu waziri huyo amesema kituo hicho kina mifumo ya kisasa ya utambuzi wa alama za vidole inayomwezesha kila mwombaji kutambuliwa kipekee, hatua inayosaidia kuzuia uwezekano wa mtu mmoja kujisajili zaidi ya mara moja.

Amesema uchapishaji wa vitambulisho hivyo unafanywa kwa mfumo wa pamoja wa kitaifa kwa lengo la kuhakikisha usalama wa taarifa za wananchi, udhibiti wa ubora wa vitambulisho pamoja na usimamizi madhubuti wa mifumo ya utambuzi wa kibayometriki.

Aidha, ameeleza mfumo huo unasaidia kulinda taarifa muhimu za wananchi kupitia teknolojia za usimbaji wa taarifa (encryption) na matumizi ya vifaa maalumu vya kiusalama.

Mahmoud amesema kuanzisha vituo vya uchapishaji katika maeneo tofauti ikiwemo Zanzibar kunaweza kuongeza gharama za uendeshaji kutokana na mahitaji ya mitambo, wataalamu pamoja na mifumo mingine ya kiusalama.

“Hatua hiyo inaweza kuongeza hatari ya kutengenezwa kwa vitambulisho bandia, udanganyifu na uwezekano wa kutofautiana kwa ubora wa vitambulisho vinavyozalishwa,” amesema naibu waziri huyo.

Serikali imeendelea kusisitiza mfumo wa sasa umewekwa kwa lengo la kuhakikisha vitambulisho vya Taifa vinatolewa kwa viwango vinavyofanana na kwa usalama mkubwa kwa wananchi wote nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *