Jamhuri yaomba kuongeza mashahidi kesi ya ‘Dk Manguruwe’Jamhuri yaomba kuongeza mashahidi kesi ya ‘Dk Manguruwe’

Dar es Salaam. Jamhuri imewasilisha mahakamani notisi ya kuomba kuongeza idadi ya mashahidi na vielelezo katika kesi ya  kuendesha biashara ya upatu inayomkabili Mkurugenzi wa Kampuni ya Vanilla International Ltd, Simon Mkondya(40), maarufu Dk Manguruwe na Rweyemamu John (59), ambaye ni Meneja na Mkaguzi wa fedha wa kampuni hiyo.

Wakili wa Serikali, Cathbert Mbiling’i ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Alhamisi, Mei 21, 2026 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa mashtaka.

Mkondya na John, wanakabiliwa na mashtaka 126 yakiwemo ya kuendesha biashara ya upatu na utakatishaji fedha yanalomkabili Mkondya pekee yake.

Wakili Mbiling’i alitoa taarifa hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini, anayesikiliza kesi hiyo.

“Leo kesi imeitwa kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji, lakini upande wa Jamhuri tumewasisha mahakamani notisi za kuomba kuongeza idadi ya mashahidi na vielelezo katika kesi hii.”

“Na tayari notisi hiyo tumeshaisajili kwenye mfumo wa Mahakama,”amesema.

Baada ya kutoa taarifa hiyo, wakili wa utetezi, Benito Mzuro amesema kuwa notisi hiyo pamoja na nyaraka bado hazijawafikia.

Hakimu Mhini baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili, amesema kwa kuwa notisi hiyo haijawafikia upande wa utetezi, anaahirisha kesi hiyo hadi Mei 26, 2026 ili kutoa nafasi ya kupata nyaraka hizo.

Mshtakiwa Mkondya amerudishwa rumande kwa sababu ana mashtaka ya kutakatisha fedha ambayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

Mashtaka yao

Katika mashtaka hayo 126: mashtaka 117 ni ya kuendesha biashara ya upatu yanayowakabili washtakiwa wote wawili na mashtaka 9 ni ya kutakatisha yanayomkabili Mkodya pekee yake.

Katika moja ya mashtaka hayo kuendesha biashara ya upatu, washtakiwa wanadaiwa  kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba Mosi,2023, jijini Dar es Salaam, walitenda makosa hayo

Inadaiwa kuwa Mkondya akiwa kama Mkurugenzi wa kampuni hiyo na John akiwa Meneja wake waliendesha biashara ya upatu kwa kuwaahidi watu watapata pesa mara mbili hadi tatu kama faida zaidi ya waliyotoa.

Washtakiwa hao wanadaiwa kujipatia pesa kutoka kwa watu zaidi ya 117 tofauti ambao walitoa kiasi tofauti cha fedha kwa kuwaahidi kuwa watapata faida mara mbili hadi tatu ya fedha walizotoa.

Katika mashtaka tisa ambayo ni ya utakatishaji fedha yanayomkabili Mkondya pekee yake, inadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba Mosi, 2023 akiwa katika mkoa wa Dar es salaam na akiwa kama Mkurugenzi wa Kampuni hiyo alijipatia jumla ya viwanja tisa vilivyopo katika kitalu namba AB eneo la Idunda mkoani Njombe.

Mkondya anadaiwa kujipatia viwanja hivyo huku akijua viwanja hivyo ni mazalia ya makosa tangulizi ya kuendesha biashara ya upatu.

Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Novemba 5, 2024 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 31523 ya mwaka 2024.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *