
Dar es Salaam. Kitunguu saumu ni kiungo kilichojikita katika mapishi ya vyakula mbalimbali hapa nchini lakini faida zake hazina mwisho Kinatumika si tu katika vyakula bali pia kwenye chai au vinywaji vingine vya moto au baridi
Kinachofanya kitunguu saumu kiwe cha kipekee ni uwepo wa ‘antioxidants allicin’ kemikali ya sulfur quercetin na misombo ya phenolic inayosaidia mwili kupambana na magonjwa na uchovu.
Eliasaph Mwana, Ofisa mtafiti lishe wa Taasisi ya Chakula na Lishe TFNC, anasema kitunguu saumu husaidia kuzuia maambukizi ya utumbo mapafu na sehemu za siri za wanawake.
Pia kinachangia kushusha shinikizo la damu kuondoa lehemu katika mishipa ya damu kuzuia kuharisha na kupunguza fangasi kinywani
‘’Kinapunguza maambukizi kwenye koo na hata katika mkanda wa jeshi,’’ anasema Mwana na kushauri kutumia kitunguu saumu kwa kiasi ikiwezekana punje zisizozidi sita kwa siku hasa kinapotumika kibichi
Gelagister Gwarasa, mtafiti na ofisa lishe Mwandamizi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwananyamala, anathibitisha faida hizi.
Anasema kitunguu saumu kinaimarisha kinga ya mwili na kupunguza baadhi ya dalili za maambukizi ya virusi vikiwamo vya Uviko-19. Uwezo huu unatokana na kemikali ya allicin inayopatikana pale kitunguu saumu kinapokatwa kupondwa au kutafunwa
Faida nyingine za kungo hiki ni kurekebisha shinikizo la damu na afya ya moyo, kupunguza maambukizi ya bakteria, baadhi ya virusi na fangasi hasa kwenye utumbo na mapafu na kusaidia uyeyushaji na ufyonzwaji wa chakula na pia kuzuia kuharisha
Kitunguu saumu kinaweza kuongezwa kwenye vyakula vingi ili kuongeza ladha . Kinaweza kutumika kizima kilichokatwa, kupondwa au kama unga.
Ushauri wa wataalamu
Gwarasa anashauri mtu mzima asitumie zaidi ya punje sita kwa siku. Ili kupata faida kamili wataalamu wa lishe wanashauri kutumia kitunguu saumu kibichi badala ya unga.
Aidha watu wenye mzio au wenye matatizo ya damu au wanaotumia dawa za kuyeyusha damu, wanapaswa kuwasiliana na wataalamu wa afya kabla ya kutumia
Elizabeth Lyimo, Ofisa lishe na mtafiti kutoka TFNC anasema vitunguu saumu vyote yaani vyeupe zambarau au pinki vina ubora sawa. Anaongeza kuwa kitunguu saumu kinaweza kutumika pia kusaidia kutuliza vidonda vya kooni kwa watu wenye maambukizi ya Ukimwi.
Kwa wanaotaka kutumia. Chukua punje nne za kitunguu saumu, kikombe kimoja cha maji na sukari au asali. Menya na katakata kitunguu, tia kwenye maji yanayochemka acha kichemke dakika 10
Epua funika na acha ipoe kisha ongeza asali au sukari kwa ladha. Kunywa kikombe kimoja kutwa mara tatu
Kitunguu saumu si tu kiungo cha ladha bali ni chanzo cha afya na nguvu za kinga mwilini
