Marufuku ya utoaji mimba inavyochochea soko haramu la siri-2Marufuku ya utoaji mimba inavyochochea soko haramu la siri-2

Dar es Salaam. Licha ya sheria dhidi ya utoaji mimba zinavyoendelea kubaki kali nchini, ndivyo biashara ya siri ya huduma hizo inavyozidi kujitanua kwa kasi nyuma ya pazia, ikiwahusisha wapatanishi, baadhi ya wahudumu wa afya, wafamasia na vituo visivyo rasmi vya matibabu.

Uchunguzi umebaini mazingira ya hofu, usiri na ukosefu wa njia salama za wazi, yamechangia kuibuka kwa soko haramu linalowanufaisha wanaoliongoza huku wanawake wakibeba gharama kubwa za kifedha na kiafya.

Huanza kama jitihada za kutafuta suluhisho la ujauzito usiotarajiwa, lakini huishia kuwa mnyororo wa biashara unaogharimu maelfu hadi mamilioni ya shilingi, na wakati mwingine maisha ya wanawake wenyewe.

Tofauti na huduma rasmi za afya, mtandao huo hufanya kazi bila risiti, kumbukumbu wala uwajibikaji wa wazi, lakini tayari umejijenga kama mfumo kamili unaounganisha maduka ya dawa, wapatanishi na watoa huduma wanaofanya kazi kwa siri.

Mahojiano yaliyofanywa na Mwananchi kwa wanawake waliowahi kupitia huduma hizo, wataalamu wa dawa na wahudumu wa afya, yameonesha kuwa hofu ya sheria na unyanyapaa imekuwa kichocheo kikubwa cha wanawake wengi kuingia kwenye mfumo huo wa chini kwa chini.

Alipoulizwa kuhusu tathmini ya Serikali juu ya utoaji mimba usio salama nchini, hususan Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Dk Ahmad Makuwani anasema utoaji mimba unaruhusiwa katika mazingira maalumu ya kitabibu pekee.

“Utoaji mimba unaruhusiwa pale ambapo kuna sababu za kitaalamu za kitabibu. Kwa maana hiyo, Tanzania hakuna utoaji mimba salama. Kwa kuwa utoaji mimba usio salama si jambo linalotambuliwa kisheria, hakuna tathmini rasmi ya kitaalamu iliyofanyika kuhusu suala hilo,” anasema.

Biashara inayokua kwa siri

“Mteja hapiti kwa mtu mmoja,” anasema mpatanishi aliyejitambulisha kwa jina moja la Rehema ambaye huwasiliana na wateja kupitia makundi ya WhatsApp.

“Tunamchukua hatua kwa hatua na kila mmoja anapata sehemu yake ya fedha.”

Anasema wanawake wengi wanaingia kwenye mfumo huo kwa sababu wanaogopa kwenda hospitali au kueleza hali zao waziwazi.

“Kila mtu anajua hairuhusiwi ndio maana mmoja akifahamu anampa taarifa mwingine juu ya namna ya kukwepa macho ya watu na mkono wa sheria,” anaongeza.

Anasema baadhi yao hupewa dawa za kutoa mimba huku wengine wakipelekwa kwenye huduma za ‘kusafishwa’, mara nyingi bila kukutana ana kwa ana na wataalamu waliothibitishwa.

“Mara nyingi kila kitu (hasa mipango ya namna ya kutimiza utoaji) kinamaliziwa kwa simu au WhatsApp,” anasema.

Anaeleza safari nyingi huanzia kwenye baadhi ya maduka ya dawa ambako dawa zinazohusishwa na utoaji mimba, ikiwamo Misoprostol, huuzwa bila agizo la daktari.

Kutoka hapo, wapatanishi huunganisha wanawake hao na watu wanaodai kutoa huduma hizo kwa siri.

Uchunguzi umebaini kuwa, wanawake wengi huanza kwa kutumia kati ya Sh40,000 hadi Sh100,000 kununua dawa, lakini gharama huongezeka kwa kasi matatizo yanapoanza.

Watu wanaohusika kwenye biashara hiyo wanasema moja ya sababu zinazolifanya soko hilo kuwa na faida kubwa ni usiri na uharamu wake.

“Jambo lolote ambalo sheria inakataza hua linakua na gharama sana. Dawa inayouzwa kati ya Sh30,000 hadi Sh50,000 kwa vidonge vitano. Lakini kwenye soko haramu bei hupanda hadi Sh150,000,” anasema mmoja wa watu wanaohusika kwenye biashara hiyo.

Rehema anakiri kuwa gharama mara nyingi haziishii kwenye malipo ya mwanzo.

“Kama mimba haitoki vizuri au mwanamke akaanza kutokwa damu mfululizo, tunamshauri kwenda kusafishwa na watu matibabu yanaanzia Sh150,000 hadi Sh300,000,” anasema.

 “Huduma za baada ya mimba kutoka ni bure lakini kwa sababu wanahofia kuulizwa wanajikuta wanabaki huku huku ili jambo liendelee kubaki siri lisifahamike na Serikali wala familia ya mhusika.”

Daktari mmoja anayefanya kazi nje ya mfumo rasmi anasema kadri hali inavyokuwa mbaya ndivyo gharama zinavyoongezeka.

“Unaweza kuanza na Sh150,000 lakini ikitokea damu nyingi au maambukizi, kiasi kinaweza kufika Sh500,000 au hata Sh1 milioni,” anasema.

Kwa wanawake wengi, kile kinachoonekana kuwa njia ya haraka ya kutatua tatizo hugeuka kuwa mzigo mkubwa wa kiafya na kifedha.

“Unalipa kimya kimya kwa sababu inakuwa siri kati yako na aliyekuuzia dawa,” anasema mfanyakazi mmoja wa famasi eneo la Kinondoni.

“Na wakati mwingine unalipia maisha yako.”

Waathirika wa mfumo wa siri

Mwanafunzi wa chuo kikuu kilichopo Dar es Salaam aliyejitambulisha kwa jina moja la Neema (22), anakumbuka siku aliyogundua ana ujauzito kama mwanzo wa mfululizo wa maamuzi ya hofu, baada ya kwenda hospitali ya umma akahofu kueleza shida yake.

Aliondoka bila msaada. Baadaye alielekezwa na wanafunzi wenzake kwa daktari mmoja aliyemwambia atalipa Sh150,000 “aliniambia tukutane usiku.”

Walikutana kwenye chumba kidogo Tandika. Baada ya malipo, alipewa dawa na maelekezo mafupi. Baada ya saa 24 baadaye alianza kuvuja damu nyingi. “Nilimpigia simu lakini haikupokewa,” anasema.

Hatimaye alikimbizwa Hospitali ya Mwananyamala akiwa katika hali mbaya.

Madaktari walibaini nimepungukiwa damu na ninahitaji kusafishwa haraka, kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya dawa. Familia ililazimika kukopa zaidi ya Sh300,000 kwa matibabu ya dharura.

“Niligundua nimelipa mara mbili mara ya kwanza kuhatarisha maisha yangu, mara ya pili kuokoa maisha yangu,” anasema kwa sauti ya chini.

Mzigo kwa sekta ya afya

Kwa wataalamu wa afya, visa kama vya Neema vinaakisi mzigo mkubwa unaobebwa na hospitali za umma.

“Matibabu ya matatizo haya ni ghali sana,” anasema Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama kutoka Hospitali ya misheni Ifakara, mkoani Morogoro, Elias Kweyamba. “Unahitaji damu, dawa za maambukizi, upasuaji na kulazwa muda mrefu.”

Tafiti mbalimbali za afya ya uzazi zinaonesha kuwa gharama ya kutibu matatizo ya utoaji mimba usio salama, inaweza kuwa mara kadhaa zaidi ya gharama ya kutoa huduma salama na kinga mapema.

Hali hiyo huifanya Serikali kubeba gharama kubwa za matibabu wakati biashara ya siri ikiendelea kuwanufaisha waendeshaji wake.

Athari za kiafya

Akizungumzia madhara ya kiafya ya utoaji mimba usio salama, daktari bingwa wa uzazi na magonjwa ya wanawake, Dk Isaya Mhando anasema wanawake wengi hupoteza maisha kabla hata ya kufikishwa hospitalini.

Anasema kutokwa damu nyingi ni moja ya sababu kuu, hasa pale mabaki ya ujauzito yanapobaki ndani ya mfuko wa uzazi.

“Maambukizi makali ya damu yanaweza kuanzia kwenye via vya uzazi na kusambaa haraka mwilini, hali inayoweza kusababisha mshtuko wa mwili na kifo,” anasema.

Anasema matumizi ya vifaa visivyo salama yanaweza kutoboa mji wa mimba na kuharibu viungo vya ndani.

Dk Mhando anasema baadhi ya madhara huendelea hata baada ya mgonjwa kupona.

“Maambukizi makubwa yanaweza kusababisha makovu ndani ya mji wa mimba au kwenye mirija ya uzazi na baadaye kusababisha ugumba,” anasema.

Sheria, kuongezeka kwa soko

Wataalamu wa uchumi wanaeleza biashara hiyo kama sehemu ya soko kivuli linalokua kutokana na mahitaji makubwa, usiri na mazingira ya kisheria.

“Kadri vizuizi vinavyoongezeka, ndivyo bei zinavyopanda,” anasema mchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Abel Kinyondo.

“Sheria inapoweka ukomo mkubwa kwenye huduma fulani huku mahitaji yakiendelea kuwepo, biashara huhamia chini kwa chini na kuwa haramu kabisa.”

Anasema biashara inapokuwa haramu hakuna usimamizi wa wazi wala udhibiti wa ubora wa huduma zinazotolewa.

Wakili wa kujitegemea, Peter Majanjala anasema hofu ya kuchukuliwa hatua za kisheria huwafanya wanawake wengi kuchelewa kutafuta msaada hospitalini.

“Wananchi wengi wanaamini wakifika hospitali wataripotiwa kwamba walitoa mimba,” anasema.

“Hofu hiyo ndiyo inayowasukuma wengi kwenda kutafuta suluhisho kwa siri na wakati mwingine kuchelewa kupata matibabu sahihi.”

Licha ya hatari zilizopo, watu wanaohusika kwenye mtandao huo wanasema biashara inaendelea kukua.

“Watu wanaendelea kuja na mtu akiwa na shida hiyo anaambiwa na rafiki zake wa chuoni, kazini au hata majirani zake nyumbani,” anakiri mmoja wa wapatanishi.

 “Kadri mahitaji yatakavyokuwepo, biashara hii haitaisha kwa sababu wenye uhitaji hawawazi kuhusu sheria wala hawaoni shida kutoa fedha, wanachokitaka ni kutokubaki na mimba zao kwa gharama yoyote.”

Itaendelea kesho

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *