Mahakama yaamuru aliyeshtakiwa kwa mauaji apelekwe taasisi ya afya ya akiliMahakama yaamuru aliyeshtakiwa kwa mauaji apelekwe taasisi ya afya ya akili

Arusha. Mahakama Kuu masjala ndogo ya Dar es Salaam, imeamuru Mgisha Leonard aliyekuwa akikabiliwa na shtaka la kumuua Rehema Mwanansori (17), kupelekwa gerezani au taasisi ya watu wenye changamoto ya afya ya akili kama mkosaji mwenye matatizo ya akili, baada ya kubaini kuwa alikuwa na matatizo ya akili wakati wa kutenda tukio hilo.

Aidha, imeagiza kwa mujibu wa kifungu cha 235 (4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), baada ya kuisha muda wa miaka mitatu kuanzia tarehe ya hukumu hiyo, Msimamizi wa gereza au taasisi ya afya ya akili atatoa ripoti ya maandishi kwa waziri kuhusu hali, historia na mazingira ya mshtakiwa.

Hukumu hiyo ilitolewa Mei 18, 2026 na Jaji Arnold Kirekiano na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa mahakama.

Baada ya kupitia ushahidi wa pande zote, Mahakama ilieleza ingawa ushahidi umeonyesha mshtakiwa ndiye aliyesababisha kifo cha marehemu, lakini kutokana na hali yake ya akili hakuwa na uwezo wa kuelewa ubaya wa kitendo alichofanya, hivyo hawezi kuwajibishwa kwa kosa hilo kwa mujibu wa sheria.

Mahakama iliagiza mshtakiwa kuwekwa gerezani au katika taasisi ya afya ya akili kama mkosaji mwenye matatizo ya akili, huku ikielekeza kuwa baada ya miaka mitatu mamlaka husika ziwasilishe ripoti kwa waziri kuhusu maendeleo ya afya yake na mazingira yake.

Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani, tukio hilo lilitokea Januari 24, 2025 katika eneo la Tanita, Kibaha mkoani Pwani.

Ilidaiwa kuwa siku hiyo Rehema alikwenda nyumbani kwa mshtakiwa kuchukua mboga ila katika mazingira ambayo hayakuelezwa kwa kina, mshtakiwa alianza kumfukuza marehemu huku akimpigia kelele.

Rehema alijaribu kukimbia lakini mshtakiwa alimfuata akiwa na kipande cha mbao na kumpiga kichwani, hali iliyomwacha akiwa amejeruhiwa vibaya.

Baada ya tukio hilo, mshtakiwa alijisalimisha mwenyewe kwa polisi.

Shahidi wa upande wa mashtaka, Sajenti Mohamed aliyekuwa askari Polisi Kibaha, alidai mahakamani kuwa siku ya tukio mshtakiwa alimfuata na kumweleza kuwa alikuwa amemuua mtu na alitaka akamatwe.

“Siku hiyo mshtakiwa alinijia akiwa na hofu na kuniambia nimfunge pingu kwa sababu alikuwa ameua mtu,” alidai shahidi huyo mahakamani.

Rehema alipelekwa Hospitali ya Tumbi kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Mloganzila kutokana na hali yake kuwa mbaya, lakini juhudi za madaktari kuokoa maisha yake hazikufanikiwa kwani alifariki dunia.

Shahidi wa tatu, Mayasa Ramadhan, aliyekuwa mpangaji mwenzake Rehema ambaye alishuhudia tukio hilo, aliiambia Mahakama kuwa alimwona mshtakiwa akimfukuza Rehema akiwa na kipande cha mbao mkononi ambacho alimpiga nacho kichwani.

Katika uchunguzi wa mwili uliofanywa Hospitali ya Tumbi, ulibainisha kuwa Rehema alikuwa na jeraha kubwa nyuma ya kichwa lililosababishwa na kitu butu.

Mahakama ilieleza ushahidi wa mashahidi wa macho pamoja na ripoti ya daktari ulithibitisha pasipo shaka kuwa Rehema alifariki kutokana na kipigo alichopewa na mshtakiwa.

Katika hatua za awali za kesi hiyo, wakili wa utetezi aliieleza Mahakama kuwa mshtakiwa alikuwa na matatizo ya akili, hivyo Mahakama iliamuru apelekwe katika Taasisi ya Afya ya Akili Isanga kwa uchunguzi wa afya ya akili.

Ripoti ya daktari kutoka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili ya Mirembe iliyowasilishwa mahakamani ilieleza kuwa mshtakiwa alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa akili, hakuwa na utulivu wa kiakili.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mshtakiwa hakuwa na uwezo wa kuelewa asili ya kitendo chake wakati wa tukio na pia hakuwa katika hali ya kumwelekeza vizuri wakili wake wakati wa mwenendo wa kesi.

Uamuzi Mahakama

Jaji Kirekiano amesema Mahakama iliridhika kuwa kifo cha Rehema kimethibitishwa kupitia ushahidi wa mashahidi pamoja na ripoti ya uchunguzi iliyobaini kuwa marehemu alifariki kutokana na jeraha kubwa la ubongo lililosababishwa na kipigo cha kitu butu kichwani.

Amesema ushahidi wa mashahidi wa macho ulionyesha kuwa mshtakiwa alimfukuza marehemu na kumpiga kwa kipande cha mbao kichwani kabla ya kukimbilia kwa askari polisi na kujisalimisha akidai ameua mtu.

Kwa mujibu wa jaji huyo, ushahidi huo uliithibitishia Mahakama kuwa mshtakiwa ndiye aliyesababisha kifo cha marehemu.

Hata hivyo, Jaji Kirekiano amesema Mahakama ilizingatia pia utetezi wa wazimu uliotolewa na mshtakiwa pamoja na ripoti ya kitabibu kutoka Taasisi ya Isanga iliyobaini kuwa alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa akili aina ya ‘schizoaffective disorder’ wakati wa tukio na hakuwa na uwezo wa kutambua ubaya wa kitendo chake.

“Mahakama imeridhika kwamba huu ni mwenendo unaostahili kutolewa uamuzi maalum kwamba ingawa kuna ushahidi alitenda kosa hilo, kutokana na wazimu wake hana hatia ya kosa hilo,” amesema Jaji Kirekiano.

Kutokana na mazingira ya tukio na vurugu zilizosababisha kifo hicho, Mahakama iliamuru mshtakiwa kuwekwa gerezani au katika Taasisi ya Afya ya Akili kama mkosaji mwenye matatizo ya afya ya akili.

Jaji amesema kwa mujibu wa kifungu cha 235(4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) baada ya miaka mitatu tangu kutolewa kwa amri hiyo, msimamizi wa gereza au taasisi ya afya ya akili atatakiwa kuwasilisha taarifa kwa waziri kuhusu hali ya mshtakiwa, historia yake pamoja na mwenendo wake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *