Wito kwa Waislamu siku kumi za Dhul-HijjaWito kwa Waislamu siku kumi za Dhul-Hijja

Dar es Salaam. Allah Mtukufu huchagua katika siku, miezi na nyakati kwa kuzifadhilisha Atakavyo; ikiwa ni rehema kutoka Kwake na ukumbusho kwa wenye kutafakari au kushukuru.

Katika neema za Allah kwa mja  ni kumwafikisha juu ya kutumia vizuri fursa za maisha yake. Maisha hupita na kuisha, na mwanaadamu hana sehemu yoyote ndani yake isipokuwa akiba ya matendo yake mema.

Allah Mtukufu amesema: “Na harakisheni msamaha wa Mola wenu Mlezi na Pepo ambayo upana wake ni mbingu na ardhi, iliyoandaliwa kwa wachamungu.” (3:133).

Basi mwenye furaha ya kweli ni yule anayetumia vizuri nyakati zake, akaongeza utiifu katika misimu ya kheri, na akajitafutia rehema za Allah Mtume wa Allah (Rehema na amani ziwe juu yake) amesema:

“Miguu ya mja haitasogea siku ya Kiyamah mpaka aulizwe: Kuhusu maisha yake aliyatumiaje, kuhusu elimu yake alifanyia nini, kuhusu mali yake aliipata wapi na aliitumia wapi, na kuhusu mwili wake aliuchosha katika nini?” Na Mtume  wa Allah alimwambia mtu mmoja akimnasihi: “Tumia vizuri mambo matano kabla ya mambo matano (hayajakufika): ujana wako kabla ya uzee wako, afya yako kabla ya maradhi yako, utajiri wako kabla ya ufukara wako, nafasi yako kabla ya shughuli zako, na maisha yako kabla ya mauti yako.”

Na katika siku zenye fadhila ambazo Allah Ameziinua hadhi yake na kuadhimisha jambo lake ni siku kumi za mwezi wa Dhulhijja (mfungo tatu), mwezi ambao Waislam duniani kote tumeuanza hivi karibuni na ndani yake kukiwa na Eid el Udh hiya au Eid ya kuchinja.

Hizi ni siku tukufu na zenye baraka; hakuna siku zinazolingana nazo wala hakuna ujira wa matendo unaolingana nazo. Mola wetu  Mtukufu ameziapia  (siku hizi) aliposema:

“Naapa kwa alfajiri, na kwa siku kumi (za mwezi wa Dhulhijja)” (89:1-2) Ibn ‘Abbās (Allah Amridhie) amesema: “Siku kumi ambazo Allah ameziapia ni za mwanzo wa Dhulhijja” Na hizi ndizo “siku maalumu” ambazo Allah amesema kuzihusu: “Ili washuhudie manufaa yao na walitaje jina la Allah katika masiku maalumu juu ya yale aliyowaruzuku katika wanyama wa mifugo…”  (22:28)

Allah Mtukufu amezipa siku kumi hizi ujira mkubwa na akaweka ndani yake kheri nyingi kwa wenye kufanya ibada. Kila tendo jema ndani yake linapendwa zaidi na Allah kuliko katika siku nyingine.

Mtume  wa Allah amesema: “Hakuna siku ambayo matendo mema ndani yake yanapendwa zaidi na Allah kuliko siku hizi kumi.” Masahaba wakauliza:“Ewe Mtume wa Allah! Hata jihadi katika njia ya Allah?” Akasema: “Hata jihadi katika njia ya Allah, isipokuwa mtu aliyetoka na nafsi yake na mali yake kisha hakurudi na chochote.”

Na katika riwaya nyingine: “Hakuna amali iliyo safi zaidi mbele ya Allah wala yenye ujira mkubwa zaidi kuliko kheri inayofanywa katika siku kumi za Adh-ha.” Siku hizi zimepewa fadhila hizi kwa sababu ndani yake hukusanyika mama wa ibada zote: Swala, Kufunga, Zaka na Hijjah  Na jambo hili halipatikani kwa ukamilifu katika nyakati nyingine.

Sadaka ni katika matendo makubwa zaidi katika siku kumi za Dhulhijja. Ibn Al-Qayyim amesema: “Sadaka ina athari ya ajabu katika kuondoa misiba na majanga, hata ikiwa imetolewa na mtu muovu, dhalimu au hata kafiri. Hakika Allah huondoa kwa sababu yake aina mbalimbali za balaa.

Hili ni jambo linalojulikana kwa watu wote, wa kawaida na wa pekee, na watu wote duniani wanalikubali kwa sababu wameliona kwa uzoefu.” Sadaka ni katika matendo yanayopendekezwa mwaka mzima, kwa hiyo ujira wake katika misimu ya ibada huwa mkubwa zaidi.

Na katika matendo yanayopendekezwa katika siku hizi kumi  ni kuchinja (udhhiya) mnyama katika wanyama wa mifugo kama ngamia, ng’ombe na kondoo kwa kujikurubisha kwa Allah Mtukufu. Allah Mtukufu amesema: “Nyama zake wala damu zake hazimfikii Allah, lakini kinachomfikia ni ucha Mungu kutoka kwenu.” [22: 37]

Ndani yake pia kuna kufufua Sunna ya Nabii Ibrahim pale alipomfidia mwanawe Ismail kwa kuchinja dhabihu. Kuchinja ni bora zaidi kuliko kutoa thamani ya mnyama wa udhhiya kama sadaka.

Na Udhhiya ya kondoo mmoja inatosha kwa mtu pamoja na watu wa nyumba yake wote aliowakusudia, wawe hai au wamefariki. Na watu saba wanaweza kushirikiana na kuchinja ngamia au ng’ombe inatosha kwa kiwango kinachotosha kondoo mmoja.

Ama watu wawili au zaidi kushirikiana kumiliki kondoo mmoja kwa Udhhiyah, jambo hilo halikupendekezwa kisharia.

Katika mambo yanayopendekezwa katika siku hizi pia ni kufunga, kwani ni katika ibada bora kabisa. Na yule ambaye hakuweza kufunga siku zote, basi asikose kufunga Siku ya Arafaa, kwani imepokewa kuhusu ubora wake mkubwa.

Mtume amesema: “Kufunga Siku ya ‘Arafa, ninatarajia kwa Allah kuwa kutafuta madhambi ya mwaka uliopita na mwaka unaofuata.” (Muslim).

Pia amesema: ‘’Kufunga Siku ya Arafa ni sababu ya kufutiwa madhambi ya miaka miwili. Hakuna siku ambayo Allah huwaokoa watu wengi zaidi kutoka motoni kuliko Siku ya Arafa.” (Muslim).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *