
Njombe. Kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa, Wazo Mwang’onda ameagiza wadau wa misitu Tanzania kuendelea kuwahamasisha wananchi juu ya utunzaji wa mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Amewataka wananchi katika Wilaya ya Makete kuhifadhi mazingira kwa kuendelea kupanda miti ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ukisisitiza kuepuka ukataji wa miti ovyo kwa ajili ya kuni na mkaa na badala yake watumie nishati mbadala.
Mwang’onda ameyasema hayo leo Mei 22, 2026 wakati akikagua banda la mradi wa uendelezaji misitu chini ya ufadhili wa Serikali ya Finland na Tanzania Iwawa, Makete mkoani Njombe.
Amesema wadau wa misitu ni watu muhimu katika kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi na kuhamasisha utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti kwa wingi ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Amesema katika kuhamasisha nishati safi na salama wananchi wanatakiwa kupanda miti kwa ajili ya kuhifadhi mazingira na kutumia mkaa mbadala na kuni poa kwa ajili ya kulinda afya zao na kuhifadhi mazingira.
“Kwa hiyo tuachane kabisa kukata miti pamoja na kutumia kuni na mkaa, kwa kufanya hivyo tutahifadhi mazingira yetu,” amesema Mwang’onda.
Amewataka wananchi kuhamia katika matumizi ya mabaki ya mawe pamoja na kuni poa kama sehemu ya nishati safi ya kupikia ili kutunza mazingira na kuepuka ukataji ovyo wa miti.
Mkufunzi kutoka Chuo cha Misitu na Viwanda Vya Misitu akiwakilisha mradi wa Forland, Freeman Masawe amesema wamefika Makete kwa ajili ya kutoa elimu ya namna ya kuhudumia misitu yao pamoja na kuchakata bidhaa itokanayo na misitu.
Amesema wapo kwa ajili ya kuhamasisha na kuchochea matumizi ya nishati mbadala ambayo inatokana na vumbi la mbao ambapo Wilaya ya Makete shughuli za uchakataji wa mazao ya mbao zinafanyika kwa wingi.
“Hivyo taka zinabaki nyingi msituni sisi tuna lengo la kuhamasisha uongezaji wa thamani kwa kutumia hizo taka zitokanazo na misitu tunaweza kupata nishati mbadala ambapo tunaongeza kipato cha mwananchi na kuokoa ukataji miti ovyo,” amesema Masawe.
Mtaalamu wa Misitu na Viwanda vya Misitu kupitia mradi wa Forland, Carlen Rite amesema mpaka sasa wamewafikia wakulima kwenye mikoa minne yenye halmashauri 19.
Amesema moja ya halmashauri hizo ni Makete ambapo mpaka sasa wana vikundi 16 wanafanya navyo kazi vikiwa na mchanganyiko wa wanawake na wanaume.
“Tumeanzisha mashamba 19 ambayo ni ya mbegu bora ili kufupisha muda wa mti kukua,” amesema Rite.
Mkazi wa Makete, Samwel Mhema amesema elimu waliyoipata inakwenda kuwanufaisha kwani wataenda kuboresha misitu yao kwa kupanda mbegu za kisasa ambazo zitawasaidia kujipatia kipato kwa muda mfupi.
“Hii elimu ambayo nimeipata hapa ni muhimu kwani itaniongezea katika kuzalisha mbegu na kupanda miti,” amesema Mhema.
