DCEA yateketeza kilo 504 za heroini MtwaraDCEA yateketeza kilo 504 za heroini Mtwara

Mtwara. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, imeteketeza kilo 504.36 za heroini zilizokamatwa kutoka kwa raia saba wa Iran katika Bahari ya Hindi ndani ya eneo tengefu la kiuchumi wilayani Kilwa, Mkoa wa Lindi.

Uteketezaji huo umefanyika leo Mei 23, 2026 kufuatia amri ya Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara iliyotaka vielelezo hivyo vilivyokamatwa kati ya Aprili 22 na 24, 2021 viharibiwe rasmi.

Akizungumza wakati wa shughuli hiyo, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali kupambana na biashara ya dawa za kulevya inayotishia usalama wa Taifa na afya ya jamii.

Amesema awali mamlaka hiyo pia iliteketeza kilo 355 za methamphetamine kutokana na dawa hizo kuwa katika mfumo unaoyeyuka haraka zinapopata joto.

“Mahakama ilitoa kibali cha kuziharibu mapema kwa kuwa huharibika kirahisi,” amesema Lyimo.

Amesema ukamataji wa dawa hizo ulifanikiwa kupitia ushirikiano wa vyombo vya dola baada ya watuhumiwa kukamatwa baharini wakisafirisha shehena hiyo kuingia nchini. Lyimo amesema ukanda wa pwani wa Mtwara, Lindi, Dar es Salaam na Tanga kwa miaka mingi umekuwa ukitumika kuingiza dawa za kulevya nchini, lakini sasa DCEA imeimarisha doria, ukusanyaji wa taarifa za kiintelijensia na matumizi ya teknolojia za kisasa kubaini majahazi yanayobeba dawa hizo.

“Tumefanikiwa kukamata majahazi kadhaa hali iliyopunguza upatikanaji wa heroini nchini,” amesema.

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha huduma za matibabu kwa waathirika wa dawa za kulevya kupitia ujenzi wa vituo vya MAT Clinic na sober houses mkoani Mtwara.

Lyimo ametoa onyo kwa wasafirishaji wa dawa za kulevya kuacha shughuli hizo akisema wataendelea kukamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Pia amewataka wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa mamlaka ili kusaidia kukamatwa kwa wahusika wa biashara hiyo haramu.

Meneja Mahusiano wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote, Mariamu Kawaga amesema dawa hizo ziliteketezwa kwa kutumia kinu maalumu chenye nyuzi joto 1,500 ambacho kina uwezo wa kuziharibu kabisa bila kuathiri mazingira.

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 12657/2025, raia mmoja wa Iran amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha dawa hizo huku wengine sita wakiachiwa huru.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *