Dar es Salaam. Mwili wa mfanyabiashara wa asili ya China, Bhaozang Ge unatarajiwa kuchomwa moto kesho Mei 24, 2026 katika eneo maalumu la Makumbusho jijini Dar es Salaam, na majivu yake kusafirishwa kwenda China kwa taratibu nyingine za mazishi kwa mujibu wa mila za familia yake.
Katika simulizi ya huzuni na kumbukizi, mdogo wa marehemu, Baosheng Ge maarufu Denis amesema kaka yake huyo aliyefariki akiwa na umri wa miaka 50, hakupenda kuitwa “Mchina” kwa kuhofia ubaguzi, akimtaja kuwa alikuwa tegemeo kubwa la familia pamoja na watu waliomzunguka.
Mbali na Denis, Mbunge wa Geita, Joseph Kasheku maarufu ‘Musukuma’, aliyekuwa miongoni mwa waombolezaji kwenye msiba huo amesema kifo cha mfanyabiashara na mwekezaji huyo kina utata mkubwa, huku akivitaka vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.
Familia ya marehemu Bhaozang Ge ikimfariji mmoja wa wafanyakazi wa kiwanda hicho, baada ya kuelezea namna walivyoishi na kufanya kazi na marehemu.
Denis amesema Bhaozang Ge aliamini watu wote ni sawa licha ya tofauti za rangi.
“Alikuwa anasema binadamu wote ni sawa, tofauti kubwa iliyopo ni rangi tu. Hakupenda kabisa masuala ya ubaguzi wa rangi,” amesema Denis.
Pia amesema kaka yake alikuwa na moyo wa kusaidia watu waliokuwa na matatizo mbalimbali, ikiwemo kuwasaidia wanafunzi waliokuwa wakikabiliwa na changamoto za ada za shule na mahitaji mengine ya msingi.
Amesema alikuwa akiguswa na matatizo ya watu na kwamba wapo wengi aliowasaidia kulipa ada za shule na wengine kuwainua katika maisha yao.
Mbunge wa Geita, Joseph Kasheku Musukuma (wa pili kutoka kushoto), akiwa katika msiba wa mmiliki wa kiwanda cha XIL LI.
Denis amesema tangu akiwa mdogo, kaka yake alikuwa mtu mwenye bidii, aliyependa elimu pamoja na kazi, hali iliyomsaidia kujijengea maisha na baadaye kuanzisha shughuli za biashara zilizokuwa msaada kwa watu wengi.
Kwa upande wake, Musukuma amesema taarifa alizozipata zinaonyesha kuwa marehemu alikuwa akiishi Tanzania kwa muda mrefu na alikuwa na uhusiano mzuri na Watanzania wengi, hali inayofanya tukio hilo kuwa la kusikitisha na kuibua maswali mengi.
“Dunia ya sasa ni kijiji. Huyu mtu alikuwa kama Mtanzania kwa sababu ameishi hapa muda mrefu, alikuwa anaongea Kiswahili na alikuwa na marafiki wengi wanaofanya kazi naye,” amesema Musukuma.
Mbunge wa Geita, Joseph Kasheku Musukuma (wa pili kutoka kushoto), akiwa katika msiba wa mmiliki wa kiwanda cha XIL LI.
Pia amesema kumekuwa na taarifa mbalimbali kuhusu mazingira ya kifo hicho, huku baadhi ya watu wakidai walinzi walihusika na tukio hilo.
“Hiki ni kitendo ambacho si kizuri kwa nchi yetu, hasa kwa wageni. Serikali inafanya jitihada kubwa kuwashawishi watu waje kuwekeza Tanzania. Matendo kama haya yanakatisha tamaa na lazima yakomeshwe,” amesema.
Amelihimiza Jeshi la Polisi kuhakikisha uchunguzi unafanyika kwa haraka na kwa umakini ili waliohusika wakamatwe na sheria ichukue mkondo wake.
Katika hatua nyingine, Musukuma amegusia suala la makundi ya vijana wanaotembea na silaha za jadi, akisema ni muhimu vyombo vya usalama kuchukua hatua dhidi ya tabia zinazoweza kuhatarisha usalama wa wananchi.
“Siwezi kusema ni jamii fulani kwa sababu nina marafiki wengi wa Kimasai, lakini kuna baadhi ya watu wenye tabia ya kutembea na mapanga, visu na silaha nyingine. Serikali na Jeshi la Polisi lazima vifanye uchunguzi na kudhibiti tabia hizi,” amesema.
Mfanyakazi wa kampuni hiyo, Crispin Massawe, ambaye amefahamiana na marehemu tangu mwaka 2017, amesema mara ya mwisho alipowasiliana na bosi wake alimpa taarifa za kupata mtoto.
“Nimeumizwa na msiba huu kwa sababu Ijumaa kabla ya kifo chake niliongea naye na kumpa taarifa za kupata mtoto. Aliniambia, ‘Njoo kesho ofisini uchukue zawadi,’ lakini nafika hapa nakutana na tukio la mauaji. Kiukweli nimeumia mno,” amesema Massawe.
Naye Eveline Mhina amesema aliwahi kupewa msaada wa Sh24 milioni kwa ajili ya kuanzisha biashara, lakini hakufanikiwa kuendesha biashara hiyo.
Amesema aliporudi tena kwa mwajiri wake, alipokewa vizuri na kupewa nafasi ya kurejea kazini.
Wafanyakazi wakiwa katika hali ya huzuni wakitoa machozi baada ya kusikiliza shuhuda za wenzao pamoja na mdogo wa marehemu Bhaozang Ge, mmiliki wa kiwanda cha XIL LI, kuhusu namna walivyoishi na kufanya kazi na marehemu.
“Bosi alikuwa na moyo wa kipekee. Nilipotaka kuanzisha biashara alinisaidia kwa kunipa kiasi kikubwa cha Sh24 milioni na hakuwahi kunidai. Hata niliposhindwa biashara, aliniambia nirudi kiwandani kufanya kazi. Nilirudi kwa aibu kwa sababu sikuwa na namna,” amesema.
Mwakilishi wa Halmashauri ya Ubungo kutoka Idara ya Mazingira na Usafi, Grace Nnembuka amesema Bhaozang alikuwa msaada mkubwa katika utunzaji wa mazingira na walikuwa wakishirikiana naye katika hatua mbalimbali zinazohusiana na mazingira.
“Tunajua kwa sasa makopo ni dili, na hii yote ni kwa sababu wapo watu wanaonunua makopo hayo na kusaidia kutunza mazingira. Zamani yalikuwa yanachangia kuziba mitaro na kuwa chanzo cha mafuriko, lakini sasa makopo yamekuwa adimu,” amesema Grace.
