Wanawake 150 wa jamii za kifugaji wapatiwa hati za kimila ManyaraWanawake 150 wa jamii za kifugaji wapatiwa hati za kimila Manyara

Manyara. Wanawake 150 kutoka jamii za wafugaji wilayani Simanjiro na Kiteto mkoani Manyara wamekabidhiwa hati za kimila za umiliki wa ardhi, hatua inayolenga kuwawezesha kiuchumi na kupunguza changamoto za mila na desturi zinazowanyima wanawake haki ya kumiliki ardhi.

Hati hizo zilikabidhiwa jijini Arusha katika hafla iliyofanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 25 ya shirika la Maasai Women Development Organization (Mwedo), ambalo limekuwa likishirikiana na serikali kuimarisha haki za wanawake na watoto wa kike katika jamii za wafugaji.

Mmoja wa wanufaika, Helena Isaya kutoka Kijiji cha Naisinyai wilayani Simanjiro, amesema hatua hiyo imeleta matumaini mapya kwa wanawake waliokuwa wakikumbana na changamoto za umiliki wa ardhi kutokana na mila na desturi kandamizi.

“Tunashukuru sana kwa kupata hati hizi kwa sababu awali tulikuwa tunanyanyasika sana. Hata kama umewekeza kwenye eneo, bila hati miliki ulikuwa unaweza kupokonywa wakati wowote. Sasa tuna uhakika wa kumiliki na kuendeleza maeneo yetu,” amesema.

Mwanufaika mwingine, Suzan Lembris, amesema hati hizo zitamuwezesha kumiliki ardhi kisheria na kufanya maendeleo bila hofu ya kupokonywa kutokana na mila zilizokuwepo katika jamii zao.

Ofisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, Valence Huruma, amesema ingawa sheria ya ardhi inatoa haki sawa kwa wananchi wote, mila na desturi zimekuwa kikwazo kikubwa kwa wanawake wa jamii za wafugaji kupata na kumiliki ardhi.

Amesema ushirikiano kati ya Serikali na wadau mbalimbali umeendelea kusaidia kuongeza uelewa wa jamii kuhusu haki za wanawake kumiliki na kutumia ardhi kwa maendeleo yao binafsi na ya kijamii.

Mkurugenzi wa Mwedo, Ndinini Kimesera, amesema utoaji wa hati hizo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 25 ya shirika hilo, ambalo limejikita katika kuwawezesha wanawake, watoto wa kike na jamii za wafugaji kupitia elimu, afya na uchumi.

Amesema shirika hilo limefanikiwa kuwasaidia zaidi ya wasichana 2,000 kupata elimu, ambapo baadhi yao sasa ni wataalamu katika fani za sheria, udaktari na uuguzi.

 Wakili Elifuraha Laltaika amesema uwezeshaji wa wanawake ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa, akisisitiza kuwa kumuwezesha mwanamke ni kuijenga jamii nzima.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *