
Tarime. Mwili wa mtoto wa kike anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 13 hadi 15 umeokotwa ukiwa unaelea kwenye maji ya Mto Mori, eneo la Kata ya Nyakonga, Wilaya ya Tarime mkoani Mara.
Mwili huo ambao umepatikana ukiwa umeanza kuharibika, umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime kusubiri taratibu zingine.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Jumapili Mei 24, 2026, Diwani wa Nyakonga, Dorisi Chacha amesema hadi sasa hakuna ndugu waliojitokeza kuutambua mwili huo na kwamba kwa mujibu wa wataalamu, mwili huo unaonekana kukaa majini kwa zaidi ya siku 10.
“Huu mwili ulipatikana Jumamosi asubuhi, wakati huo kuna vijana wawili walikuwa pale mtoni wakichota mchango, ghafla wakaona mwili unaelea majini ukienda uelekeo wa maji, ndipo wakafanya jitihada za kuuopoa na walipomaliza wakatoa taarifa na mimi mwenyewe nilifika eneo la tukio,” ameeleza.
Amesema walitoa taarifa polisi ambapo askari walifika katika eneo hilo na kuuchukua mwili na kwenda kuuhifadhi kwa ajili ya taratibu zingine.
Amesema kutokana na Mto Mori kupita katika maeneo mengi ndani ya Wilaya ya Tarime na hata nchi jirani ya Kenya, kuna uwezekano wa mwili huo kuwa umetoka mbali na kata yao, hivyo ametoa wito kwa wakazi wote wanaopakana na mto huo kutoa taarifa kwa wenzao mwili uweze kutambuliwa na hatimaye kuzikwa.
“Mto umepita katika vijiji vingi, yawezekana huu mwili ukawa umetoka mbali na ndugu wasiwe na taarifa, kupitia habari hizi, nitoe ombi kwa wale wanaoshi kandokando ya mto kupeana taarifa ili kusaidia kupatikana kwa ndugu wa marehemu ili wafike Tarime na kumchukua mpendwa wao kwa ajili ya mazishi,” amesema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tarime/Rorya, Mark Njera amesema bado hajapata taarifa kuhusu tukio hilo yupo safarini na kuahidi kutoa taarifa baadaye.
“Niko safari, naomba nifuatilie, nitakupa mrejesho,” amesema Kamanda Njera.
