Chanzo cha picha, Afp via Getty
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema amewaagiza wapatanishi wa Marekani “kutoharakisha kufikia makubaliano” na Iran, baada ya hapo awali kuashiria kuwa pande hizo zilikuwa karibu kufikia mwafaka.
Makubaliano yanayojadiliwa yanaripotiwa kujumuisha kuongezwa kwa usitishaji mapigano kwa siku 60, kufunguliwa tena kwa Mlango Bahari wa Hormuz, pamoja na mpango wa kuendelea na mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Trump alisema mazungumzo yanaendelea kwa “mtazamo chanya”, lakini akasisitiza kuwa:
“Pande zote mbili zinapaswa kuchukua muda wao na kuhakikisha kila jambo linafanyika kwa usahihi.”
Siku ya Jumamosi, Trump alisema kuwa makubaliano hayo yalikuwa “kwa kiasi kikubwa yamejadiliwa”, hali iliyozua matarajio kwamba tangazo rasmi lingeweza kutolewa wakati wowote.
Kwa upande wake, maafisa wa Iran pia wameashiria kuwepo kwa maendeleo katika mazungumzo hayo. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei, alisema kuwa pande hizo mbili ziko:
“Karibu sana sio mbali sana” kufikia makubaliano.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Marekani, makubaliano yanayojadiliwa kwa sasa si suluhisho la mwisho, bali yanaacha baadhi ya masuala magumu zaidi yaamuliwe katika mazungumzo ya baadaye.
Masuala hayo ni pamoja na matakwa ya Iran ya kuondolewa vikwazo vya kiuchumi, kurejeshewa fedha zake zilizozuiwa nje ya nchi, pamoja na shinikizo la Washington kwa Iran kupunguza shughuli zake za nyuklia.
Ripoti hizo pia zinasema kuwa mapendekezo ya makubaliano hayo yamezua mgawanyiko ndani ya Chama cha Republican, huku baadhi ya wanachama wakidai kuwa masharti yake yanaipa Iran nafuu kubwa kupita kiasi.
Pia unaweza kusoma:
