
Spika wa bunge nchini Senegal El Malick Ndiaye, ametangaza kujiuzulu, uamuzi ambao unaiweka nchi hiyo kwenye sintofahamu ya kisiasa.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Uamuzi wa Ndiaye, unakuja baada ya wiki iliyopita rais Bassirou Diomaye Faye kumfuta kazi Waziri Mkuu Ousmane Sonko na kulivunja baraza la Mawaziri.
Aidha, uamuzi huu unamsafishia njia Sonko kuwania nafasi ya Uspika, katika bunge ambalo chama chake cha Pastef kina idadi kubwa ya wabunge.
Tayari wabunge katika taifa hilo la Afrika Magharibi, wameitisha kikao siku ya Jumanne, ili kumrejesha Sonko kama mbunge na kumchagua Spika mpya.
Wachambuzi wa siasa wanasema, iwapo Sonko atachaguliwa Spika, rais Faye atakuwa na wakati mgumu sana kupitisa mipango ya serikali yake bungeni, na hivyo kukwamisha baadhi ya ajenda zake.
Miezi ya hivi karibuni, rais Faye na Sonko wameonekana wakitofautiana kuhusu masuala mbalimbali ya namna ya kuongoza nchi hiyo, licha ya wawili hao kuonekana kuwa washirika wa kisiasa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2024.
Rais Faye alichaguliwa rais wa Senegal kwa sababu ya uungwaji mkono mkubwa wa Sonko, ambaye bado anaonekana kuwa na ushawishi mkubwa nchini humo na sasa maswali yanaulizwa kuhusu uwezo wa kiongozi huyo kuongoza kwa utulivu bila ya uugwaji mkono wa chama tawala.
