Mfumo wa elimu ya umma unavyojenga tabakaMfumo wa elimu ya umma unavyojenga tabaka

Dar es Salaam. Katika Shule ya Msingi Sinza iliyopo Wilaya ya Ubungo, dhana ya usawa wa fursa, imebaki kuwa kauli tu, huku uhalisia wake ukitenganishwa na ukuta unaoonekana kwa macho na pia kwa maana ya kijamii.

Upande mmoja wa shule hiyo kuna mkondo mpya wa Kiingereza ulioboreshwa, wenye madarasa ya kisasa, mazingira safi na mandhari yanayovutia.

Lakini upande mwingine, uliobaki na mfumo wa Kiswahili, bado unaendelea kubeba sura ileile ya changamoto za muda mrefu zinazolikumba Taifa katika sekta ya elimu ya umma.

 Ndani ya eneo moja la shule ya Serikali, kuna mgawanyiko unaodhihirisha wazi kuzaliwa kwa mfumo mpya wa elimu wa matabaka mawili nchini.

Hali hiyo ya Sinza si tukio la kipekee tena. Utafiti wa kawaida uliofanywa Wilaya ya Kinondoni umeonesha kuwa, idadi ya shule za msingi za Serikali zinazotumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia imeongezeka kutoka shule moja pekee mwaka 2021 hadi zaidi ya shule kumi mwaka 2026.

Kwa kiwango cha kitaifa, mahitaji ya shule hizo yameongezeka kwa kasi kubwa. Aprili 2025, Serikali ilikuwa tayari inamiliki shule 68 za aina hiyo nchini kote.

Ingawa hatua hiyo imekuwa ikiwasilishwa kama ishara ya maendeleo na mageuzi ya elimu, wadau mbalimbali wanaonya hali hiyo kuwa, inaibua mgawanyiko rasmi wa kitabaka ndani ya mfumo wa elimu ya umma.

Mkazi wa Sinza, Sophia Amoni anaeleza hali ya wazazi wengi wa kipato cha kati wanaojikuta katikati ya mfumo huo mpya.

“Siku zote nilitamani mwanangu asome shule yenye elimu bora, lakini shule binafsi zilikuwa nje ya uwezo wangu,” anasema.

Kwake, mkondo wa Kiingereza ndani ya shule ya Serikali ni kama tumaini jipya, licha ya ada ya Sh400,000 kwa mwaka.

Hata hivyo, jirani yake, Juma Amos mfanyabiashara mdogo wa Kimara, anasema kiwango hicho cha fedha ni mzigo usiowezekana.

Anasema watoto wake wameendelea kubaki upande wa Kiswahili, wastani wa kitaifa wa wanafunzi darasani ni mwanafunzi 72 kwa darasa moja, tofauti na wenzao wa mkondo wa Kiingereza wanaonufaika na uwiano wa wanafunzi 47 pekee kwa darasa, huku wakitenganishwa kwa umbali wa mita chache tu.

Katika Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma, hali hiyo ya tofauti za kielimu inaonekana kwa namna ya kusikitisha zaidi, huku vikwazo vya kujiunga vikiwa vikubwa zaidi.

Shule ya Msingi ya Serikali ya Bahi English Medium inawataka wazazi kulipa Sh250,000 kama mchango wa chakula na kiasi kingine cha Sh250,000 kama ada ya kujiunga.

Katika mazingira ambayo elimu ya msingi inapaswa kuwa ya bure kwa mujibu wa Katiba na sera za Taifa, gharama hizo zimekuwa kikwazo kinachowabagua wananchi wengi ambao mfumo wa elimu ya umma ulipaswa kuwahudumia bila ubaguzi.

Zaidi ya hapo, shule hiyo imeweka utaratibu wa kuongea Kiingereza pekee, ndani ya mazingira ya shule, jambo ambalo wakosoaji wanasema linajenga hisia potofu kwamba Kiswahili ni lugha ya hadhi ya chini au isiyofaa kwa elimu bora.

Mwaka 2024 aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais(Tamisemi), Mohamed Mchengerwa, aliwahi kutetea mwelekeo huo wakati wa uzinduzi wa Shule ya Msingi ya Chief Zulu English Medium mjini Songea.

Akiwa mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo, alisema shule hiyo iliyojengwa kwa Sh626.4 milioni kutokana na mapato ya ndani ya manispaa, imelenga kuwasaidia wazazi wanaotaka huduma bora za elimu ya Kiingereza kwa gharama nafuu zaidi ukilinganisha na shule binafsi.

Alieleza pia, shule hiyo inatoa mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kwa vitendo pamoja na lugha ya Kifaransa ili kuwaandaa wanafunzi kuhimili ushindani wa soko la dunia.

Hata hivyo, wataalamu wa saikolojia ya watoto wanaonya mgawanyiko huo wa kimazingira na kijamii unaweza kuwa na athari za muda mrefu kwa ukuaji wa watoto.

Gharama za kisaikolojia

Mwanasaikolojia wa watoto kutoka Dar es Salaam, Dk Amina Mrema anasema watoto wanapolazimika kuingia katika milango tofauti ndani ya shule moja kulingana na uwezo wa kifedha wa wazazi wao, hali hiyo hujenga hisia za kitabaka tangu wakiwa wadogo.

“Mtoto mmoja anaonekana wa kundi la ‘walio nacho’ na mwingine wa kundi la ‘wasio nacho’. Hilo linaweza kuibua chuki, kujiona duni na kuporomoka kwa hali ya kujiamini kwa watoto wanaohisi wamewekwa pembeni,” anasema.

Anaongeza watoto wanafundishwa tangu umri wa miaka sita kwamba thamani yao katika jamii inategemea uwezo wa wazazi wao kulipia michango ndani ya Serikali ambayo kimsingi wote wanapaswa kuwa na haki sawa nayo.

Ukubwa wa tatizo hilo unaonekana zaidi kwenye takwimu. Shule za Serikali za mkondo wa Kiingereza zina wastani wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 47, wakati shule nyingi za Kiswahili zina mwalimu mmoja kwa wanafunzi 70 au zaidi.

Kupitia mfumo huo wa matabaka, Serikali inaonekana kuweka mazingira yanayoweza kwenda kinyume na Ibara ya 11 ya Katiba ya Tanzania inayotamka haki ya kila mwananchi kupata fursa sawa ya elimu.

Kwa mujibu wa makundi mbalimbali ya wadau waliohusika katika uchunguzi wa mfumo huo wa tabaka mbili, unaendelea kuzalisha aina mbili tofauti za Watanzania ndani ya taasisi moja ya umma.

Akichangia mjadala huo, Mwanasaikolojia wa Elimu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Robert Mbele anasema kuna tofauti kubwa kati ya malengo ya mtalaa mpya wa elimu na hali halisi inayotekelezwa mashuleni.

Anaeleza wakati mtalaa wa Taifa unalenga kujenga ujuzi wa karne ya 21 kama ushirikiano, uwajibikaji wa kijamii na uwezo wa kufanya kazi kwa pamoja, mfumo wa sasa wa kuwatenganisha wanafunzi kwa misingi ya uwezo wa kifedha wa wazazi wao, unaharibu malengo hayo.

“Ushirikiano unahitaji watoto wa mazingira tofauti kujifunza pamoja, kushirikiana kutatua changamoto na kuelewana kijamii. Ukianza kuwatenganisha kwa msingi wa uwezo wa wazazi wao kulipa, siyo tu unatenganisha madarasa, bali pia unadhoofisha ukuaji wa ujuzi wa kijamii na kihisia ambao sera yenyewe inadai kuupa kipaumbele,” anafafanua.

Dk Mbele anaongeza kuwa, kile kinachoitwa elimu bora katika mikondo ya Kiingereza mara nyingi hufunika ukweli kwamba, hata wahitimu wengi wa mfumo mzima wa elimu bado wanakosa ubunifu na uwezo wa kutatua matatizo, kwa sababu mifumo ya msingi kama mafunzo bora kwa walimu na mazingira jumuishi ya kujifunzia bado ni dhaifu.

Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya elimu, Dk Thomas Jabir anasema mvuto mkubwa wa shule za Serikali za English Medium haupo kwenye Kiingereza, bali unatokana na ukweli kwamba, Serikali imeamua kupeleka miundombinu bora kwa kundi dogo la shule hizo huku nyingine zikibaki nyuma.

Wakati elimu bora inapogeuzwa bidhaa ya wenye uwezo

Wakati wanafunzi milioni 5.38 nchini wanalazimika kukaa nje ya madarasa kutokana na uhaba wa nafasi, shule zile chache za mkondo wa Kiingereza zinaendelea kupewa kipaumbele katika matumizi ya mapato ya ndani ya halmashauri.

“Badala ya kuunda matabaka ndani ya elimu ya umma, Serikali inapaswa kuboresha shule zote kwa kiwango sawa,” anasisitiza Dk Jabir.

Mchanganuo wa changamoto za kielimu zinazoweza kujitokeza kutokana na mgawanyiko huo, unaoelezewa kwa kina na Richard Mabala, mdau mkongwe wa masuala ya elimu.

Anaonya kuwa, walimu wa sekondari watakabiliwa na kazi ngumu sana watakapopokea wanafunzi wa kidato cha kwanza kutoka katika mifumo miwili tofauti kabisa ya lugha na mazingira ya kujifunzia.

“Mwalimu hawezi kwenda kasi sana kwa sababu atawaacha nyuma waliotoka na mfumo wa Kiswahili. Lakini pia hawezi kwenda taratibu sana kwa sababu wale waliotoka English Medium wataona anawachelewesha,” anasema Mabala. “Katika mazingira kama hayo, tunawezaje kusema kuna usawa wa fursa katika elimu?”

Kadri idadi ya shule hizi inavyoendelea kuongezeka, Serikali inaendelea kuwa katika hatari ya kukiuka Ibara ya 11 ya Katiba inayohakikisha kila mwananchi anapata fursa sawa ya elimu.

Kupitia mfumo huu mpya wa matabaka ndani ya shule za umma, Taifa linaelekea kuzalisha makundi mawili tofauti ya Watanzania ndani ya taasisi moja ya Serikali, kundi la wasomi wanaotumia Kiingereza na kundi kubwa la wananchi wanaobaki katika mazingira duni ya mfumo wa Kiswahili.

Itaendelea kesho

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *