UDSM yawaita wadau kutafakari fikra za Mwalimu NyerereUDSM yawaita wadau kutafakari fikra za Mwalimu Nyerere

Dar es Salaam. Wadau wa maendeleo ya siasa, uchumi na masuala ya kijamii wametakiwa kushiriki Kongamano la Kigoda cha Kiprofesa cha Mwalimu Julius Nyerere cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Kongamano hilo litakalofanyika kwa siku tatu mfulululizo kuanzia Mei 28-30, 2026, linatarajiwa kuwakutanisha wanazuoni na wadau kutoka sehemu mbalimbali kwa lengo la kuibua na kujadili mustakabali wa Tanzania na Afrika kwa kukumbuka na kuenzi fikra za Mwalimu Nyerere.

Akizungumza na waandishi wa habari chuoni hapo jana Jumatatu Mei 25, 2026, Mwenyekiti mpya wa Kigoda hicho, Profesa wa Sayansi ya Siasa, Alexander Makulilo amesema kongamano hilo lenye kauli mbiu ya “Siasa za Kikanda, Maendeleo na Mwelekeo wa Afrika” ni la 17 tangu kuanzishwa kwa Kigoda hicho mwaka 2008.

“Kongamano hilo litabeba mijadala kuhusu amani, maendeleo jumuishi, nafasi ya vijana, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na mchango wa mawazo ya Julius Nyerere katika siasa za kikanda na mshikamano wa Afrika,” amesema.

Kuhusu mada kuu za kongamano hilo, Profesa Makulilo amesema kutakuwa nha mada na watoa mada tofauti kila siku akifafanua Mei 28 kutakuwa na hafla ya kumsimika yeye rasmi kuwa mwenyekiti mpya wa Kigoda hicho kabla ya kutoa mhadhara wake wa kwanza utakaolenga kuchambua mawazo ya Mwalimu Nyerere katika siasa za kikanda barani Afrika.

Hafla hiyo itafuatiwa na warsha ya kuvalishwa vazi maalumu mzungumzaji mkuu wa kongamano hilo, Profesa Zachariah Mampilly kutoka Marekani na kutoa mhadhara wa kitaaluma kuhusu uzalishaji wa maarifa ya Kiafrika baada ya mfumo wa Kiliberali.

“Siku ya pili mjadala mkubwa utahusu mtazamo wa Tanzania na utekelezaji wa Dira 2050 ukiongozwa na Waziri wa Uwekezaji, Kitila Mkumbo. Atakayewasilisha mada ya Mwelekeo wa Afrika, Tafakuri kutoka Dira ya Taifa 2050.

Profesa Makulilo amesisitiza mada hiyo ni muhimu kwa Tanzania na Afrika kwa kuwa mwaka huu nchi inaanza rasmi utekelezaji wa Dira 2050, huku wasemaji watatu wakitarajiwa kuwasilisha mada kuhusu nafasi ya vijana katika kujenga mwafaka wa kitaifa na maendeleo ya Afrika kwa ujumla.

Aidha amesema siku ya tatu ya kongamano hilo itahusisha uzinduzi wa kitabu cha Joan Wicken na Ushirikiano wake wake wa maisha na Mwalimu Nyerere, kilichoandikwa na Profesa Aili Mari Tripp wa Chuo Kikuu cha Wisconcin Madson, Marekani, mtafiti na mwanaharakati wa mchango wa wanawake katika jamii.

Katika kongamano hilo, amesema zaidi ya wasemaji 40 kutoka Tanzania, Marekani, Ulaya na Asia wanatarajiwa kushiriki, huku mada ndogondogo zaidi ya 40 zikijadiliwa kuhusu changamoto zinazoikabili Afrika katika ulimwengu wa sasa unaotawaliwa na mataifa makubwa yenye nguvu za kisiasa na kiuchumi.

“Tunajadili namna gani Tanzania na Afrika zinaweza kwenda mbele katika kipindi hiki cha mitikisiko ya kidunia, kuanzia kupanda kwa bei za mafuta, vita vya Mashariki ya Kati, mabadiliko ya viwanda hadi masuala ya mazingira,” amesema Profesa Makulilo.

Umuhimu wa kongamano hilo

Profesa Makulilo amesema Kigoda hicho kilichoanzishwa mwaka 2008 kimekuwa jukwaa muhimu la mijadala kuhusu utaifa, maendeleo endelevu, umoja wa Afrika na nafasi ya nchi za Afrika katika mfumo wa dunia, kikiongozwa awali na kiongozi wake wa kwanza, Profesa Issa Shivji na baadaye Rwekaza Mukandala kabla ya yeye kukabidhiwa uongozi huo.

Amesema pamoja na kupita kwa miaka mingi tangu enzi za Mwalimu Nyerere, mawazo yake bado yana umuhimu mkubwa hasa katika masuala ya amani, mshikamano wa Afrika na ushirikiano wa kikanda, akiamini bara la Afrika likiungana litakuwa na sauti kubwa katika siasa za dunia zinazotawaliwa na mataifa yenye nguvu yaliyoitawala Afrika hapo awali.

Akizungumzia na Mwananchi kuhusu Kigoda hicho, Mwanahabari mkongwe na mchambuzi wa siasa, Absalom Kibanda amesema, kigoda hicho kimekuwa jukwaa muhim kwa wadau kutoa maoini na kuibua hoja za maendeleo.

“Tangu mwanzo wake, mjadala wa Kigoda cha Mwalimu umekuwa chachu ya fikra kwa watu kutambua wajibu waSerikali na haki zao. Limekuwa jukwaa ,uhimu la kuibua maoni na hoja za watu, uhuru huo wa maoni na hoja ni jambo muhimu kwa maendeleo ikiwa mamlaka zitayachukua na kuyafanyia kazi,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu hilo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie anaonesha mashaka juu ya uhuru wa maoni kwa wadau, akisema mijadala ya kitaifa kwa kipindi cha miaka ya hivi karibuni imekuwa na mwelekeo wa kusifu zaidi kuliko kuibua matatizo ya jamii na kushauri njia za utatuzi wa changamoto.

“Hapo awali mijadala ya wadau ilikuwa mikubwa sana ikiibua matatizo na suluhu, siku hizi mijadala ya namna hii haipewi nafasi kabisa.

“Hali hii imewanyamazisha wanazuoni wengi. Tunasubiri tuone kupitia kongamano hili, ikiwa litasimama na kuwaleta wadau watakaoibua hoja za msingi kuhusu maono ya Mwalimu Nyerere na njia za kukabiliana na matatizo halisi ya Tanzania na Afrika ya sasa, huenda ukawa mwanzo mpya wa kuchochea fikra za maendeleo,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *