Mambo ya Nje waanika vipaumbele wakiomba Sh359 bilioniMambo ya Nje waanika vipaumbele wakiomba Sh359 bilioni

Dodoma. Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imetaja vipaumbele vinne katika bajeti ya 2026/27, wakati ilipoomba bajeti ya Sh359.32 bilioni.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabiti Kombo ametaja mikakati hiyo leo Jumanne Mei 26, 2026 wakati akisoma hotuba yake.

Waziri amevitaja vipaumbele ni kuendelea kuimarisha uratibu na ushirikiano wa uwili, Kikanda na Kimataifa, kuratibu utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001, Toleo la Mwaka 2024 hususani utekelezaji wa diplomasia ya uchumi.

Vingine ni kulinda taswira, heshima na kutetea maslahi ya Tanzania katika nyanja ya kimataifa na kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi wa Wizara, kuimarisha utawala bora ikiwemo rasilimali watu pamoja na kutekeleza miradi ya maendeleo ya Wizara na taasisi zake.

Waziri amesema mbali na vipaumbele vya jumla, kila Taasisi imepewa mikakati katika kutekeleza vipaumbele vyake chini ya Wizara ambavyo kwa ujumla wake vipo katika vipengere 12.

Katika hotuba yake leo, Balozi Kombo amesema kati ya kiasi kilichoombwa, Sh46.36 bilioni zitatumika kwa ajili ya shughuli za maendeleo zitakazojumuisha ujenzi wa majengo na ukarabati wa ofisi.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo akizungumza wakati akiwasilisha Makadilio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika mashariki kwa mwaka wa fedha wa 2026/2027 Bungeni jijini Dodoma. Picha na Said Khamis

“Kwa mwaka 2026/27 tumetenga Sh200 milioni kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa jengo la Mahakama ya Haki za Binadamu na Watu Jijini Arusha wakati kiasi cha Sh5 bilioni zitafanya ukarabati wa jengo la Wizara jijini Dar es Salaam,” amesema Balozi Kombo.

Katika hatua nyingine, Waziri Kombo amesema licha ya kutetereka kwa mahusiano na migogoro ya vita vya moja kwa moja kwa baadhi ya Mataifa Duniani, hali ya amani kwa Bara la Afrika imeendelea kuimarika licha ya changamoto ndogondogo kwa baadhi ya Mataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *