Kesi ya mauaji ya Rhoda Mobe yaahirishwa hadi JuniKesi ya mauaji ya Rhoda Mobe yaahirishwa hadi Juni

Musoma. Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma imeiahirisha kwa mara nyingine kesi ya mauaji inayowakabili washtakiwa watatu wanaodaiwa kumuua kwa kumkakata mapanga mkazi wa Kijiji cha Burunga, wilayani Serengeti, Rhoda Mobe (42).

Kesi hiyo namba 23/12/2025 imeahirishwa hadi Juni 9, 2026, kutokana na upelelezi kutokukamilika.

Akiahirisha shauri hilo Jumanne, Mei 26, 2026, Hakimu Mkazi Mkuu, Eugenia Rujwahuka alisema kesi itatajwa tena tarehe hiyo kwa ajili ya hatua nyingine za kisheria.

Awali, Wakili wa Serikali, Joyce Matimbwi aliieleza mahakama kuwa upelelezi bado unaendelea na kuiomba ipange tarehe nyingine ya kutajwa kwa shauri hilo, akibainisha kuwa jalada la kesi limerudishwa kutoka kwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (RCO) kwenda kwa Mwendesha Mashtaka wa Taifa (NPS).

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Simon Ruhinda (55), mfanyakazi wa ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Marco Maginga (45), mwalimu wa shule ya msingi jijini Mbeya na Mwita Maginga (47), mkulima mkazi wa Tarime.

Inadaiwa kuwa Oktoba 23, 2025 usiku, washtakiwa hao walivamia nyumbani kwa Rhoda na kumshambulia kwa kumkata mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake, kinyume cha kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu.

Washtakiwa wote wanaendelea kushikiliwa rumande kutokana na kesi hiyo kutokuwa na dhamana, huku mahakama hiyo ya hakimu mkazi ikikosa mamlaka ya kusikiliza shauri hilo la mauaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *