Mbeya. Waislamu na wananchi kwa ujumla nchini wameshauriwa kutumia sikukuu ya Eid El Adh’haa kurejesha umoja, mshikamano, amani na maridhiano kama alivyoelekeza Mungu katika kitabu kitukufu cha Quran.
Leo Mei 27, Waislamu duniani kote wanaungana kusherehekea sikukuu hiyo ambayo ni maalumu kwa ajili ya kuchinja. Kwa Mkoa wa Mbeya, ibada hiyo imefanyika katika Uwanja wa Sokoine jijini humo.
Eid Al Adha ni sikukuu ya pili katika Uislamu inayosherehekewa kukumbuka utayari wa Nabii Ibrahim kumtoa mwanawe Ismail kama dhabihu kwa amri ya Mungu.
Lakini, msingi wake ni kuadhimisha kilele cha Ibada ya Hijja, ambapo waumini huchinja wanyama kama ng’ombe au mbuzi na kugawa kitoweo hicho kwa wasiojiweza na jamaa zao.
Baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu mkoani Mbeya wakiwa katika swala ya Eid Al Adha iliyofanyika leo Jumatano Mei 27, 2026 katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya. Picha na Sadam Sadick
Akizungumza baada ya swala hiyo, Kadhi wa Mkoa wa Mbeya, Sheikh Hassan Mbalazi, amesema wananchi na Watanzania wote wanapaswa kurejesha maridhiano, umoja na mshikamano.
Amesema wapo waliotofautiana kwa mali, maneno, siasa, vyeo na madaraka, akieleza kuwa kila mwenye nafasi anapaswa kumpatanisha anayemuweza ili kurejesha undugu wa dini, ubinadamu na utaifa.
“Lazima tuwe pamoja, sadaka iliyo bora ni kupatanisha ndugu waliogombana, leo ni siku ya mapatano, maridhiano, kuwa pamoja na kuishi kama atakavyo Mungu, kupitia siku kuu hii tunajifunza mengi,” amesema Dk Mbalazi.
Ameongeza kuwa kwa sasa Watanzania wanapaswa kuendelea kuliombea Taifa juu ya amani ili iweze kupatikana haki na maendeleo, akieleza kuwa wanapogombana wawili lazima watulizwe kwa kuuliza mkosaji.
“Kinachotangulia ni amani kisha haki kufuata, ndiyo maana hata Nabii Ibrahim alipouombea mji wa Makka alitanguliza amani kisha kuwaombea watu wa mji wake matunda, sisi tunaombea amani na maridhiano.
“Tunashukuru nchi yetu inaenda kwenye amani, tusipoteze jambo hili kwani itakuwa tatizo kwa vizazi vyetu. Mungu atusaidie katika hili ili tuweze kupata mafanikio na maendeleo,” amesema.
Kwa upande wake, Sheikh wa Mkoa wa Mbeya, Msafiri Njalambaha amesema sikukuu hiyo ni ukumbusho na funzo kwa vijana kuhusu maadili, akinukuu kisa cha mtoto wa Nabii Ibrahim kukubali kuchinjwa na baba yake.
“Haya ndiyo mafundisho katika siku kuu hii ya kuchinja, ambapo hata nchi inapaswa kwenda nayo ikiwa ni maadili kwa vijana na suluhu kwani Nabii Ibrahim alikuwa na matatizo na mke wake mkubwa ila kwa kujali ndoa na amani alimpeleka mke mdogo sehemu nyingine.
“Hivyo suluhu na maridhiano ni vitu muhimu sana na tunaomba Mungu atujaalie nchi yetu ambayo siku zote ni kisiwa cha amani ipite katika mambo hayo, Nabii Ibrahim ametufundisha mengi katika kisa hiki,” amesema.
Akitoa salamu za Mkoa, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbeya, Mohamed Aziz, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Beno Malisa, amewaomba wananchi kusherehekea kwa amani, upendo na mshikamano.
“Lakini tusaidiane kwa mwenye nacho na asiye nacho kwa lengo la kujiwekea amana huko mbinguni, tujitokeze pia kujenga umoja wetu na kuchangia shughuli za dini hasa Uislamu,” amesema Aziz.
