RC Tanga ahimiza ulinzi wa watoto swala ya EidRC Tanga ahimiza ulinzi wa watoto swala ya Eid

Tanga. Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Burian amewasihi wakazi wa mkoa huo, wanaposherehekea Sikukuu ya Eid Al Adha, wahakikishe wanalinda usalama wa watoto.

Amewataka pia, kulinda amani na kujenga mshikamano baina yao ili kuwe na umoja miongoni mwa wananchi wa mkoa huo na maeneo mengine.

Dk Batilda ametoa kauli hiyo leo, Jumatano Mei 27, 2026 baada ya swala ya Eid Al-Adhaa iliyofanyika katika Msikiti wa Ijumaa jijini Tanga.

Amesema ni muhimu kwa Waislamu na wananchi wote kuhakikisha watoto wanakuwa salama wanapokwenda kutembea, kucheza au kuogelea ndani ya siku hiyo.

“Ninawaomba wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanakuwa chini ya uangalizi wakati wote wa sikukuu ili kuepusha ajali zinazoweza kujitokeza, ikiwemo ajali za barabarani na maji,” amesema Dk Burian.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Burhan wakanza kushoto akiwa na waumimi wa dini ya kiislam wakati wa swala ya Eid Al Adha katika msikiti wa Ijumaa barabara ya kumi jijini Tanga.

Aidha, amewataka wananchi kuendelea kuonesha mshikamano kwa kuwasaidia watu wenye uhitaji, wakiwemo majirani, watoto wanaoishi katika vituo vya yatima pamoja na wajane ili kila mmoja aweze kusherehekea sikukuu hiyo kwa furaha na amani.

Amesema sikukuu hiyo inapaswa kuwa chachu ya kuimarisha upendo, mshikamano na kusaidiana katika jamii, huku wananchi wakihimizwa kuendelea kumuomba Mungu ailinde nchi na kuijalia amani.

“Ni muhimu kuhakikisha sikukuu yetu inaisha salama huku tukiendelea kumuomba Mwenyezi Mungu atujalie amani na kutuongoza katika mema,” ameongeza.

Sheikh wa Mkoa wa Tanga, Jumaa Luwuchu, amesema dini ya Kiislamu inasisitiza amani, upendo na kusaidiana, huku akibainisha kuwa hakuna sehemu yoyote inayoruhusu uvunjifu wa amani.

Amesema waumini wanapaswa kuendelea kufanya matendo mema, kushikamana na kuwasaidia wasiojiweza kwani hayo ni miongoni mwa mafundisho muhimu ya dini ya Kiislamu.

Kwa upande wake mkazi wa Tanga, Hamisi Mdoe, amesema Sikukuu ya Eid Al-Adha ni muda muhimu wa kuimarisha undugu na kusaidiana baina ya wananchi bila kujali tofauti zao.

“Sikukuu hii hutukumbusha umuhimu wa kushirikiana na kuwasaidia wenye uhitaji katika jamii yetu,” amesema Hamisi.

Naye Asha Ali, ambaye ni mmoja wa waumini wa Kiislamu jijini Tanga, amesema amani na utulivu uliopo nchini unapaswa kuendelea kulindwa na kila mwananchi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Amesema wazazi wanapaswa kuwa karibu zaidi na watoto wao katika kipindi cha sikukuu ili kuepuka matukio ya ajali yanayoweza kuzuilika.

“Watoto wengi hupenda kwenda baharini na sehemu za starehe wakati wa sikukuu, hivyo ni wajibu wa wazazi kuhakikisha wanakuwa salama muda wote,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *