Wanawake wakumbushwa kuepuka mashindano ya mavazi na mapamboWanawake wakumbushwa kuepuka mashindano ya mavazi na mapambo

Moshi. Wanawake wa Kiislamu nchini wametakiwa kuepuka kushindana kwa mavazi na mapambo yasiyo na tija, badala yake wazingatie maadili mema, hofu ya Mungu na malezi bora ya familia.

Eid Al Adha ni sikukuu ya pili katika Uislamu inayosherehekewa kwa kukumbuka utayari wa Nabii Ibrahim kumtoa mwanawe Isihaka kama dhabihu kwa amri ya Mungu.

Msingi wake ni kuadhimisha kilele cha Ibada ya Hijja, ambayo waumini huchinja wanyama kama ng’ombe au mbuzi na kugawa kitoweo hicho kwa wasiojiweza na jamaa zao.

Wito huo umetolewa leo Jumatano Mei 27, 2026 na Sheikh Thabit Tarimo wakati akitoa mawaidha katika swala ya Eid al-Adha iliyofanyika kimkoa katika Msikiti wa Riadha mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza mbele ya mamia ya waumini waliojitokeza kushiriki ibada hiyo, Sheikh Tarimo amesema wanawake wanapaswa kutambua kuwa uzuri wa kweli haupatikani katika mapambo ya nje pekee bali katika tabia njema na ucha Mungu.

Amesema katika kipindi hiki wanawake wengi wamekuwa wakishindana katika mavazi na mapambo huku wakisahau misingi ya dini na maadili inayopaswa kuwa kipaumbele katika maisha yao ya kila siku.

Baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu Mjini Moshi wakitoka katika ibada ya Eid al-Adha iliyofanyika kimkoa  Msikiti wa Riadha.

“Mnapenda sana kujipamba, lakini pambo lililo bora ni taqwa. Mnapenda kushindana kwenye mavazi, lakini nguo bora ni haya na maadili mema,” amesema Sheikh Tarimo.

Amesema mwanamke mwenye maadili mema na anayemcha Mungu ana mchango mkubwa katika kujenga familia imara na jamii yenye heshima.

Katika mawaidha hayo, Sheikh Tarimo pia amewataka wanaume kuhakikisha wanawahimiza wake zao pamoja na watoto kufanya  ibada ya swala na kuzingatia mafundisho ya dini.

“Baba anaweza kuwa kila adhana inamkuta msikitini lakini mke wake haswali na watoto hawaswali, huku akiwa hafanyi  juhudi yoyote ya kuwahimiza. Kila mmoja ataulizwa juu ya familia yake,” amesema.

Amesema si sahihi kwa mzazi kujisitiri katika ibada binafsi huku akiacha familia yake bila malezi ya dini na maelekezo ya kiroho.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa wazazi kuwafundisha watoto swala tangu wakiwa wadogo ili kuwajengea msingi mzuri wa dini na maadili.

“Tumeamrishwa kuwaelekeza watoto wetu swala tangu wakiwa wadogo ili wakue katika njia sahihi ya dini,” amesema.

Sheikh Tarimo amesema kusimamisha swala tano kwa wakati ni msingi muhimu katika maisha ya Muislamu na kwamba uzembe katika ibada hiyo unaweza kuathiri maisha ya kiroho ya mtu.

Pia, amewataka waumini kuitumia siku ya Eid al-Adha kujitathmini na kurekebisha mwenendo wao kwa kuzingatia mafundisho ya dini katika maisha yao ya kila siku.

Mmoja wa waumini waliohudhuria swala hilo, Khadija Lema amesema mawaidha hayo yamekuwa somo muhimu kwa wanawake kuhusu nafasi yao katika malezi na maadili ya familia.

“Tumekumbushwa kuwa heshima ya mwanamke haipo katika mavazi ya gharama bali katika tabia njema, malezi bora na kumcha Mungu,” amesema Khadija.

Naye Omar Mongi amesema siku ya Eid ni wakati wa kuimarisha mshikamano, kusaidiana na kuendeleza upendo miongoni mwa jamii.

“Siku hii si ya furaha pekee, bali pia ni nafasi ya kukumbushana mambo mema na kuimarisha undugu,” amesema Omar.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *