
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5
Nje ya lango la shule ya Utumishi Girls Academy mjini Gilgil, baadhi ya wazazi walikuwa wamepiga magoti wakisali. Wengine walikuwa wakilia kimya kimya huku wakishikilia simu zao mikononi, wakingoja tu simu moja, simu ambayo ingeweza kuwaambia mtoto wao bado yuko hai.
Wanafunzi 16 wamethibitika kufariki baada ya moto mkubwa kuzuka katika bweni la shule hiyo usiku wa kuamkia Alhamisi, Mei 28, 2026, huku wengine wakijeruhiwa walipokuwa wakijaribu kujiokoa kupitia madirishani au kukimbia gizani.
Kwa Fredrick Aloo, taarifa hizo zilianza kwa simu ya ghafla alfajiri.
“Nilipowasha TV na kuona habari zile, moyo wangu ulisimama,” alisema.
Binti yake alikuwa amelala katika bweni lililokuwa likiungua.
“Ni kwa rehema za Mungu tu amepona. Mungu mwenyewe alimwokoa. Amepoteza kila kitu lakini maisha ni muhimu zaidi kuliko vitu. Vitu vinaweza kununuliwa tena, lakini huwezi kununua maisha.”
Moto ulianza wanafunzi wakiwa wamelala
Chanzo cha picha, Reuters
Kwa mujibu wa polisi, moto huo ulianza majira ya saa saba usiku kwa saa za Afrika Mashariki na kuteketeza bweni lililokuwa na takribani wanafunzi 220.
Zaidi ya wanafunzi 800 walikuwa katika shule hiyo wakati wa tukio hilo.
Waziri wa Elimu Julius Ogamba alisema moto huo ulianzia katika ghorofa ya kwanza ya bweni hilo, ambalo liliharibiwa kabisa.
“Vikosi vya uokoaji vilifanikiwa kuuzima moto majira ya saa tisa usiku, lakini kufikia muda huo madhara makubwa yalikuwa tayari yametokea,” alisema alipofika eneo la tukio.
Alisema wanafunzi wataanza kukabidhiwa kwa wazazi na walezi wao huku uchunguzi ukiendelea kubaini chanzo cha moto huo.
Kamanda wa polisi Masoud Mwinyi alisema baadhi ya wanafunzi walikimbia kuelekea maeneo ya karibu kutokana na hofu na mshtuko.
“Maafisa wetu bado wanafuatilia maeneo ya karibu kwa sababu baadhi ya wanafunzi walikimbia usiku kutokana na hofu,” alisema.
Mwinyi alieleza tukio hilo kuwa “la kusikitisha na lenye kuumiza sana.”
“Hatukujua watoto wetu wako hai au wamekufa”
Nje ya shule, hali ilikuwa ya sintofahamu huku baadhi ya wazazi wakikimbia kutoka hospitali moja hadi nyingine kutafuta watoto wao.
Roselyn Rakamba alisema alipata taarifa hizo kupitia simu ya rafiki yake mapema asubuhi.
“Rafiki yangu alinipigia akaniuliza, ‘Mtoto yuko salama?’ Nikamuuliza mtoto gani? Ndipo akaniambia kuhusu moto wa shule ya Utumishi,” alisema.
Alisema alijaribu kuwasiliana na shule lakini hakukuwa na taarifa za kutosha.
“Niliambiwa kulikuwa na moto na baadhi ya watoto walikuwa wamejeruhiwa. Rafiki yangu aliyekuwa tayari shuleni alisema bado hawajawaona watoto.”
Dakika za kusubiri zilionekana kama saa nzima.
“Kabla sijafika shuleni, mwanangu alipata njia ya kunipigia simu. Nilikuwa nimechanganyikiwa sana lakini niliposikia sauti yake nilipata nafuu kidogo.”
Hata hivyo alisema furaha yake ilikuwa ya huzuni pia.
“Ninafuraha mwanangu yuko salama… lakini siwezi kusema nina furaha kabisa kwa sababu wazazi wengine wamewapoteza watoto wao. Katika shule hii tulikuwa kama familia moja. Tunaumia pamoja.”
Mama mwingine aliyekuwa akizungumza kwa machozi alisema familia yake ilikuwa imetafuta mtoto wao katika hospitali mbalimbali bila mafanikio.
“Tumekuwa hapa tangu saa kumi na mbili asubuhi. Hawatuambii mtoto wetu yuko wapi,” alisema.
“Tumetafuta hospitali zote za hapa karibu. Walimu hawatuambii chochote.”
Chanzo cha picha, Peter Njoroge / BBC
Wanafunzi waliruka kutoka dirishani kujiokoa
Wambui Nderitu, ambaye binamu yake ni mwanafunzi katika shule hiyo, alisema familia nyingi zilifika shuleni zikiwa katika hali ya hofu kubwa.
“Tulipoingia tuliambiwa tusimame kwenye foleni. Tulikuwa na wasiwasi mkubwa kwa sababu tulikuwa tumesikia baadhi ya wanafunzi wamefariki na wengine wako hospitalini.”
Alisema baadhi ya wanafunzi waliokuwa ghorofa ya juu walilazimika kuruka kutoka dirishani kujiokoa.
“Baadhi ya waliokuwa juu waliruka, ndiyo maana wameumia.”
Binamu yake alinusurika lakini alivunjika mguu.
“Nilimpata… yuko hai… lakini mguu wake umevunjika,” alisema.
Leah Serem, ambaye binti yake ni mwanafunzi wa mwaka wa mwisho katika shule hiyo, alisema alipata taarifa hizo akiwa nyumbani mjini Nakuru.
“Tulikuwa na hofu kwa sababu hatukujua watoto wetu walikuwa hai au wamefariki,” alisema.
Baadaye alimkuta binti yake akiwa salama.
“Nilifurahi sana na nikamshukuru Mungu.”
Binti yake alimweleza kuwa wanafunzi walikuwa wakigongana na kuamshana wakati moto ulipoanza.
“Tunawaombea wazazi ambao bado hawajawaona watoto wao. Tunawaomba Wakenya watuombeee huku chanzo cha moto kikichunguzwa,” alisema.

Historia ya moto mashuleni Kenya
Waziri wa Mambo ya Ndani Kipchumba Murkomen, ambaye pia alifika shuleni humo, alituma salamu za pole kwa familia zilizopoteza watoto wao.
“Ni wakati wa hofu kubwa. Tunapothibitisha vifo vya wanafunzi 16 hadi sasa, naomba Wakenya wote tusimame pamoja na familia hizi kwa maombi na msaada,” alisema.
Aliwataka wananchi kuwa watulivu huku uchunguzi ukiendelea.
“Naomba watu wawe wavumilivu na waepuke kutoa taarifa za kubahatisha.”
Moto katika shule za bweni si jambo geni nchini Kenya.
Mwaka 2001, wanafunzi 67 walifariki katika shule moja eneo la Machakos baada ya bweni kuteketekea kwa moto, tukio ambalo bado linatajwa kuwa baya zaidi katika historia ya shule nchini humo.
Mwaka 2024, watu wasiopungua 21 walifariki katika moto mwingine ulioteketeza bweni katikati mwa Kenya.
Baada ya tukio hilo, tathmini ya Wizara ya Elimu ilibaini kuwa shule nyingi zilikuwa na mabweni yenye madirisha yenye nondo, milango michache ya kutokea na milango iliyokuwa ikifunguka kuelekea ndani, hali iliyokuwa ikihatarisha usalama wa wanafunzi wakati wa dharura.
Msongamano mkubwa wa wanafunzi mabwenini pia ulitajwa kuwa moja ya sababu zinazochangia idadi kubwa ya vifo wakati wa majanga ya moto.
Mwaka 2021, Wizara ya Elimu nchini Kenya ilisema kulikuwa na matukio 126 ya uchomaji moto mashuleni kati ya Januari na Novemba 2020 pekee.
Lakini nje ya lango la Utumishi Girls Academy mjini Gilgil, wazazi wengi hawakuwa wakifikiria kuhusu takwimu wala historia ya majanga ya moto mashuleni.
Walikuwa wakingoja tu kuona watoto wao wakitokea wakiwa hai.
Taarifa hii imechangiwa na waandishi mbalimbali wa BBC akiwemo Akisa Wandera, Basillioh Rukanga na Nairobi Thomas Mukwana
