Dodoma. Wakati Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ikisema imeanza utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa kudhibiti migogoro ya ardhi, Kamati ya Bunge ya wizara hiyo, imeitaka Serikali kuongeza kasi ya upangaji, upimaji na kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro.
Mbali na hayo, wabunge wamesema ukosefu wa mwongozo bora wa matumizi ya ardhi pamoja na maofisa ardhi kuwa chini ya halmashauri kunachangia kuongezeka kwa migogoro ya ardhi nchini.
Hayo yameelezwa leo Ijumaa Mei 28, 2026 wakati Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Leonard Akwilapo alipowasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara kwa mwaka 2026/27.
Wizara hiyo imeliomba Bunge kuidhinisha bajeti ya Sh210.3 bilioni kwa mwaka wa fedha 2026/27, huku ikiainisha vipaumbele vinane vya utekelezaji ndani ya wizara hiyo.
Mbunge wa Rorya, Jafari Wambura akizungumza wakati akichangia Makadilio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya makazi kwa mwaka wa fedha wa 2026/2027 Bungeni jijini Dodoma. Picha na Said Khamis
Kuhusu utatuzi wa migogoro ya ardhi kiutawala, Dk Akwilapo ameliambia Bunge kuwa wizara imeendelea kutatua migogoro hiyo kupitia njia mbalimbali, ikiwamo kliniki za ardhi katika mikoa na mamlaka za Serikali za mitaa, madawati ya kushughulikia kero na malalamiko, pamoja na timu maalumu za wataalamu wa Serikali.
Amesema, viongozi wa wizara wamekuwa wakifanya ziara katika maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi zinazohusiana na ardhi.
Dk Akwilapo amesema migogoro inayoshughulikiwa inahusisha masuala ya fidia, milki pandikizi, migogoro ya mipaka ya vijiji, viwanja na mashamba, uvamizi wa maeneo ya umma na binafsi, pamoja na udanganyifu unaotumia nyaraka za kughushi.
Amesema changamoto nyingine zinazopatiwa ufumbuzi ni madai ya mali za urithi au wanandoa, pamoja na migogoro inayotokana na urasimishaji wa makazi na upimaji shirikishi wa ardhi.
Pia, amesema yapo malalamiko yanayotokana na wananchi kutoridhika na uamuzi unaotolewa na vyombo vya utoaji haki kisheria.
Mbunge wa Bunda mjini Ester Bulaya akizungumza wakati wa kipindi cha maswali na majibu Bungeni jijini Dodoma.
“Kutokana na kuwepo kwa migogoro ya ardhi inayoendelea kujitokeza katika maeneo mbalimbali nchini, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba alielekeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuandaa mkakati wa kupata ufumbuzi wa kudumu wa migogoro hiyo.
“Kufuatia maelekezo hayo, Serikali imeandaa na kuanza utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa kudhibiti migogoro ya ardhi nchini.
“Mkakati huo unahusisha wadau na makundi yote muhimu hususan wakulima, wafugaji, wawekezaji na mamlaka za hifadhi ili kuhakikisha changamoto ya migogoro ya ardhi inapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
“Napenda kutumia fursa hii kumshukuru tena mheshimiwa Waziri Mkuu kwa dhamira yake ya dhati ya kuhakikisha migogoro ya ardhi inadhibitiwa hivyo kuwawezesha watumiaji wa ardhi kufanya kazi zao kwa amani na utu,” amesema Dk Akwilapo kwenye hotuba yake.
Katika kushughulikia agizo hilo, amesema katika mwaka 2025/26, wizara ilipanga kushughulikia migogoro ya ardhi 3,000 lakini hadi Mei 15, 2026, jumla ya migogoro ya ardhi 5,573 ilitatuliwa ambapo kati ya hiyo, migogoro 3,183 imetatuliwa kupitia Kliniki za Ardhi na 2,390 kupitia utaratibu wa kawaida wa kiutawala.
Mbunge wa Bunda mjini Ester Bulaya akizungumza wakati wa kipindi cha maswali na majibu Bungeni jijini Dodoma
Kwa bajeti ya mwaka 2026/27 amesema, wizara imepanga kushughulikia migogoro 4,000 kiutawala huku akiwataka watumishi na wananchi kwa jumla kuzingatia sheria na taratibu ili wasizalishe migogoro mipya.
Amesema katika mwaka wa fedha unaoishia 2025/26 wizara ilipanga kuendelea na ukamilishaji wa kazi zilizobaki za utekelezaji wa uamuzi wa Baraza la Mawaziri kuhusu utatuzi wa migogoro ya ardhi katika vijiji 975.
Dk Akwilapo amesema uamuzi umeendelea kutekelezwa ikiwamo kurejesha ardhi kwa wananchi na ekari milioni 3.13 zimerejeshwa na Sh95.27 bilioni zimelipwa kwa wananchi waliostahili kulipwa fidia katika maeneo hayo.
Amesema kazi hiyo imefanywa na timu ya wataalamu kutoka taasisi na wizara za kisekta huku akisisitiza kuwa, kufuatia tathmini iliyofanyika, mpango kazi kwa ajili ya kukamilisha kazi zilizobaki umeandaliwa, hivyo wizara kwa kushirikiana na taasisi na wizara za kisekta, itaendelea kuratibu ukamilishaji wa kazi hizo.
Dk Akwilapo amesema utekelezaji husika utahusisha vijiji 349 na mitaa 11 ambayo sehemu ya utekelezaji wa uamuzi imeanza kufanyiwa kazi, pamoja na vijiji 166 ambavyo utekelezaji wake utafanyika katika mwaka 2026/27.
Vipaumbele vya Wizara
Dk Akwilapo pia amevitaja vipaumbele hivyo kuwa ni kuongeza kasi ya upangaji, upimaji, umilikishaji na usajili wa ardhi mijini, vijijini na maeneo ya kimkakati, kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji, kuimarisha mifumo ya Tehama (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano) katika utunzaji wa kumbukumbu, utoaji wa huduma, ukusanyaji wa maduhuli na upatikanaji wa taarifa za ardhi na uthamini.
Vipaumbele vingine ni kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro ya ardhi kwenye mabaraza ya ardhi na nyumba ya wilaya, kuhakikisha uwepo wa nyumba bora, ukuaji wa sekta ya milki na maendeleo ya makazi kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kuimarisha mipaka ya kimataifa na kuendeleza miji ya mipakani.
Hata hivyo, Dk Akwilapo amesema wataimarisha upatikanaji wa ramani ili kuwezesha uandaaji wa mipango ya kitaifa na matumizi mengine na kuimarisha mifumo ya usimamizi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa vipaumbele.
Maoni ya Kamati
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeitaka Serikali kuongeza kasi ya upangaji, upimaji, umilikishaji na usajili wa ardhi mijini, vijijini na maeneo ya kimkakati na utunzaji wa kumbukumbu, utoaji wa huduma, ukusanyaji wa maduhuli na upatikanaji wa taarifa za ardhi na uthamini.
Makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, Mary Masanja amesisitiza kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro ya ardhi kwenye mabaraza ya ardhi pamoja na nyumba ya wilaya.
Pia, amesema kuwepo nyumba bora na maendeleo ya makazi kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
“Serikali iongeze kasi katika kuandaa na kuweka mipango ya matumizi bora ya ardhi ili vijiji vyote vifikiwe na mipango, iongeze kasi ya kupima, kupanga, kumilikisha na kusajili haki miliki za ardhi kwa kila kipande cha ardhi ili kuondoa migogoro lakini pia kuongeza pato la Taifa litokanalo na rasilimali ardhi,” amesema Masanja.
Maoni ya wabunge
Mbunge wa Bariadi Vijijini (CCM), Masanja Kadogosa akichangia mjadala wa bajeti ya wizara hiyo amesema chanzo cha migogoro ya ardhi ni wizara kukosa mwongozo wa matumizi bora ya ardhi.
Mbunge wa Bagamoyo Subira Mgalu akizungumza wakati wa kipindi cha maswali Bungeni jijini Dodoma.
Amesema hali hiyo inachangia kuwepo wa ugumu kwenye biashara akitolea mfano wa ujenzi wa viwanda mbali na vyombo vya usafirishaji ikiwamo treni ya mwendokasi (SGR).
Mbunge wa Dodoma Mjini (CCM), Paschal Chinyele akichangia mjadala wa bajeti hiyo ametaja kiini cha migogoro ambacho ni kitendo cha maofisa ardhi kuwa chini ya halmashauri wakati inawajibika moja kwa moja Wizara ya Ardhi kitendo kinachoonesha wanashindwa kuwajibika.
Chinyele amesema watumishi hao wanazalisha migogoro mingi akitolewa mfano wa Jiji la Dodoma ambako kuna migogoro mingi inayosababishwa na watumishi hao.
Amesema wananchi wengi wamezaliwa na kuzeekea katika maeneo hayo lakini ghafla wanakuja watu wenye hati miliki jambo alilosema ni la aibu.
