
Udongo wenye afya ni msingi wa uzalishaji bora wa chakula na ustawi wa wakulima. Hata hivyo, katika kijiji cha Mbangamao, wilayani Mbinga mkoani Ruvuma, simulizi ya mkulima mmoja inaakisi hali halisi inayowakabili mamilioni ya wakulima barani Afrika.
Miaka kumi iliyopita, alivuna kwa wingi na kuhudumia familia pamoja na kuuza ziada. Leo, licha ya kutumia mbinu zilezile, mavuno yamepungua, hali inayodhihirisha kupungua kwa rutuba ya ardhi.
Hali hii si ya mkulima huyo pekee, bali ni changamoto pana inayolikumba bara la Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara, ambako kilimo bado ni uti wa mgongo wa uchumi na ajira. Takribani asilimia 65 ya watu wanaojihusisha na kazi barani humo wanategemea kilimo, wakati idadi ya watu ikiendelea kuongezeka na kufikia zaidi ya bilioni 1.5. Hii inaweka shinikizo kubwa zaidi kwenye ardhi inayozidi kuchoka.
Kwa miaka mingi, wakulima wengi wameendelea kutumia mashamba yaleyale bila kuyapa nafasi ya kurejesha rutuba yake ya asili. Matokeo yake ni udongo kupoteza virutubisho muhimu kama naitrojeni, fosforasi na potasiamu vinavyohitajika kwa ukuaji wa mazao.
Kila msimu wa mavuno unapoisha na mazao kuondolewa shambani, virutubisho hupungua bila kurudishwa ipasavyo, na hivyo kupunguza uwezo wa ardhi kuzalisha kwa kiwango kilekile cha awali.
Hali hii imewafanya wakulima wengi kulalamika kupungua kwa mavuno, huku wengine wakishindwa kupata faida bila kutumia mbolea. Hata hivyo, kiwango cha matumizi ya mbolea bado ni kidogo na hakikidhi mahitaji ya mazao, jambo linalochangiwa pia na gharama kubwa za pembejeo.
Gharama hizo zinatokana na utegemezi mkubwa wa Afrika kwa malighafi na virutubisho vya mbolea kutoka nje ya bara, pamoja na gharama za usafirishaji, kodi, na mabadiliko ya bei ya mafuta. Mnyororo mrefu wa usambazaji nao huongeza bei, na hivyo kuwafanya wakulima wengi kushindwa kumudu gharama hizo.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo, serikali mbalimbali barani Afrika zimekuwa zikitoa ruzuku za mbolea na pembejeo za kilimo. Kwa Tanzania, kwa mfano, zaidi ya shilingi 300 bilioni zilitengwa kwa msimu wa 2024/2025 kwa ajili ya ruzuku ya mbolea. Katika kipindi hicho, zaidi ya wakulima 4.5 milioni walisajiliwa kunufaika na mpango huo kati ya zaidi ya milioni 12 wanaojihusisha na kilimo nchini.
Hata hivyo, mjadala mpana unaendelea kuhusu suluhisho la muda mrefu. Je, Afrika inapaswa kuiga mifumo ya kilimo ya maeneo mengine, au inahitaji njia yake ya kipekee inayozingatia mazingira yake? Marehemu Kofi Annan aliwahi kutoa wito wa “Mapinduzi ya Kijani ya Afrika” yanayozingatia utofauti wa udongo, hali ya hewa na mifumo ya maisha ya wakulima wa bara hili.
Wataalamu wa kilimo wanaeleza kuwa rutuba ya udongo huathiriwa na mambo mawili makuu: asili ya udongo wenyewe na namna unavyosimamiwa. Katika baadhi ya maeneo, matumizi ya kilimo cha kuhamahama na kupumzisha mashamba kwa muda mfupi hayatoshi tena kurejesha rutuba iliyopotea. Aidha, matumizi yasiyo sahihi ya samadi na mbolea huongeza tofauti ya uzalishaji kati ya mashamba yaliyo karibu na makazi na yale ya mbali.
Suluhisho la msingi linaanza na maarifa. Upimaji wa afya ya udongo unawawezesha wakulima kujua hali halisi ya virutubisho vilivyopo na vinavyohitajika. Kupitia taarifa hizo, mkulima anaweza kufanya maamuzi sahihi kuhusu aina ya mazao na mbolea inayofaa, hivyo kuongeza tija na kupunguza gharama zisizo za lazima.
Upimaji wa udongo hubaini viwango vya virutubisho muhimu kama Naitrojeni (N), Fosforasi (P) na Potasiamu (K). Maarifa haya husaidia kuzuia matumizi ya kupita kiasi ya mbolea, ambayo si tu hupoteza fedha bali pia huharibu mazingira na kuathiri viumbe hai wanaosaidia kuboresha afya ya udongo.
Katika kuhakikisha mbolea inachangia uboreshaji endelevu wa udongo, baadhi ya bidhaa kama mbolea za Minjingu hutengenezwa kwa mfumo wa chembechembe ndogo zinazoyeyuka taratibu ardhini, hivyo kuongeza rutuba kwa muda mrefu zaidi ikilinganishwa na mbolea zinazoyeyuka haraka na kutoa virutubisho kwa muda mfupi.
Mustakabali wa kilimo Afrika unategemea uwekezaji katika afya ya udongo, elimu kwa wakulima na matumizi sahihi ya pembejeo. Bila kufanya hivyo, ongezeko la watu na mahitaji ya chakula yataendelea kushinda uwezo wa uzalishaji. Udongo wenye afya si chaguo, bali ni msingi wa usalama wa chakula na maendeleo ya kiuchumi barani Afrika.
