Miamala ya simu yageuka dhahabu mpya kampuni za mawasilianoMiamala ya simu yageuka dhahabu mpya kampuni za mawasiliano

Kwa miaka mingi, kampuni za mawasiliano nchini zilijenga biashara zao kwa kutegemea zaidi huduma za kupiga simu na ujumbe mfupi wa maandishi (SMS). Hizo ndizo zilikuwa injini kuu ya mapato na ushindani katika sekta hiyo.

Hivyo, mabadiliko ya teknolojia na tabia za watumiaji sasa yamegeuza mwelekeo huo, huku huduma za miamala ya fedha kupitia simu zikijitokeza kama “dhahabu mpya” ya sekta ya mawasiliano.

Hadi Machi 31, 2026 nchini Tanzania kulikuwa na akaunti za miamala ya simu zipatazo 80,977,268 ambazo zinafanya miamala 742,751,361 kwa mwezi. M-pesa inatawala soko kwa asilimia 41, ikifuatiwa na Mixx by Yas asilimia 31 huku watoa huduma wengine wakigawana kiwango kinachobakia.

Huduma za miamala ya simu sasa si nyongeza tena kwenye huduma za simu, bali zimekuwa msingi mpya wa mapato na ukuaji wa kampuni za simu, zikibadili kabisa namna biashara ya mawasiliano inavyoeleweka nchini.

Mfano wa wazi ni kampuni ya Vodacom Tanzania kupitia huduma yake ya M-Pesa, ambayo imepanuka kutoka huduma ya kutuma na kupokea fedha hadi mfumo mpana wa kifedha unaojumuisha mikopo, uwekezaji, akiba za vikundi na malipo ya kidijitali.

Akizungumza katika ripoti ya fedha ya mwaka ulioishia Machi 31, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Philip Besiimire alisema kampuni hiyo imeendelea kuwawezesha mamilioni ya Watanzania kupitia M-Pesa, huduma inayotekelezwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, M-Pesa sasa imekuwa zaidi ya huduma ya fedha za haraka, bali ni jukwaa la ujumuishwaji wa kifedha kupitia suluhisho mbalimbali za kidijitali.

Takwimu zinaonyesha ukubwa wa mabadiliko hayo. Katika mwaka wa fedha ulioishia Machi 31, 2026, mapato ya Vodacom Tanzania yalifikia Sh1.84 trilioni, ambapo huduma za M-Pesa zilichangia Sh734.79 bilioni, sawa na ongezeko la asilimia 24.5 kutoka Sh590 bilioni mwaka uliotangulia.

Ongezeko hilo linaashiria wazi kwamba karibu nusu ya mapato ya kampuni hiyo sasa yanatoka kwenye huduma za kifedha kidijitali, badala ya huduma za mawasiliano za jadi.

Hali hiyo inaakisi mabadiliko makubwa ya soko la mawasiliano, ambapo ushindani sasa haupo tena kwenye bei ya dakika za maongezi pekee, bali kwenye ubunifu wa huduma za kifedha na kidijitali.

Kupungua kwa matumizi ya SMS na simu za kawaida kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya intaneti na mitandao ya kijamii kumelazimisha kampuni za simu kubuni vyanzo vipya vya mapato, huku huduma za fedha zikiwa jibu kuu.

Kupitia M-Pesa, Vodacom Tanzania imejenga mfumo mpana unaogusa maisha ya kila siku ya Watanzania, hususan kupitia mikopo midogo na huduma za ‘overdraft’ kama Songesha.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya kifedha, zaidi ya wateja milioni tano walitumia huduma za mikopo na Songesha kwa mwaka uliopita, huku Sh3.4 trilioni zikitolewa kupitia huduma hizo. Hii ni ongezeko la asilimia 17.8, na Songesha pekee ikikua kwa asilimia 33.8 kwa mikopo ya muda mfupi kwa wateja binafsi.

Hali hii inaonyesha namna kampuni za simu zilivyoingia moja kwa moja kwenye sekta ya huduma za kifedha, eneo ambalo hapo awali lilihusishwa zaidi na benki.

Huduma nyingine inayoonyesha mageuzi hayo ni M-Wekeza, inayotolewa kwa ushirikiano na Sanlam Investments East Africa, ambayo imefungua milango ya uwekezaji kwa wananchi wa kipato cha kawaida.

Tangu kuanzishwa kwake Novemba 2024, huduma hiyo imewezesha maelfu ya Watanzania kuwekeza zaidi ya Sh370 bilioni, ikionyesha wazi kuwepo kwa mahitaji makubwa ya bidhaa rahisi za uwekezaji.

Katika upande wa akiba, huduma ya M-Koba inayotolewa kwa kushirikiana na Tanzania Commercial Bank pia imeonyesha ukuaji mkubwa, ambapo amana ziliongezeka kwa zaidi ya asilimia 80 na kuvuka Sh1 trilioni. Zaidi ya asilimia 60 ya fedha hizo zilihusisha wanawake, ishara ya kuimarika kwa ushiriki wa wanawake katika shughuli za kifedha kupitia majukwaa ya kidijitali.

Huduma za malipo pia zimeendelea kuwa chanzo muhimu cha mapato. Idadi ya wafanyabiashara wanaotumia huduma ya “Lipa kwa simu” iliongezeka kwa asilimia 29, hatua inayochochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.

Serikali nayo imenufaika na mabadiliko hayo, ambapo miamala ya malipo ya kidijitali iliongezeka kwa asilimia 17.8, huku thamani ya fedha zilizopitia mfumo huo ikikua kwa asilimia 24.6.

Hata hivyo mbali na ukuaji wa mapato ya miamala, upande mwingine, huduma za intaneti zimeendelea kuwa mhimili mwingine wa mapato kwa kampuni za mawasiliano. Kwa Vodacom Tanzania, mapato ya intaneti yaliongezeka kwa asilimia 29.5 hadi Sh546.7 bilioni, wakati huduma za kupiga simu zikichangia Sh334.8 bilioni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *