Dili iliyokufa – 4Dili iliyokufa – 4

““LINALETA ubishi. Tutakunyoosha, ondoa mikono yako”

Nikaondoa mikono kwenye uso.

“Naomba msinipige, Mimi ni mgeni” Nikawambia kwa sauti ya kusihi.

“Tena linanuka pombe, linajifanya ni mgeni”

“Ni mgeni kweli, nilikuja juzi hapa Dar”

“Unatoka wapi!”

“Ninatoka Muheza”

“Wewe si unakula unga?”

“Hapana”

“Hii si kete yako?” Polisi aliyeniuliza alichukuwa ile kete akanionyesha kisha akanitandika kibao.

“Hapana si yangu” Nikamjibu kwa kelele.

“Ni yanani?”

“Ngoja niwaeleze”

“Lifungulie jalada tulipeleke mahakamani leo leo” Polisi mwingine akamwambia mwezake.

“Ngoja tulisikilize, Tunaweza kupata watuhumiwa wengine, Unataka kutueleza nini?” Polisi huo akaniuliza.

Nikakieleza kisa chote kilicho nitokea tangu nilivyo wasili Daresalaam mpaka nilivyo kutwa nimelala kwenye mfereji.

“Una uhakika kwamba ulilipwa milioni kumi na pesa hizo zimeibiwa?” Polisi mmoja akaniuliza baada ya kunisikiliza.

“Nina ahakika” Nikamjibu kwa kusisitiza.

“Unataka twende kwenye Ofisi za shirika la bahati na nasibu na kwenye hoteli unayodai umefikia, tukaulize?”

“Twendeni sasa hivi”

“Wakisema wewe ni muongo tukufanye nini?”

“Mtanifanya mnavyotaka nyinyi”

“Sawa”

Polisi huyo akanishika mkono na kunikokota kuelekea kwenye mlango wa chumba kimoja kati ya vyumba kadhaa vilivyo kuwa ndani ya kituo hicho, aliniingiza ndani ya chumba kile ambako tulikutana na Polisi mwengine mwenye nyota tatu,

“Afande huyu mtuhumiwa ameletwa hii asubuhi……..” Polisi huyo akaendelea kumueleza afande huyo kuhusu tuhuma zilizokuwa zinanikabili na yale madai niliyo yatowa.

“Sasa tunataka tuende naye katika shiriki la bahati nasibu pamoja na hoteli anayodai amefikia ili tupate ukweli”

“Sawa, tunaweza kwendanaye lakini kwanza mfungulieni jalada”

“Sawa afande”

Tukatoka na yule polisi. Alinifungulia jalada kisha nika pakiwa kwenye gari pamoja na polisi watatu, tukaenda kwenye ofisi za shirika la bahati na sibu.

Muda huo ulikuwa  ukikaribia saa mbili na nusu asubuhi, tulikuta ofisi hizo zilikuwa zishafunguliwa.

Wafanyakazi wa shirika hilo walishangaa waliponiona kwenye ofisi zao nikiwa nimefatana na polisi. Niliwalekeza polisi hao kwenye ofisi ya yule afisa alienipa hundi, tulipoingia kwenye ofisi hiyo tulimkuta ofisa huyo akisoma gazeti, akashituka

Polisi hao walimsalimia kisha wakamuuliza kama alikuwa ananifahamu.

“Nina mfahamu “ afisa huo akajibu na kuuliza. “Kuna tatizo gani?”

“Amedai kwamba alishinda milioni kumi na jana mlimlipa hundi ya pesa hizo. Je ni kweli?”

“Ni kweli.”

Polisi hao wakaniangalia kwa mshangao.

“Kwani nini kimetokea?” Afisa wa shirika hilo la bahati nasibu akawauliza.

Poilisi hao wakamueleza mkasa ulionitokea.

Ofisa huyo wa shirika la bahati nasibu akatikisa kichwa kusikitika.

“Nilimwambia jana kuwa kutembea na milioni kumi katika Jiji hili ni hatari”

“Alikuambia anatoka wapi?” polisi mmoja akamuuliza.

 “Alinivyonieleza ni kwamba yeye ni mwenyeji wa kijiji cha Kibanda kilichopo Wilayani Muheza na huko ndiko alikopata tiketi iliyompa ushindi.Hapa Dar alikuja tu kuchukua zawadi yake na aliniambia angerudi jana ileile”

“Matatizo aliyataka mwenyewe.Wewe badala ya kurudi kwenu unataka kufanya starehe!”

“Lakini atakuwa ni yule msichana niliyekwenda kulala naye kwa sababu ndiye aliyeng’ang’ania tuhame katikas ile hoteli,” nikasema bila kuona aibu kama vile nilikuwa nasema kitu cha maana.

“Sasa unajua ulikwenda kulala naye katika hoteli gani?” polisi mmoja akaniuliza kwa ukali

 “Kwa kweli sikumbuki”

 “Ni nani alikununulia ile kete ya unga?”

 “Nafikiri yule msichana alinitilia mfukoni mwangu wakati nikiwa sijifahamu”

 “Na ni kwanini upotewe na fahamu kiasi hicho kama hukula unga?”

 “Inawezekana walimtilia kwenye bia.Huo mtindo upo hapa Dar. Walimtilia ili apotewe na fahamu wapate kumwibia.” Afisa wa shirika la bahati nasibu akaingilia kati.Na mimi nikakubaliana hapohapo.

 “Inawezekana yule msichana alinitilia kwenye bia bila mimi kujua”

 Ninaamini polisi hao waliniona nilikuwa bwege kupita kiasi.

 Hata hivyo polisi mmoja aliendelea kusisitiza kuwa nilikula unga kwa ridhaa yangu mwenyewe.Kwa hiyo mbali ya kuwatafuta hao walioniibia lakini ni lazima wanifungulie kesi.

 Tulipotoka katika ofisi za shirika hilo nilikwenda na polisi hao katika ile hoteli niliyokuwa nimekodi chumba.

 Karani wa vyumba aliponiona nimekwenda na polisi akaniuliza.  “Imekuwaje?”

 “Kuna matatizo yametokea” nikamjibu

 “Ni lini alikuja kuchukua chumba kwako?” Polisi mmoja akamuuliza yule karani.

 “Alichukua chumba juzi.Kusema kweli chumba hicho alipangiwa na shirika la bahati nasibu.Hao ndiyo waliyonilipa.Jana asubuhi alitakiwa aondoke lakini mchana alirudi tena akajipangishia mwenyewe.” Karani huyu akawaeleza polisi

 “Kuna vitu vyovyote ambavyo alifika navyo hapa hoteli?”

 “Ndiyo.Tulipompa chumba alitoka,baadaye alirudi na taksi akiwa na vitu vingi.Tuliona redio,nguo na mifuko yenye vitu”

 “Na aliporudi usiku nini kilitokea?”

 “Ilikuwa ni kasheshe.Huyu bwana alirudi karibu saa tisa usiku na taksi.Kwa jumla walikuwa watu wanne,wanaume wawili na wanawake wawili.Lakini yeye alishuka na mwanamke mmoja.Alikuwa amelewa sana.Akaniambia anataka kuhama chumba usiku huo”

Karani huyo akaendelea kuwaeleza polisi. “Nilimsihi sana asiondoke usiku lakini hakunisikia akachukua mizogo yake na kuondoka pamoja na yule mwanamke.”

 Polisi wakaniuliza nilipoondoka hapo nilikwenda hoteli gani lakini sikuwa na jibu.

“Na zile pesa ziko wapi”

“Bila shaka pesa nimeibiwa.”

“Hebu ngoja tupekue humu ndani.”

Polisi wakaanza kupekua humo chumbani. Nilikuwa nimesimama karibu na mlango.

Nilirudi kinyumenyume hadi nikaufikia mlango.Wakati polisi hao wakishughulika kupekua wakidhani wangeweza kuziona pesa hizo nilitoka kwenye mlango,nikatembea harakaharaka hadi mlango wa nje.Nilipotoka nje nikatimua mbio.Nilikata kona kwenye mtaa uliokuwa karibu na hoteli hiyo kisha nikakata kona nyingine na kutokea mtaa wa tatu. Nilijichanganya katika makundi ya watu nikaacha kukimbia lakini nikawa natembea haraka haraka huku nikiangalia nyuma.

Mara nikaliona lile gari la polisi likikata kona na kuingia katika ule mtaa huku likienda kwa kasi.Nilijua kuwa polisi hao walikuwa wananitafuta.Nikaingia kwenye duka moja.

Gari hilo likapita kwa kasi.Nikatoka kwenye lile duka bila kuuliza kitu chochote.Niliona lile gari likiendelea kwenda na mimi nikaanza tena kutembea kwa mwendo wa haraka haraka.

Kwa akili yangu niliona nimefanya jambo la maana kuwakimbia polisi hao ambao walikuwa wamekusudia kunifungulia mashitaka ya kukutwa na kete ya madawa ya kulevya.Mbali ya kupata hasara ya kuibia shilingi milioni kumi,bado nipate kesi ambayo itanifunga jela!

Haiwezekani, nilijiambia huku nikitembea.Ni bora nipate hasara ya pesa lakini mwenyewe nisalimike. Mawazo yangu sasa yalikuwa kwenda  kupanda basi  nirudi Muheza lakini sikuwa na hata senti tano mfukoni.Nitalipa nauli kwa pesa gani.

Nikaona nimtafute Dastan Lazaro ili nimueleza matatizo yaliyonitokea ili aweze kunipa msaada wake.Nilitegemea nikimpata Dastan anaweza kujua yule msichana aliyeniibia anapatikana wapi.Na Dastan pia anaweza kunisaidia kuzipata pesa zangu hata kama si zote.

Sasa kulikuwa na tatizo la kumpata Dastan kwa sababu nilikuwa sijui anakoishi.Hapo hapo nikakumbuka kwamba aliniambia yeye ni meneja masoko katika kiwanda cha bia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *