BAADA ya KVZ kushinda bao 1-0 dhidi ya Uhamiaji, kocha mkuu wa timu hiyo, Hababuu Ali, amesema watahakikisha hawashuki kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) hadi kumalizika msimu huu wa 2025-2026.
Amesema hilo linawezekana kwani hivi sasa wanaongoza kwa tofauti ya pointi sita dhidi ya timu ya pili, huku wakiwa wametoka kucheza mechi ngumu lakini wakashinda. KVZ ina poiti 58, JKU (pointi 52) na Fufuni (pointi 48).
Kocha huyo ameeleza kwamba, mechi dhidi ya Uhamiaji haikuwa nyepesi lakini mbinu zake sambamba na wachezaji kufuata kile walichoelezwa, kimesaidia kuondoka na ushindi.
“Tunapambana ili timu isishuke kileleni hadi mwisho wa msimu ambapo malengo ni kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar, tunahitaji kuandika historia ya kuchukua ubingwa kwa mara ya kwanza,” amesema.
Hababuu amesema, miongoni mwa mechi ambayo imewasaidia zaidi katika kuelekea lala salama ni dhidi ya Fufuni walipoibuka na ushindi wa mabao 2-1 kisiwani Pemba.
Amesema, Fufuni sio timu ya kuibeza kwani ina wachezaji wazuri na wenye uwezo wa kupambana, hivyo kuwafunga wakiwa kwao hilo limewapa uelekeo mzuri wa mbio za ubingwa.
Kocha huyo amesema hana wasiwasi kuhusu ubora wa wachezaji wake kwani wanacheza kwa ari ya kutimiza malengo ya timu ndio maana imekuwa rahisi kupata matokeo mazuri kila mechi. Naye, mfungaji wa bao pekee dhidi ya Uhamiaji, Mussa Majuto, amesema alifanya jitihada zote kuhakikisha timu hiyo inapata ushindi kwa sababu kama wangepoteza hali ingekuwa mbaya upande wao.
Pia mchezaji huyo amewataka mashabiki wa KVZ kuhudhuria uwanjani kwa lengo la kushuhudia timu hiyo ikichukua ubingwa kwani hiyo ndio kiu yao.
