KILIMANJARO: SERIKALI ya Awamu ya Sita imeendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi wa kike nchini kupitia uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya elimu, ambapo zaidi ya Sh bilioni 4.4 zimetumika kujenga Shule ya Sekondari ya Wasichana Kilimanjaro wilayani Siha mkoani Kilimanjaro.
Akizungumza baada ha kukagua shule hiyo leo Mei 29,2026 Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Kenani Kihongosi amesema uwekezaji huo unaonesha dhamira ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha watoto wa kike wanapata elimu bora katika mazingira salama na rafiki.
Kihongosi amesema hayo wakati wa ziara yake shuleni hapo ambapo alikagua utekelezaji wa mradi huo unaojumuisha madarasa, mabweni, nyumba za walimu, maabara pamoja na miundombinu mingine muhimu ya kujifunzia.
“Niwashukuru sana kwa mradi huu mkubwa na mzuri ambao tumeutembelea hapa leo. Hakika ukiutazama unaona ni mradi unaovutia sana na ni uwekezaji mkubwa ambao Rais Samia Suluhu Hassan ameufanya kwa kutoa zaidi ya sh bilioni 4.4,” amesema Kihongosi.
Amesema zamani shule bora za wasichana zilikuwa hazipatikani kwa urahisi katika maeneo mengi nchini, lakini sasa kila mkoa umepewa shule maalum za wasichana ili kuongeza fursa za elimu kwa watoto wa kike.

“Serikali imejenga shule za msingi, sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu kwa sababu tunaamini elimu ni ukombozi mkubwa wa taifa,” amesema.
Aidha, amewapongeza viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Wilaya ya Siha pamoja na wataalamu waliohusika kwa kusimamia vizuri fedha za mradi huo, akisema ubora wa majengo unaonesha wazi kuwa fedha za serikali zimetumika kwa uadilifu.
Kihongosi pia amewataka wanafunzi kutumia fursa ya mazingira bora ya kujifunzia kwa kusoma kwa bidii ili kutimiza ndoto zao na kuleta heshima kwa wazazi na taifa kwa ujumla.
Akitoa taarifa ya mradi huo, Mkuu wa Shule hiyo, Mariana Msangi amesema shule ina wanafunzi 745 kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita, huku mradi huo ukitekelezwa kwa awamu mbili kupitia mradi wa SEQUIP.
Amesema hadi sasa utekelezaji wa awamu ya pili umefikia asilimia 92 huku serikali ikiendelea kuboresha maeneo yaliyosalia ikiwemo ujenzi wa walkways kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum pamoja na uzio wa shule.
