
Dodoma. Wimbi jipya la matumizi ya dawa za kulevya kupitia vyakula na vinywaji limeibua hofu nchini, huku mamlaka zikionya kuwa mbinu hiyo inazidi kuenea kwa kasi na kuwaweka hatarini vijana na watoto wa shule.
Ujanja wa wafanyabiashara wa dawa hizo unaonyesha kuwa bangi na viambata vyake vinaingizwa kwenye bidhaa za kawaida zinazotumiwa majumbani na maeneo ya starehe ikiwemo biskuti, keki, pipi, chokoleti na vinywaji.
Katika taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya ya Mwaka 2025 iliyowasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba Kabudi leo Ijumaa Mei 29, 2026 imeonyesha matumizi ya dawa za kulevya kwenye vyakula yameibua changamoto mpya inayohitaji uangalizi mkubwa wa jamii na vyombo vya dola.
Kwa mujibu wa Profesa Kabudi, baadhi ya wahalifu hutengeneza vyakula hivyo katika viwanda bubu au majumbani kwa lengo la kusambaza kwa siri huku wakikwepa mkono wa sheria.
Amesema tofauti na uvutaji wa bangi, dawa hizi zinapoliwa hupitia tumboni na kwenye ini ambako hubadilishwa kuwa kemikali yenye nguvu inayojulikana kama 11-hydroxy-THC, hali inayoweza kusababisha athari kwa mtumiaji.
Waziri amesema operesheni zilizofanyika mwaka 2025 zinaonyesha mamlaka zilikamata tani 3.2 za bangi aina ya skanka, ikiwemo kilogramu 9.82 zilizokuwa zimechanganywa kwenye biskuti na keki ambapo watuhumiwa 137 walikamatwa kuhusiana na biashara hiyo wakiwemo wanaume 116 na wanawake 21.
Bangi aina ya skanka ni bangi chotara yenye kiwango kikubwa cha kemikali ya THC inayosababisha madhara kwa mtumiaji na inaonyesha bangi hiyo huingizwa nchini kutoka baadhi ya nchi za kusini mwa Afrika na kusambazwa kupitia mitandao ya siri.
Bangi yaongoza
Profesa Kabudi ameitaja bangi kuwa imeendelea kuwa dawa ya kulevya inayoongoza kwa matumizi na ukamataji nchini ambapo taarifa ya Serikali inaonyesha kuwa mwaka 2025 jumla ya tani 1,014.06 za bangi zilikamatwa nchini ambacho ni zaidi ya dawa zingine.
“Katika operesheni hizo, watuhumiwa 7,715 walikamatwa, wakiwemo wanaume 7,014 na wanawake 701, lakini pamoja na hayo,ukamataji wa bangi umepungua kwa zaidi ya asilimia 55 ikilinganishwa na mwaka 2024,” amesema Profesa Kabudi.
Amesema dawa zinazofuata kwa kukamatwa kwa wingi ni mirungi kwani katika kipindi hicho, zinaonyesha kuwa tani 26.36 za mirungi zilikamatwa huku watuhumiwa 1,458 wakikamatwa.
Dawa za viwandani
Kwa upande mwingine taarifa imeonyesha kuwepo kwa ongezeko la dawa za kulevya za viwandani ambazo wataalamu wa afya wanaeleza kuwa zina nguvu na uwezo mkubwa wa kusababisha uraibu.
Kwa mwaka 2025, Serikali ilikamata kilogramu 907.18 za methamphetamine, kilogramu 672.23 za heroin, kilogramu 4.89 za cocaine pamoja na gramu 178 za MDMA maarufu kama ecstasy ambapo kwa mara ya kwanza Tanzania ilikamata tani 29.52 za dawa mpya aina ya Kratom iliyokuwa imeingizwa kwa jina la mbolea.
Serikali imesema kundi la vijana ndio kundi linaloathirika zaidi na matumizi ya dawa za kulevya nchini na sababu zinazochangia hali hiyo ni pamoja na ushawishi wa marafiki, malezi duni, migogoro ya kifamilia, ukosefu wa elimu sahihi na urahisi wa upatikanaji wa dawa hizo.
Juhudi za Serikali
Profesa Kabudi ametaja mikakati ya kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya ni kupunguza uhitaji wa matumizi, kupunguza madhara kwa waraibu pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kitaifa na kimataifa.
Amesema katika kipindi cha mwaka mmoja, watu 85,425 wenye uraibu walipatiwa matibabu bure lengo ni kurudisha nguvu kazi ya Taifa ambayo ingeweza kupotea kutokana na matumizi ya dawa za kulevya.
“Serikali imeendelea kuendesha mashauri mahakamani dhidi ya watuhumiwa wa dawa za kulevya ambapo mwaka 2025 jumla ya mashauri 1,124 yalifunguliwa mahakamani na kati ya mashauri 1,373 yaliyotolewa hukumu, Serikali ilishinda mashauri 1,058,”amesema Waziri Profesa Kabudi.
Katika kipindi hicho, mali zenye thamani ya zaidi ya Sh3.3 bilioni zilizohusishwa na biashara ya dawa za kulevya zilitaifishwa.
Waziri amesema Tanzania imemaliza tatizo la dawa za kulevya aina ya Heroin na imetajwa kuwa ni mfano kwa Dunia katika udhibiti huo ingawa akasema haipaswi kulewa sifa.
Kwa upande wake Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo ameutaja Mkoa wa Morogoro kwamba unaongoza kwa kilimo cha Bangi ukifuatiwa na Mkoa wa Mara, Tabora na Arusha.
Kuhusu meli iliyokamatwa na dawa za kulevya ikiwa na bendera ya Tanzani, Kamishina Lyimo amesema ilikuwa na bendera za Tanzania kweli kutokana na mashirikiano yaliyopo lakini mzigo wake haukuwa umetoka nchini.
