
Dar es Salaam. Ndugu wa kijana Alex Bumbuni aliyefariki baada ya kujirusha chini ya lori daraja la Kijazi, wamesimulia hali aliyokuwa nayo ndugu yao siku chache kabla ya kufikwa na umauti.
Alex aliyekuwa dereva bodaboda mwenye miaka 20, alifariki Jumatano Mei 27, 2026 saa 11 kuelekea 12 jioni baada ya kujirusha kwenye lori ambalo lilikuwa likipita kwa kasi katika eneo la Daraja la Kijazi, Ubungo jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, walisema kabla ya umauti, Alex alionekana akiwa anaongea na simu kwa muda mrefu na ghafla akaivunja kisha kujirusha chini ya gari hilo.
Shughuli za mazishi za kijana huyo zinatarajiwa kufanyika Kivule kwa dada yake baada ya taratibu zote za maziko kukamilika na mwili wake umehifadhiwa Hospitali ya Mwananyamala Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Mei 29, 2026, kaka wa marehemu, Boniface Bumbuni, amesema wamebakiza takribani Sh1 milioni moja ili kuweza kukamilisha taratibu hizo huku wakiwaomba wasamaria wema kujitokeza kuwasaidia ili kuweza kumsitiri ndugu yao.
Wasimulia hali yake kabla ya kufikwa na umauti
Wakisimulia kwa nyakati tofauti hali aliyokuwa nayo ndugu yao siku chache kabla ya kufikwa na umauti, Boniface amesema mara ya mwisho kuwasiliana na mdogo wake huyo ilikuwa siku aliyofikwa na umauti majira ya saa nane kwenda saa tisa mchana.
“Siku hiyo alinipigia akasema braza nina shida na Sh15,000, nikamwambia aaah! Mimi hela ninayo lakini ni ya kodi sababu kodi yangu imeshaisha na pale mama mwenye nyumba ameshanipigia simu akasema ana shida anauguliwa na ndugu yake.
“Kwa hiyo nitakupa lakini sijajua maana mimi siwezi kukuvumilia kwa siku moja au siku mbili kwa hiyo ikifika jioni natakiwa nimpe huyo mwenye nyumba, akanijibu usijali mimi saa 11 nitakurudishia,” ameeleza Boniface.
Baada ya hapo amesema alimpigia mke wake simu ambapo hela ilikuwa kwenye simu yake na kumtaka amtumie marehemu lakini ajabu hakumrudia kumwambia asante au kumtaarifu kwamba aliipata na hapo ndio alikuwa amesikia sauti yake kwa mara ya mwisho mpaka alipopata taarifa za kifo chake.
Kwa mujibu wa Boniface na mdogo wake huyo, huwa wakisaidiana hela pindi anapokwama, hivyo hakuwa na mashaka naye kwamba hela hiyo hatairudisha kwani katika maisha yake pia alikuwa mtu mwaminifu.
“Mdogo wangu alikuwa si tu mwaminifu, bali mpambanaji katika maisha, anafanya kazi kwa bidii na hata mimi kuna wakati namwambia nimekwama familia nyumbani haina kitu cha kula, ananisaidia na kwa kiasi kikubwa yeye ndio alikuwa kimbilio langu,” amesema kaka huyo.
Ukiacha kumkopa yeye, pia amesema Alex alimkopa Sh450,000 bosi wake aliyekuwa akifanya naye kazi za kupeleka mizigo kwa wateja mwenye duka la vipodozi maeneo ya Sinza Madukani.
Kwa mujibu wa kaka huyo, Alex alianza kukopa hela kwa watu siku moja kabla ambapo kwa bosi wake awali alichukua Sh200,000, kesho yake akachukua Sh150,000 halafu baada ya saa moja akarudi kumuomba tena Sh100,000.
“Baada ya bosi wake kuona hivyo, alimuuliza kulikoni kuchukua hela zote hizo, alimdanganya kuwa baba anaumwa na amefanyiwa operesheni,” amesimulia Boniface.
Hata hivyo amesema hakuiishia hapo kwani aliomba tena Sh50,000 na hapo bosi wake ndipo alipozidi kumuhoji mbona hela anayoichukua ni nyingi.
“Hapa akambadilishia Kiswahili na kumwambia ana ndugu yake yuko Ulaya ndio anamtumia hizo hela, bosi akamuomba ampe namba yake ampigie ili ajue anataka kiasi gani na atamrudishia kwa muda gani.
“Alimjibu kwamba hana simu kwa wakati huo na kumuomba ampe muda aende akaichukue nyumbani lakini tangu alivyoondoka ndio hakurudi tena.
“Kama haitoshi siku hiyo pia inaelezwa alimuomba dada yake Sh70,000 kwa kile alichomueleza anataka kwenda Tanga kwa kumweleza bosi wake wa vipodozi kafungua duka jingine huko anatakiwa akapange vitu dukani na hela hiyo angeitumia kwa nauli.
Kuhusu taarifa za kifo, Boniface amesema aliposikia kutoka kwa bosi wake aliyempa pikipiki, hakuamini mpaka pale alipofika ofisini kwake na kumuonyesha video ambapo baada ya hapo walienda kuuthibitisha mwili Hospitali ya Mwananyamala na kumtambua kuwa ni yeye.
Kutokana na mazingira yaliyomkuta kabla ya umauti, Boniface ameomba msaada wa kufuatilia mawasiliano yake kujua ni nani hasa walikuwa wanawasiliana ikiwemo miamala waliokuwa wakimtumia labda kuna alipokuwa akiipeleka.
Kwa kufanya hivyo amesema huenda wakapata pa kuanzia na kujua chanzo cha kuchukua maamuzi ya kujiua kwa njia hiyo ukizingatia alikuwa bado kijana mdogo, huenda pia ikatumika kama funzo kwa vijana wengine wanaokabiliwa na changamoto za kifedha.
Kaka yake mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Bumbuti Mtubutu ambaye walikuwa wakiishi naye chumba kimoja, amesema siku ya Jumatatu Mei 25, ndugu yake huyo aliomba amkope Sh50,000.
Hata hivyo Mtubutu amesema alishindwa kumpatia fedha hiyo kwa kuwa ndio alikuwa katoka kulipa kodi na kumuomba amvumilie hadi wiki inayofuata.
“Baada ya majibu hayo akaniambia kwani wewe hapo kwa sasa una Shilingi ngapi, nikamwambia ninayo kidogo ambapo nikiangalia na matumizi yangu nikisema nikupatie nitabaki sina kitu, akanijibu basi haina shida, nadhani hapo ndio akampigia dada kumuomba,” amesema kaka huyo.
Hata hivyo siku anafikwa na umauti amesema aliondoka akamuacha bado kalala lakini alimwambia kuwa ana safari ya kwenda Tanga na atakaa huko kwa wiki moja.
“Ilipofika jioni na kurejea nyumbani amesema sehemu walipokuwa wakihifadhi funguo ya chumba chao hakuikuta ikabidi ampigie simu, ikaaita mara ya kwanza akakata, nikapiga tena mara ya pili ikaita akakata, ikabidi nimtumie ujumbe kumuuliza dogo ufunguo umeweka wapi, hakunijibu.
“Nikajipa moyo kuwa kwa kuwa nimeshamtumia sms, huenda yupo busy ofisini hivyo atakuja tu, nikaondoka nikaenda kwa jamaa zangu na ilipofika saa 12 jioni nikarudi lakini akawa bado hajafika na nikaamua tena kumpigia simu lakini hakupatikana moja kwa moja.
“Nikasema labda yupo busy, ikabidi nivunje kufuli niweze kuingia ndani. Japo huwa wakati mwingine anachelewa kurudi lakini usiku huo nililala nikiwa na hofu kubwa sana japo nikajipa moyo kwa kuwa alishaniambia atakuwa na safari huenda kaondoka ghafla,” amesema Mtubutu.
“Pia pamoja na kuona clip ikisambaa mitandaoni kuhusu bodaboda aliyefariki daraja la Kijazi sikuitilia maanani na ilipofika saa nne usiku ndio nikapigiwa simu na kaka kwamba mdogo wetu katuacha.
“Hata hivyo baada ya taarifa hizo ndio nikapata kumbukumbu kuwa kuna karatasi na kalamu aliviona kwenye meza ya redio na kuonekana kama kuna kitu alitaka kukiandika lakini akaahirisha.
“Pia wiki moja nyuma alishawahi kumwambia aliagiza simu Dubai ya Sh500,000 na alivyomuuliza uliyemuagiza umfahamu, akamjibu si unajua biashara za mitandaoni na hata baadaye nilipomuuliza kama alishaletewa hakunipa majibu ya kueleweka.”
Kwa mujibu wa kaka zake, katika familia yao wamezaliwa watoto sita, Alex akiwa mtoto wa tano katika familia ya Mzee Mtabutu Bumbuni na Pili Machopa.
