Chato. Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi amefichua namna aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2015, Dk John Magufuli, alivyomweleza kuwa tofauti za kimawazo na kubishana katika mijadala ya kisiasa, hazipaswi kuchukuliwa kama uadui.
Dk Nchimbi amesema hayo leo Mei 29, 2026 alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, kwenye mazishi ya Sussana Ngolo Mussa, mama mzazi wa hayati Magufuli, yaliyofanyika nyumbani kwake Chato, mkoani Geita.
Marehemu Sussana alifariki dunia Mei 25, 2026 baada ya kusumbuliwa na tatizo la moyo, kisukari na shinikizo la damu kwa muda mrefu.
Mazishi hayo yamehudhuriwa pia na makamu wa Rais mstaafu, Dk Philip Mpango, Waziri Mkuu mstaafu, Kassim Majaliwa, Naibu Waziri Mkuu mstaafu, Dk Doto Biteko, Spika mstaafu Dk Tulia Ackson na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Stephen Wasira.
Dk Nchimbi kwenye hotuba yake ameweka wazi ujumbe aliotumiwa na Magufuli akimweleza kwamba kutofautiana mawazo na kubishana si uadui.
Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Emmanuel Nchimbi, akizunguma na waombolezaji wakati wa mazishi ya marehemu Suzana Ngolo Magufuli ambaye ni Mama wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dk John Magufuli, yaliyofanyika leo Ijumaa Mei 29, 2026 Kilimani Wilayani Chato.
Amesema ujumbe huo ulikuwa wa kumtia moyo baada ya yeye (Nchimbi) kusema anastaafu siasa, baadaye Magufuli alimteua kuwa balozi nchini Brazil.
“Mungu atakusaidia, siwezi kukutupa mdogo wangu nilikwishaahidi kwamba mimi (Magufuli) ni pamoja na wewe, haijalishi yaliyopita yamepita, wewe bado ni kijana siwezi kuharibu ‘future’ yako, natambua kazi nzuri ulizofanya kwa nchi hii, kutofautiana mawazo na kubishana bishana siyo uadui, salamu kwa familia,” ulisema ujumbe huo aliotumiwa Dk Nchimbi na hayati Magufuli.
Wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais CCM mwaka 2015, kuliibuka sintofahamu baada ya Edward Lowassa kuenguliwa na Kamati Kuu, pale wajumbe watatu – Dk Nchimbi, Adam Kimbisa na Sophia Simba walipojitokeza mbele ya wandishi wa habari na kutangaza kujitenga na maamuzi hayo, kwa kuwa wao waliamini aliyestahili alikuwa Lowassa.
Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Emmanuel Nchimbi, akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu Suzana Ngolo Magufuli ambaye ni Mama wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dk John Magufuli, wakati wa mazishi yaliyofanyika leo Ijumaa Mei 29, 2026 Kilimani Wilayani Chato.
Baada ya sekeseke hilo Dk Nchimbi aliamua kustaafu siasa, hatua iliyosababisha Magufuli ampe ushauria ambao kwa mara ya kwanza ameutangaza kwenye mazishi hayo.
Amesema baada ya yeye kutangaza kustaafu siasa, Wasira (sasa makamu mwenyekiti CCM) alimpigia simu akimtaka kubatilisha uamuzi wake.
“Emmanuel mdogo wangu hivi umepata wazimu? Nani amekwambia siasa tunastaafu? Wewe unakuwa mpinzani wa demokrasia, unapogombea ukashinda unashukuru na ukishindwa unashukuru na uchaguzi ujao unarudia tena, sasa mambo gani unaanzisha?” Dk Nchimbi alisema yalikuwa ni maneno ya Wasira.
Dk Nchimbi amesema baada ya simu ya Wasira ilifuata simu ya Magufuli akimweleza maneno ya kumtia moyo kama mdogo wake kwa umri na baadaye bnaada ya kuwa Rais akamteua kuwa Balozi Brazil.
Dk Nchimbi alinukuu maneno ya Magufuli kwamba: “Mtani hivi niliyoyasikia ni kweli au wanasema uongo? Unapumzika siasa? Nikamwambia ni kweli, akasema (Magufuli) katika umri huo mimi sijapumzika na nimekuzidi miaka 10.”
Amesema Dk Magufuli alimwambia akishinda urais atampatia nafasi ya ubunge kati ya nafasi 10 alizonazo kikatiba za uteuzi wa wabunge, lakini yeye (Dk Nchimbi) hakuwa tayari.
Dk Nchimbi ameongeza kuwa baada ya uchaguzi mkuu kupita, alikaa mwaka mzima nje ya siasa hali iliyomfanya (Magufuli) kumpigia tena simu akitaka kufahamu kama amebadili uamuzi wa kupumzika.
“Hayo mapumziko hayajaisha mtani? Nikamwambia hapana, nimeamua kupumzika siasa,” amesema Dk Nchimbi alivyoulizwa tena na Rais Magufuli.
Amesema baada ya kauli hiyo, Rais Magufuli alimteua Dk Nchimbi kuwa Balozi nchini Brazil, jambo ambalo amesema asingeweza kupinga uteuzi wa Rais.
Pia, Dk Nchimbi amesema Rais Magufuli hakupenda kukomaa na jambo fulani kama wengi wanavyodhani, badala yake alipenda mabishano yenye hoja, na yeye (Nchimbi) alipenda kubishana naye walipokuwa wakikaa pamoja bungeni kwa miaka mitatu.
Amemtaja marehemu Sussana kuwa alikuwa na malezi bora akitolea mfano wa Dk Magufuli, kwamba alikuwa na utashi wa kulea na kuandaa viongozi wengine ili waje kulitumikia taifa.
Amesema wazazi wanao wajibu wa kulea watoto kwa kuwaandaa kulitumikia taifa ambapo amesema kufanya mema kwa binadamu mwenzako siyo lazima yalipwe kwako.
Askofu wa Jimbo Katoliki la Bunda, Simon Masondole, akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), ametoa wito kwa jamii kumuenzi marehemu Sussana Ngolo Mussa kwa kuendeleza malezi bora na kudumisha mshikamano wa kitaifa.
Askofu Masondole amesema maisha ya marehemu yanapaswa kuwa chachu ya kuimarisha maadili katika familia na jamii, huku akisisitiza umuhimu wa taifa kuendelea kushikamana katika misingi ya amani, upendo na umoja.
Amesema kuwa malezi bora ni msingi muhimu wa kuijenga jamii yenye maadili, hivyo akawahimiza Watanzania kuiga mfano wa maadili mema kama sehemu ya kumuenzi marehemu.
Kwa upande mwingine, akitoa salamu za shukrani kwa niaba ya familia, Simon Michael ameishukuru Serikali, madaktari na wahudumu wa afya pamoja na wananchi kwa kuwa karibu na familia wakati wote wa matibabu na malezi ya marehemu hadi alipofikwa na mauti.
Waombolezaji wakiwa katika mazishi ya marehemu Suzana Ngolo Magufuli ambaye ni Mama wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dk John Magufuli, yaliyofanyika leo Ijumaa Mei 29, 2026 Kilimani Wilayani Chato.
Amesema msaada huo wa karibu umeonyesha upendo wa kweli na mshikamano, akibainisha kuwa familia inathamini sana mchango huo katika kipindi chote cha changamoto ya ugonjwa na matibabu.
Ilivyokuwa CCM
Mwaka 2015 wajumbe watatu wa Kamati Kuu ya CCM, Dk Nchimbi, Sophia Simba na Kimbisa walitangaza mbele ya waandishi wa habari kujitenga maamuzi ya Kamati Kuu ya kumwengua Edward Lowassa kwenye kinyang’anyiro cha kuteuliwa kuwa mgombea urais wa CCM kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Tukio hilo lilitokea Julai 2015 mjini Dodoma wakati CCM ikiwa kwenye hatua za mwisho za mchujo wa majina ya watia nia wa urais kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka huo.
Nchimbi, Kimbisa na Simba walieleza kuwa waliona ulazima wa kuweka wazi msimamo wao kutokana na kile walichodai kuwa ni kutotendewa haki kwa baadhi ya wagombea waliokuwa na uungwaji mkono mkubwa ndani na nje ya CCM.
Baadaye, Lowassa alihamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kuwa mgombea urais wa Chadema chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, hatua iliyobadilisha kwa kiasi kikubwa taswira ya siasa za ushindani nchini.
Miaka miwili baadaye, Machi 2017, Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM ilichukua hatua dhidi ya makada hao kwa madai ya kukisaliti chama wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Katika maamuzi hayo, Sophia Simba alivuliwa uanachama wa CCM na kupoteza nafasi zake zote za uongozi ndani ya chama. Hata hivyo, baadaye mwaka huo alirejeshewa uanachama wake baada ya mchakato wa maridhiano ndani ya chama.
Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Emmanuel Nchimbi, viongozi mbalimbali pamoja na familia, wakishuhudia mwili wa marehemu Suzana Ngolo Magufuli ambaye ni Mama wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dk John Magufuli, ukishushwa kaburini wakati wa mazishi yaliyofanyika leo Ijumaa Mei 29, 2026 Kilimani Wilayani Chato.
Kwa upande wake, Dk Nchimbi alipewa onyo kali na kutakiwa kuomba radhi kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni ukiukwaji wa maadili na misingi ya chama.
Adam Kimbisa alisamehewa na chama baada ya hatua za ndani za nidhamu kufanyika.
