Serengeti Boys gumzo AFCONSerengeti Boys gumzo AFCON

TAKWIMU za fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 (AFCON U17) zinazoendelea huko Morocco, ni uthibitisho wa ubora wa kitimu na mchezaji mmoja ambao timu ya vijana ya Tanzania kwa umri huo ‘Serengeti Boys’ inaonyesha katika mashindano hayo.

Timu hiyo juzi ilifuzu kuingia hatua ya fainali baada ya kuichapa Misri kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya mechi hiyo ya nusu fainali kumalizika kwa sare tasa ndani ya dakika ya 90.

Wakati ikijiandaa na mechi ya fainali dhidi ya Senegal ambayo itachezwa Jumanne ijayo, Serengeti Boys imeonekana kuwa ndio timu yenye takwimu bora zaidi katika nyanja tofauti za mashindano kulinganisha na timu nyingine.

SERE 01

Ndio timu ambayo inaongoza kwa kufumania nyavu mara nyingi zaidi ikifanya hivyo mara 10 ikifuatiwa na Algeria iliyopachika mabao nane.

Inashika nafasi ya tatu katika orodha ya timu zilizoruhusu mabao machache huku zinazoongoza zikiwa ni Mali na Cameroon ambazo kila moja imefungwa mabao matatu.

Serengeti Boys inaongoza kwa kuwa timu iliyocheza idadi kubwa ya mechi bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa (clean sheets) ikifanya hivyo mara tatu.

Kwa upande wa mchezaji mmojammoja, hadi sasa Serengeti Boys ina mchezaji anayeongoza kwa kufumania nyavu, kinara wa kucheza mechi nyingi bila kuruhusu bao na pia kwa ushindi wa tuzo za mchezaji bora wa mechi.

Kipa Haji Abdallah anaongoza kwa kucheza mechi tatu bila kuruhusu bao na kinara wa ufungaji hadi sasa ni Dismas Athanas mwenye mabao matatu.

SERE 02

Issa Chole ndiye mchezaji anayeongoza kwa kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mechi mara nyingi kwenye mashindano hayo akifanya hivyo mara mbili. Kocha wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger ameipongeza Serengeti Boys akisema imeonyesha kiwango bora.

“Hongera Tanzania (Serengeti Boys) mmefanya vizuri kupitiliza na sisi FIFA tunaona fahari kwenu kwa sababu mmecheza soka la kuvutia. Hongera pia kwa Misri. Nategemea kuwaona muda mfupi ujao katika Kombe la Dunia,” amesema Wenger ambaye kwa sasa ni mkuu wa Maendeleo wa Fifa.

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Paul Makonda ameahidi usimamizi mzuri wa wachezaji wa Serengeti Boys huku akiomba mikoa iandae mikusanyiko ya kuonyesha mechi ya fainali ya Serengeti Boys.

“Nami naomba kutumia nafasi hii kuwaomba wakuu wa mikoa. Siku ya Jumanne, vijana hawa Serengeti Boys watakuwa wanacheza na timu ya Senegal. Basi kila mkoa kwa kuwaunga mkono, tuweke luninga kubwa kuangalia heshima inayojengwa na vijana wetu wa Kitanzania ikiwa ni sehemu ya kuweka hamasa.

“Vijana hawa hawataenda kwa mameneja uchwara. Wanaenda katika vituo vya michezo vya kimataifa,” amesema Makonda.

SERE 03

Sababu wawili Serengeti kuitwa Stars

BENCHI la Ufundi la Taifa Stars, limewaongeza kikosini wachezaji wawili wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 maarufu Serengeti Boys baada ya kukoshwa na viwango wanavyoonyesha katika Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON U-17) zinazoendelea Morocco. Wachezaji hao ni mshambuliaji Luqman Mbalasalu na beki Kassim Juma.

Taarifa ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imesema wawili hao watakuwa sehemu ya kikosi cha Taifa Stars katika mechi mbili za kirafiki dhidi ya Uganda na Rwanda mwezi ujao. Hata hivyo, sababu kuu ya mastaa hao kuitwa kwenye kikosi cha Stars ni kiwango bora ambacho wamefanikiwa kukionyesha kwenye michuano hiyo mikubwa Afrika.

Mechi hizo ambazo zipo katika kalenda ya Fifa ya kwanza itakuwa Juni 5 dhidi ya Uganda na Juni 9 dhidi ya Rwanda.

Katika fainali hizo, Luqman amechangia mabao mawili ambapo amefunga moja na kupiga pasi moja ya mwisho. Kwa upande wa Kassim amekuwa mchezaji tegemeo katika safu ya ulinzi ya Serengeti Boys ambayo haijaruhusu bao katika mechi tatu kati ya tano ilizocheza za mashindano hayo.

Kassim pia ndiye nahodha wa kikosi cha Serengeti Boys ambacho kimetinga hatua ya fainali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *