Marekani. Msanii wa Hip Hop Marekani, Lil Wayne (43), anaripotiwa kumchumbia kwa siri binti mwenye umri wa miaka 20 kutokea jimbo la Indiana nchini humo, jambo ambalo limeacha maswali kuhusu mtindo wa maisha wa rapa huyo.

Lil Wayne aliyevuma zaidi kupitia ngoma yake, Lollipop (2008), anarejea tena katika vichwa vya habari akihusishwa na uhusiano mpya akiwa tayari ni baba watoto wanne kutoka kwa wanawake wanne tofauti.

Kulingana na TMZ, Lil Wayne alimchumbia kimya kimya ‘mtoto huyo wa 2000’ mapema mwaka huu lakini hadi sasa bado hajatoa taarifa rasmi kuhusiana na jambo hilo licha ya mtandao huo kuwasiliana na watu wake wa karibu ili kupata maelezo zaidi.

Lil Wayne, Mtendaji Mkuu wa Young Money Entertainment, katika miaka ya hivi karibuni amekuwa akiweka maisha yake binafsi mbali na vyombo vya habari na hata mitandao ya kijamii, hatua iliyopelekea uchumba huo kubaki siri kwa muda mrefu.

Hayo yanajiri baada ya Mei mwaka uliopita, mpenzi wa muda mrefu wa Lil Wayne, Denise Bidot kumtuhumu rapa huyo kwa kumnyanyasa kimwili na kihisia kisha kumuacha siku ya kinamama duniani.

“Lil Wayne amenifukuza mimi na binti yangu siku ya kinamama leo. Ndio tu nimepona kutoka kwenye upasuaji. Zimepita wiki tano tu baada ya kufanyiwa upasuaji wa kurekebisha mwili mzima. Siwezi hata kuinua chochote kile,” alieleza Denise.

Mwaka 2010, Lil Wayne akiongea na Jarida la Ozone alifunguka kuhusu ukosoaji ambao anaokumbana nao kwa kuzaa na wanawake wanne tofauti akisema hajali kile ambacho watu wanafikiri au kusema.

Mtoto wake wa kwanza, Reginae Carter alizaliwa Novemba 29, 1998, wakati huo Lil Wayne akiwa na umri wa miaka 16. Mama wa mtoto huyo ni Toya Johnson ambaye walifunga ndoa mwaka 2004 lakini walikuja kuachana kwa talaka mwaka 2006.

Utakumbuka Lil Wayne alivuma baada ya kuachia albamu yake ya nne, Tha Carter (2004), albamu yake ya sita, Tha Carter III (2008) ilimpa heshima zaidi kufuatia kushinda tuzo ya Grammy kama Albamu Bora ya Rap.

Albamu ya Tha Carter III ilikuwa na nyimbo kali zilizompa heshima kubwa rapa huyo, baadhi ya nyimbo hizo ni A Milli, Got Money na Lollipop ambao uliandika rekodi kama wimbo wake wa kwanza kushika nafasi ya kwanza kwenye chati za Billboard Hot 100.
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *