Dar es Salaam. Rasmi imetimia miaka minne bila mwimbaji na mwanamitindo, Hamisa Mobetto (31), kusikika katika muziki licha ya kuwa tayari alishaanza kupata mashabiki upande huo na hata kutengeneza nyimbo maarufu.
Hamisa, mkali wa kibao cha Ex Wangu Remix (2021), ni kama alishapanga iwe hivyo na ndio sababu aliamua kuachia Extended Playlist (EP) yake, Your Truly (2022) ambayo ndio mradi wake wa mwisho katika uimbaji.
EP hiyo ilisimamiwa na Mobetto Music ikiwa na jumla ya nyimbo sita, ilitoka Mei 27, 2022. Hivyo wiki hii imetimiza miaka minne tangu mashabiki walipoisikiliza kwa mara ya kwanza.
Hamisa aliwashirikisha wasanii wawili katika EP hiyo ambao ni Otile Brown kutokea Kenya pamoja Korede Bello wa Nigeria, huku watayarishaji wakiwa ni Mocco Genius, Abbah Process, S2kizzy n.k.
Ndani ya EP hiyo yenye dakika 16, Hamisa ameimba miondoko mbalimbali ikiwamo Bongofleva, Baibuda, Afropop na Singeli ambayo ndio hasa anaiwezea na ndio iliyompatia wimbo wake maarufu zaidi, Ex Wangu Remix (2021) akishirikiana na Seneta Kilaka.
Hamisa, Miss XXL After School Bash 2010, aliwahi kudai tangu akiwa mdogo alipenda sana kuja kuwa mwanamuziki ila kutokana na kutafuta fedha akajikuta ameingia kwenye filamu na mitindo kabla ya muziki.
Mnamo Agosti 2018, ndipo aliachia wimbo wake wa kwanza ‘Madam Hero’ uliotayarishwa na C 9, huku Januari 2019 akifanya show yake ya kwanza pamoja na mastaa wengine kama Lady Jaydee, Aslay, Christian Bella na Ruby.
Licha ya kuwa kimya kimuziki, hadi sasa Hamisa ni miongoni mwa wasanii
wa kike Bongo ambao nyimbo zao zimefanya vizuri katika mitandao, mathalani tayari kazi zake zimeshatazamwa mara milioni 25.3 YouTube hadi sasa.
Ikumbukwe mbali na kuwa mwimbaji, Hamisa aliwahi kuwa video vixen ambapo alifanya kazi na waimbaji kama Abdukiba (Hatuna Habari Nao), Barnaba (Magubegube ), Diamond Platnumz (Mawazo & Salome), Quick Rocka (My Baby), na Alikiba (Dodo).
Kwa hiyo ni video vixen na mwigizaji mwingine aliyejaribu bahati yake kwenye Bongofleva kama ilivyo kwa kina Gigy Money, Amber Lulu, Lyyn, Nai, Caren Simba, Snura, Shilole na Rose Ndauka ambaye alikuja na EP yake, Majibu Rahisi (2025).
Hata hivyo, Hamisa si msanii pekee wa kike Bongo kukaa kimya muda mrefu, kuna Queen Darleen ambaye ana miaka zaidi ya sita bila kutoa wimbo wake binafsi.
Queen Darleen, msanii wa WCB Wasafi, mara ya mwisho kutoa wimbo ilikuwa Machi 11, 2020 alipoachia ngoma yake ‘Bachela’ akimshirikisha Lava Lava huku Abby Dady na Rash Don wakihusika katika utayarishaji.
Hamisa amekuwa kimya kimuziki lakini bado anaendelea na kazi yake ya ushawishi wa chapa mtandaoni (influencer) akiwakilisha na kutangaza bidhaa, huduma na hata kuongoza kampeni mbalimbali anazopatiwa na washirika wake.
Hii ndio kazi inayomweka bize sana kwa sasa kwa sababu anafanya kazi na kampuni, taasisi na mashirika mbalimbali ambayo yanazidi kumwamini kutokana na jinsi alivyoiweka chapa (brand) yake mbele ya jamii.
Kwa asilimia kubwa Hamisa anatumia mitandao ya kijamii hasa Instagram ili kufanisha shughuli hizo akiwa na mamilioni ya wafuasi (followers) ambao wengi wao amewapata kutoka na muziki, uigizaji na hata mtindo wake wa maisha.
Kwenye moja ya mahojiano yake, aliwahi kueleza kuwa ukurasa wake wa Instagram ndio kila kitu kwake kwa sababu umemfungulia fursa nyingi ambazo sasa zinampatia fedha ya kuendesha maisha yake kwa sehemu.
Utakumbuka Hamisa ndiye mwanamke mwenye wafuasi wengi Instagram hapa Tanzania akiwa nao milioni 12.2, na kwa ujumla anashika nafasi ya tatu. Hiyo inamfanya kuhesabika kuwa miongoni mwa watu wenye nguvu ya ushawishi mtandaoni na ndio sababu ya kupata dili hizo.
Mbali na kazi hiyo, pia maisha binafsi ya Hamisa yamekuwa na shughuli nyingi, mathalani Julai 2025, alikuwepo Marekani kumuunga mkono mumewe Aziz Ki katika michuano ya Kombe la Dunia la Klabu akiwa na Wydad AC.
Hatua hiyo ilikuja takribani mwezi mmoja tangu Aziz Ki kujiunga na miamba hiyo ya Morocco ambapo pia Hamisa aliongozana naye siku aliyoenda kusaini mkataba ikiwa ni muda mfupi tu baada ya kuondoka Yanga SC ambapo alicheza kwa mafanikio.
Utakumbuka Aziz Ki ambaye kwa sasa anaichezea Al Ittihad ya Libya, alifunga ndoa na Hamisa hapo Februari 16, 2025 katika msikiti wa Masjid Nnuur uliopo Mbweni, Dar es Salaam, ikiwa ni siku moja baada ya mahari kutolewa.
Hamisa alilipiwa mahari ya ng’ombe 30 na fedha kiasi cha Sh30 milioni ambapo Rais wa Yanga, Mhandisi Heris Said ndiye alikabidhi kwa niaba ya familia ya bwana harusi kutokea nchini Burkina Faso.