Musoma. Serikali mkoani Mara imewaagiza wataalamu wake kutumia vyombo vya habari kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo na kijamii ili kuchochea maendeleo endelevu katika jamii.

Pia, waandishi wa habari mkoani humo wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili ya taaluma na kutumia vyombo vyao kuelimisha jamii kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo tamaduni za Kitanzania ili kukabiliana na mmomonyoko wa maadili.

Wito huo umetolewa leo Mei 30, 2026 mjini Musoma na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi wakati wa uzinduzi wa kituo cha redio cha GM FM.

Kanali Mtambi amesema vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kuleta maendeleo endapo vitatumika kwa usahihi.

Baadhi ya wananchi wakiwa kwenye uzinduzi wa kituo cha radio cha GM FM mjini Musoma. Picha na Beldina Nyakeke

Amesema umefika wakati wa kutumia njia mbalimbali za mawasiliano, ikiwemo vyombo vya habari, kuwafikishia wananchi elimu ya maendeleo na masuala ya kijamii kwa wakati na kwa watu wengi zaidi.

“Kuna watu wanafanya ufugaji, kilimo, biashara na shughuli za madini lakini wengi wao wanafanya bila uelewa wa kutosha. Wanahitaji miongozo kutoka kwa wataalamu wetu, na kwa kuwa si rahisi kuwafikia wote kwa wakati mmoja, tumieni vyombo vya habari kuwafikia,” amesema.

Ametoa mfano wa umuhimu wa wataalamu wa afya kutumia vyombo vya habari kutoa elimu kuhusu huduma za kliniki kwa wajawazito ili kusaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.

Kanali Mtambi amesema hakuna sababu ya wananchi kuendelea kufanya shughuli zao kwa mazoea wakati wataalamu wana uwezo wa kuwapa elimu ya kisasa itakayoongeza tija na ufanisi.

Amesema vyombo vya habari vinaweza kuwa nyenzo muhimu ya maendeleo, lakini vikitumika vibaya vinaweza kuleta madhara makubwa kwa jamii.

“Waandishi wa habari tumieni vyombo vyenu kuleta mshikamano, umoja na amani. Vyombo hivi vikitumika vizuri vitasaidia kupambana na mmomonyoko wa maadili, ukatili wa kijinsia na vitendo vingine visivyofaa katika jamii,” amesema.

Amempongeza mmiliki wa GM FM kwa kuwekeza mkoani Mara akisema kituo hicho kitasaidia kutoa ajira na kuwa jukwaa la kuwaunganisha wananchi na Serikali.

Awali, Mkurugenzi wa GM FM, Michael Kembaki amesema kituo hicho kimeanzishwa kwa lengo la kuchochea maendeleo ya jamii mkoani Mara.

“Tunalenga kuwafikia wafugaji, wavuvi, wachimbaji madini, wanawake, vijana na wazee. Hatutaki kumuacha mtu nyuma, tunataka redio hii iwe sehemu ya kuhamasisha maendeleo ya mkoa wetu,” amesema.

Kwa upande wake, Meneja wa kituo hicho, Nyambili Yohana amesema GM FM imejipanga kutoa huduma kwa jamii kwa weledi huku ikilenga kuwa daraja kati ya wananchi na mamlaka mbalimbali katika kutatua changamoto za kijamii.

“Tutaendelea kuhamasisha amani, umoja na maadili ya Kitanzania. Pia tutahakikisha wananchi wanapata habari sahihi zenye ukweli bila kupotosha jamii,” amesema.

Amesema kituo hicho pia kitahamasisha wananchi kutumia fursa mbalimbali zilizopo mkoani Mara ili kuboresha maisha na uchumi wao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *