
Dar es Salaam. Licha ya juhudi mbalimbali za Serikali na wadau wa maendeleo kuboresha upatikanaji wa pedi za kike nchini, gharama kubwa za bidhaa hizo, upatikanaji mdogo hasa katika maeneo ya vijijini na unyanyapaa unaoendelea katika jamii bado vinatajwa kuwa vikwazo vikubwa vinavyowakabili mamilioni ya wasichana na wanawake Tanzania.
Changamoto hizo si suala la usafi wa mwili pekee, bali zinaathiri pia elimu, afya, ushiriki wa wanawake katika shughuli za kiuchumi na heshima yao katika jamii.
Hayo yamebainishwa katika utafiti wa soko uliofanywa na kampuni ya KPMG kwa niaba ya Msichana Initiative, uliolenga kuchunguza athari za kiuchumi za mageuzi ya kodi yaliyowahi kufanyika na yanayopendekezwa pamoja na uwezekano wa kutambua pedi za kike kama bidhaa muhimu za afya.
Utafiti huo ulifanyika ili kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha sera na mikakati ya kuongeza upatikanaji wa bidhaa za hedhi kwa gharama nafuu kwa wasichana na wanawake nchini.
Matokeo ya utafiti yanaonyesha kuwa pamoja na hatua zilizochukuliwa na Serikali katika miaka ya hivi karibuni, bado bei za bidhaa hizo zimeendelea kuwa changamoto kwa makundi mengi yenye kipato cha chini.
Mwaka 2017, Serikali iliondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye pedi za kike kwa lengo la kupunguza bei na kuongeza upatikanaji wake kwa wananchi wenye kipato cha chini.
Hata hivyo, msamaha huo uliondolewa mwaka uliofuata.
Baadaye, Serikali ilifanya marekebisho katika mifumo ya kodi za kampuni na ushuru wa bidhaa kwa lengo la kuhamasisha uzalishaji wa ndani na kupunguza gharama za uzalishaji.
Hata hivyo, utafiti huo unaonyesha kuwa hatua hizo hazikuleta matokeo makubwa yaliyotarajiwa katika kushusha bei za bidhaa hizo wala kuongeza upatikanaji wake kwa makundi yaliyo hatarini zaidi.
Aidha, utafiti umebaini kupungua kwa kiasi cha pedi za kike zinazoingizwa nchini na kuwepo kwa tofauti kubwa ya bei kati ya bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi na zile zinazoagizwa kutoka nje, hali inayochangia changamoto ya upatikanaji kwa watumiaji wengi.
“Matokeo hayo yanaonyesha wazi kuwa bado kuna haja ya kuchukua hatua za ziada ili kuhakikisha wasichana na wanawake wanapata bidhaa za hedhi kwa bei nafuu na kwa urahisi zaidi,” amesema Mkurugenzi wa Msichana Initiative, Consolata Chikoti.
Amesema tofauti kubwa ya bei kati ya pedi zinazozalishwa ndani ya nchi na zile zinazoagizwa kutoka nje inaashiria umuhimu wa kuwekeza zaidi katika ubunifu wa ndani na matumizi ya malighafi zinazopatikana nchini ili kupunguza gharama za uzalishaji.
“Endapo tutaimarisha uzalishaji wa ndani kwa kutumia teknolojia na malighafi zinazopatikana hapa nchini, tunaweza kuongeza upatikanaji wa bidhaa bora za hedhi kwa gharama nafuu zaidi kwa wasichana na wanawake wengi,” amesema.
Utafiti huo pia unapendekeza mapitio ya sera za kodi na uainishaji wa pedi za kike kama bidhaa muhimu za afya, hatua ambazo zinaweza kusaidia kupunguza gharama kwa watumiaji wa mwisho.
Amesema pamoja na hatua za kiuchumi, kuna haja ya kuboresha mifumo ya usambazaji wa bidhaa hizo, hususan katika maeneo ya vijijini, na kuimarisha upatikanaji wa maji safi na vyoo salama shuleni na katika jamii.
Consolata amesema vita dhidi ya changamoto za afya ya hedhi haviwezi kufanikiwa bila kuondoa unyanyapaa na dhana potofu zinazozunguka suala hilo.
“Tunahitaji kampeni endelevu za elimu kwa umma ili kuvunja ukimya na kuondoa aibu inayowazuia wasichana wengi kupata taarifa sahihi na msaada wanaouhitaji,” amesema.
Amesisitiza kuwa upatikanaji wa bidhaa za hedhi kwa gharama nafuu si suala la afya pekee bali ni suala la usawa wa kijinsia na haki za msingi.
“Hakuna msichana au mwanamke anayepaswa kukosa fursa za elimu, maendeleo au ustawi kwa sababu ya kushindwa kumudu au kupata bidhaa za hedhi zinazomwezesha kuishi kwa heshima,” amesema Consolata.
Akiwasilisha mapendekezo ya utafiti huo, mtafiti kutoka KPMG, Geofrey Kamugisha amesema Serikali inaweza pia kuzingatia kuweka udhibiti wa bei za pedi za kike, ingawa suala hilo linaweza kuwa na mjadala mpana, hususan baada ya kutekeleza hatua mbalimbali za kupunguza kodi kwenye bidhaa hizo.
Amesema hatua hiyo inaweza kusaidia kuhakikisha manufaa ya punguzo la kodi yanawafikia watumiaji wa mwisho kupitia bei nafuu zaidi sokoni.
Aidha, Kamugisha amependekeza pedi za kike zitambuliwe kama bidhaa muhimu za afya sawa na dawa muhimu, jambo ambalo litawezesha bidhaa hizo kunufaika na mfumo wa kodi nafuu unaotumika kwa bidhaa za afya.
“Hatua hiyo inaweza kusaidia kupunguza bei za pedi za kike na wakati huohuo kufungua fursa ya bidhaa hizo kuingizwa katika mifumo ya kitaifa ya usambazaji wa dawa na vifaa vya afya inayosimamiwa na Serikali, hivyo kuongeza upatikanaji wake kwa wananchi,” amesema.
Ameongeza kuwa wahudumu wa afya ngazi ya jamii wanaweza kutumika kusaidia usambazaji wa bidhaa za afya ya hedhi hadi maeneo ya mwisho kabisa ambayo mara nyingi hukumbwa na changamoto za upatikanaji.
Kuhusu masuala ya udhibiti wa soko, Kamugisha amesema kuna haja ya kurahisisha gharama na taratibu za usimamizi wa bidhaa hizo kwa kuunganisha mamlaka za udhibiti chini ya mamlaka moja.
Utafiti huo pia unapendekeza kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, mashirika ya kiraia na wadau wa maendeleo ili kujenga mazingira yatakayowezesha upatikanaji wa bidhaa za hedhi kwa gharama nafuu na kwa usawa zaidi nchini.