
Mkuranga. Watu sita wamefariki dunia na wengine wanne kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha basi la Kampuni ya Mahuta na gari aina ya Toyota Coaster iliyotokea leo Jumamosi saa 11 alfajiri katika eneo la Kimanzichana, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.
Ajali hiyo ilitokea baada ya vyombo hivyo viwili kugongana uso kwa uso wakati basi la Mahuta likitoka Newala mkoani Mtwara kuelekea Dar es Salaam, huku Toyota Coaster ikitoka Dar es Salaam kuelekea Somanga.
Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi Rufiji, Protase Mutayoba amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa watu sita walifariki dunia papo hapo, huku majeruhi wanne wakipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga ambako wanaendelea kupatiwa matibabu.
Amesema miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali hiyo wakati taratibu za utambuzi zikiendelea kabla ya kutangazwa rasmi majina ya waliofariki na kujeruhiwa.
Kamanda Mutayoba amesema madereva wa vyombo vyote viwili walitoroka mara baada ya ajali hiyo na kwamba juhudi za kuwatafuta zinaendelea ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Jeshi la Polisi limewataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuendesha vyombo vya moto kwa umakini ili kuepusha ajali zinazoweza kusababisha vifo, majeraha na hasara nyingine kwa wananchi.
Uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo unaendelea.