Dar es Salaam. Serikali imeondoa hofu kwa wananchi wanaopisha utekelezaji wa mradi wa maji Manyoni mkoani Singida, ikiahidi kulipa fidia kwa mujibu wa sheria.

Hakikisho hilo limetolewa kufuatia malalamiko ya baadhi ya wananchi waliodai kunyang’anywa maeneo yao ili kupisha miradi ya maendeleo, hususan mradi wa maji unaotekelezwa wilayani Manyoni.

Akizungumza mbele ya wananchi wakati wa ziara ya Waziri Mkuu mkoani Singida Mei 30, 2026, Naibu Waziri wa Maji, Kundo Mathew amesema Serikali haitaki miradi ya maji kuwa chanzo cha migogoro kati yake na wananchi.

Kundo amesema mafanikio ya miradi ya maji yanategemea ushiriki wa wananchi katika hatua zote za utekelezaji wake, akionya kuwa kutoshirikishwa kwa wananchi kunaweza kuzalisha hofu na migogoro isiyo ya lazima.

Amesema kwa mujibu wa sera za sekta ya maji, maeneo yanayotengwa kwa ajili ya vyanzo vya maji au miundombinu ya miradi lazima yafanyiwe tathmini na wananchi wanaomiliki maeneo hayo walipwe fidia stahiki.

“Wizara ya Maji haitaki kuwa kero kwa wananchi wake. Miradi ya maji lazima iende sambamba na ushirikishwaji wa wananchi,” amesema.

Naibu Waziri huyo amesema Mradi wa Maji Manyoni unaotarajiwa kunufaisha vijiji 28 utahitaji takribani hekari 50 za ardhi kwa ajili ya miundombinu yake, akisema tathmini inafanyika kulipa fidia.

“Maeneo ya wananchi ambayo mradi wa maji unayafanya yasiweze kutumika kwa shughuli zao, Serikali inapaswa kufanya tathmini yake na kuwalipa fidia wananchi wake,” amesema.

Hata hivyo, ameeleza kuwa si kila eneo linalopitiwa na mradi litastahili fidia.

“Eneo ambalo hatulipi fidia ni pale ambapo tunapitisha bomba. Tunachokimo cha kupitisha mabomba yetu na shughuli za wananchi zinaendelea,” amesema.

Naibu Waziri huyo ameongeza kuwa Serikali itaharakisha taratibu zote zinazohitajika ili wananchi wanaostahili fidia waweze kulipwa kwa wakati na kuondoa malalamiko yaliyojitokeza.

Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha utekelezaji wa mradi unaendelea bila migogoro huku haki za wananchi zikilindwa.

Akizungumzia umuhimu wa mradi huo, Kundo amesema Wilaya ya Manyoni imekuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji kutokana na ukame unaolikumba eneo hilo kwa muda mrefu.

Amesema Mradi wa Maji Manyoni, ambao umefikia asilimia 80 ya utekelezaji wake, unatarajiwa kuwa suluhisho la kudumu kwa tatizo la maji kwa maelfu ya wananchi wa wilaya hiyo.

Kwa mujibu wa Serikali, mradi huo utakapokamilika utaongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika vijiji 28 na kupunguza adha ya wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo muhimu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *