
Lindi. Serikali imesema itaendelea kutatua changamoto zinazowakabili wachimbaji na wazalishaji wadogo wa chumvi nchini, ikiwemo kuboresha miundombinu ya barabara, kuwezesha upatikanaji wa mitaji na kupeleka huduma ya umeme katika maeneo ya uzalishaji.
Akizungumza Mei 29, 2026, wakati wa uzinduzi wa kiwanda cha kuchakata chumvi ghafi cha Rafiki Salt mkoani Lindi, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alisema wakulima wa chumvi wa mikoa ya Lindi na Mtwara sasa wamepata suluhisho la changamoto ya soko kutokana na uwepo wa kiwanda hicho chenye uwezo wa kuchakata tani 25,000 za chumvi kwa mwaka.
Alisema kiwanda hicho kitatoa ajira kwa wananchi wa maeneo husika na pia kutoa mafunzo kwa wazalishaji wa chumvi ili kuboresha ubora wa bidhaa zao na kuongeza ushindani sokoni.
“Mradi huu unalenga kuwapatia wakulima soko la uhakika, kuongeza thamani ya chumvi yao na kukuza uzalishaji wenye tija. Serikali itahakikisha changamoto zenu zinatatuliwa na pia mtapatiwa mitaji kupitia taasisi za kifedha husika ili kuendeleza shughuli zenu,” alisema Mavunde.
Kwa upande wake, Dk Venance Mwasse kutoka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) amesema ujenzi wa kiwanda hicho utagharimu Sh4 bilioni, huku hadi sasa zaidi ya Sh3 bilioni zikiwa tayari zimetumika.
Amefafanua kuwa pamoja na kuchakata chumvi, kiwanda hicho kitatoa mafunzo kwa wakulima ili kuwajengea uwezo wa kuzalisha chumvi yenye ubora wa juu na kukidhi mahitaji ya soko.
“Kiwanda hiki kikikamilika kitagharimu Sh4 bilioni na kitatoa ajira kwa wazawa pamoja na kuwapa mafunzo wazalishaji wa chumvi ili waweze kuongeza ubora wa bidhaa zao,” amesema Dk Mwasse.
Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji wa Chumvi Tanzania (TASPA), Hawa Ghasia, alisema ujio wa kiwanda hicho ni fursa kubwa kwa wazalishaji wa chumvi wa mikoa ya Lindi na Mtwara, kwani utawapatia soko la uhakika na kuongeza kipato chao.
“Tunatarajia kupata soko la uhakika na kuongeza uzalishaji wa chumvi katika mikoa ya kusini. Hii itasaidia kupunguza changamoto ya kuuza chumvi kwa bei ya chini,” amesema Ghasia.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainabu Telack, ameahidi ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na wawekezaji ili kuhakikisha changamoto ya soko la chumvi inapatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa manufaa ya wananchi.
“Nakuahidi Waziri kwamba tutashirikiana na viongozi wa kiwanda hiki kuhakikisha changamoto ya soko la chumvi inatatuliwa kwa manufaa ya wananchi wa Lindi na Mtwara,” amesema Telack.
Kwa upande wake, mkulima wa chumvi kutoka Mtwara, Said Said, amesema kukamilika kwa kiwanda hicho kutamaliza changamoto ya kutafuta soko la chumvi ghafi na kupunguza gharama za usafirishaji.
“Kiwanda hiki kimetuondolea adha ya kusafirisha chumvi hadi Mkuranga kutafuta soko. Tunaomba pia kipewe kipaumbele kununua chumvi zinazozalishwa hapa nchini kwani ni bora na zinatosheleza mahitaji,” amesema Said.