Dar es Salaam. Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba ameamuru kurejeshwa mara moja kwa zaidi ya Sh500 milioni zilizobainika kuhamishwa kutoka akaunti mbalimbali za miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, mkoani Singida.

Akizungumza katika ziara yake waliyani Manyoni Jumamosi, Mei 30, 2026, Waziri Mkuu amesema ameshtushwa na namna fedha za umma zinavyotumika bila kuzingatia taratibu huku wananchi wakihitaji huduma na kukamilisha utekelezaji miradi ya maendeleo.

Amesema uchunguzi umeonyesha zaidi ya Sh200 milioni zilichotwa kutoka akaunti za maendeleo na Sh250 milioni nyingine kutoka akaunti ya amana ya maendeleo, jambo ambalo limeibua maswali kuhusu matumizi yake.

Pia, ameeleza kutoridhishwa na baadhi ya matumizi ya fedha katika miradi mbalimbali, ukiwemo wa ujenzi wa jengo la utawala la halmashauri kwa zaidi ya Sh1 bilioni, ukamilishaji wa nyumba ya mkurugenzi kwa Sh100 milioni na nyumba za wakuu wa idara kwa Sh70 milioni.

“Wakati hatua stahiki za kiutumishi zikiendelea, kamata hawa wasitoke mpaka hii Sh500 milioni ya Serikali irudi.

 “Mtashughulikia mambo ya kiutumishi, lakini fedha za wananchi lazima zirudi,” amesema.

Amesema si mara ya kwanza kukutana na vitendo vya aina hiyo, akisema katika mkoa mwingine alibaini vifaa vya ujenzi vilivyonunuliwa na kuachwa bila kutumika huku watendaji wakiendelea kuomba fedha za kununua vingine.

“Nilifika pia mkoa mmoja nikakuta wamekwenda kununua bati za ajabu ajabu, wakaziacha huko halafu wakaomba nyingine. Nikasema kamata, taratibu za utumishi zitafuata,” amesema.

Hata hivyo, amesema lengo lake si kuwa kiongozi katili bali kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa manufaa yaliyokusudiwa.

“Mimi si kiongozi katili, lakini wasiposoma alama za nyakati watakutana na fyekeo,” ameonya.

Asisitiza haki

Mbali na vita dhidi ya ubadhirifu, Waziri Mkuu amesema hatawaacha wananchi waonewe badala yake atatumia nafasi yake kusimamia haki kwa wote.

Amesema amechagua kutoka nje ya ofisi na kwenda moja kwa moja kwa wananchi kusikiliza changamoto zao na kupata picha halisi ya maisha wanayoishi.

“Mimi sitaki mtu mnyonge aonewe. Najua maana na thamani ya haki. Ndiyo maana badala ya kukaa ofisini, natoka nje kuwasikiliza Watanzania, najua watu wana mambo yanayowasumbua,” amesema.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa haki haiwezi kutenganishwa na uwajibikaji, akisema kila mtendaji lazima atekeleze wajibu wake kwa mujibu wa sheria na taratibu.

Amesema anaifahamu kiu ya Watanzania ya maendeleo kwa sababu ameyaishi maisha yao na si kwa kusoma taarifa pekee.

Aidha, ametaja uzoefu wake serikalini na ushiriki wake katika maandalizi ya ilani za uchaguzi na Dira ya Taifa kuwa nyenzo zinazomsaidia kuelewa vipaumbele vya maendeleo vya Serikali.

“Nimeshiriki kuandaa ilani tatu za uchaguzi, ikiwemo hii iliyopita. Nimeshiriki pia kuandaa dira, hivyo nayajua yale ambayo Rais Samia Suluhu Hassan amewaahidi Watanzania. Kwa maana hiyo sitawaangusha,” amesema.

Kukatika umeme

Waziri Mkuu ametolea pia maelezo changamoto ya kukatikatika kwa umeme inayoshuhudiwa katika baadhi ya maeneo nchini, akisema haisababishwi na upungufu wa uzalishaji wa umeme bali uwezo wa Gridi ya Taifa kuhimili mahitaji yanayoongezeka.

Amesema wakati gridi ilipoanzishwa, huduma ya umeme ilikuwa inafika katika makao makuu ya mikoa na wilaya pekee, lakini sasa imeenea hadi vijiji vyote na katika baadhi ya maeneo hadi vitongojini.

Amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika uimarishaji wa gridi ili kuondoa changamoto hiyo ambayo imekuwa ikiathiri wananchi na shughuli za uzalishaji.

“Tunatambua kuwa kukatikatika kwa umeme kuna madhara mengi. Vifaa vinaharibika na wakati mwingine husababisha hitilafu. Serikali inaendelea kuimarisha gridi ili kulimaliza tatizo hili,” amesema.

Amengeza kuwa Serikali imeelekeza nguvu katika kukamilisha miradi ya nishati na miundombinu mingine ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma.

Akemea wapenda vyeo

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka madiwani na watendaji wa halmashauri kuacha siasa za makundi na mbio za madaraka ambazo zimekuwa zikikwamisha maendeleo ya wananchi.

Amesema katika ziara zake amekutana na migogoro mingi ya ardhi na mashamba ambayo imeachwa kwa muda mrefu bila ufumbuzi kutokana na viongozi na watendaji kujikita katika masuala ya vyeo.

“Kila halmashauri nimekuta migogoro mingi ya ardhi. Hata migogoro ya mashamba hatuitatui kwa sababu watu wamejikita kwenye vyeo,” amesema.

Amesema katika baadhi ya maeneo hata wataalamu wa Serikali wamekuwa sehemu ya makundi yanayolinda masilahi binafsi badala ya kutumikia wananchi.

“Katika maeneo mengine wataalamu wetu wanaingia, wanapanga dili na ushabiki, wakiamini kwamba akiingia huyu basi dili zao hazitakwenda,” amesema.

Amewaonya watendaji wanaoshindwa kutatua changamoto za wananchi huku wakitumia muda mwingi kwenye siasa za ndani na kugombea nafasi za uongozi.

“Unakwenda kwenye mkutano unapunguza muda ili Serikali isipate mzigo, wakati unajua Watanzania wana shida. Wengine wameaminiwa wanapata fedha wanagawana,” amesema.

Amesisitiza kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua watendaji wote watakaobainika kushindwa kutekeleza wajibu wao au kutumia vibaya fedha za umma.

Apewa ng’ombe

Katika ziarahiyo pia, Dk Mwigulu amekabidhiwa zawadi ya ng’ombe.

Akitangaza zawadi hiyo, Mbunge wa Jimbo la Manyoni, Dk Pius Chaya amesema zawadi hiyo ni alama ya kutambua utendaji wake katika kushughulikia maendeleo ya wananchi.

Akitaja sababu ya kumpa zawadi ya ng’ombe, mbunge huyo amesema kuwa katika hotuba zake mbalimbali, Waziri Mkuu huyo amekuwa akisema aliishi katika maisha ya kifugaji na kuchunga ng’ombe, hivyo zawadi hiyo ni muhimu kwake.

“Mimi na madiwani wa Manyoni tukasema kaka yetu anakuja nyumbani, tumekuandalia ng’ombe jike, lengo letu umpeleke akazae ili ng’ombe wawe wengi,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *