Moshi. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimewataka wananchi wa Moshi kulinda miundombinu ya mradi wa Stendi ya Kimataifa ya Ngangamfumuni, kisisitiza kuwa ni mali ya umma iliyogharimu fedha nyingi hivyo inapaswa kutunzwa ili idumu na kuwanufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.

Kimesema miradi ya maendeleo ni nguzo muhimu ya ustawi wa wananchi na hivyo inahitaji ulinzi na ushirikiano wa kila mwananchi katika kuilinda dhidi ya uharibifu.

Hayo yamesemwa leo Jumamosi Mei 30,2026 na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kenani Kihongosi, akizungumza baada ya ukaguzi wa stendi hiyo ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake ya ukaguzi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na uhai wa chama hicho, mkoani Kilimanjaro.

Amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati katika Mkoa wa Kilimanjaro, ambao umeanza kutekelezwa mwaka 2019 na Serikali imeendelea kuupatia fedha ili kuhakikisha unakamilika.

Amesema Serikali tayari imetoa zaidi ya Sh12 bilioni katika awamu mbili za utekelezaji wa mradi huo na kuwa mradi huo utaleta mageuzi makubwa ya kiuchumi kwa wananchi wa Moshi, ikiwemo kuongeza ajira, biashara na mapato ya Halmashauri ya Manispaa ya Moshi.

“Mradi huu ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati katika Mkoa wa Kilimanjaro ambao kutokana na changamoto mbalimbali za kifedha ulisimama kwa kipindi fulani. Sasa jukumu letu sote ni kuhakiisha tunailinda miundombinu hii.

Amesema mradi huo utaendelea kukuza uchumi wa Mkoa huo kutokana na mazingira kuendelea kuboreshwa.

“Miradi yote ya maendeleo ni mali ya wananchi na ni wajibu wetu kuitunza ili iweze kudumu na kuwanufaisha vizazi vya sasa na vijavyo,” amesema

Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Mwajuma Nasombe, amesema mradi huo umefikia asilimia 70 ya ujenzi wake ambapo ukikamilika utaweza kuwa na maegesho ya mabasi 100 pamoja na magari mengine madogo kwa wakati mmoja ukiwa umejumuisha maduka ya biashara,migahawa, na huduma nyingine muhimu kwa wasafiri na wafanyabiashara.

Amesema, ujenzi ulianza rasmi Januari 28, 2018 na ulitakiwa kukamilika Januari 28, 2021 lakini uliongezewa muda hadi Mei 14, 2022 kutokana na changamoto za kifedha, kabla ya kusimama rasmi Mei 12, 2022 baada ya fedha za utekelezaji kukosekana.

Amesema baada ya kusimama kwa miaka mitatu, Serikali ilifanya mazungumzo na mkandarasi na hatimaye kurejea kwa kazi, ambapo mkataba mpya ulisainiwa Juni 20, 2025 na mradi kukadiriwa kukamilika Aprili 26, 2026 kabla ya kuongezewa muda hadi Oktoba 27, 2026 kutokana na changamoto za mfumo wa malipo.

Amesema katika awamu ya kwanza ya utekelezaji, Halmashauri ilipokea Sh8.73 bilioni ambazo zilitumika kwa ujenzi wa boma la jengo la abiria hadi ghorofa ya kwanza, hatua iliyofikisha mradi kwenye asilimia 51 kabla ya kusimama na kuwa hadi kukamilika kwake utagharimu Sh28.5 bilioni.

Amesema awamu ya pili, hadi sasa zaidi ya Sh4 bilioni zimepokelewa na kutumika huku mkandarasi akiendelea na kazi mbalimbali zikiwemo kupaua jengo, kupiga lipu, uwekaji wa mfumo wa maji na umeme, pamoja na maandalizi ya maeneo ya kupakia na kushusha abiria na sasa kazi inayoendelea imejumuisha pia ujenzi wa jengo la kupokelea umeme na kuhifadhia majenereta pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya mitaro na maeneo ya stendi.

Mmoja wa wananchi wa Manispaa ya Moshi, Julitha Tarimo amesema kukamilika kwa stendi hiyo kutasaidia kuongeza vichocheo vya maendeleo ya kiuchumi kutokana na mchango wake katika kuongeza mzunguko wa biashara na huduma.

“Tunatarajia kukamilika kwa mradi huo kutafungua fursa za ajira kwa wananchi wengi kupitia shughuli mbalimbali zitakazofanyika ndani na nje ya kituo hicho.Tunaamini sisi stendi itaibua na kukuza biashara ndogondogo, jambo litakaloongeza kipato kwetu.”

Naye Julius Materu amesema mradi huo utaimarisha mfumo wa usafiri kwa kupunguza msongamano na kuongeza ufanisi wa huduma za mabasi na sekta ya usafirishaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *