Maswa. Wananchi wa vijiji vya Mwabayanda na Mwasita wilayani Maswa mkoani Simiyu, wanatarajia kunufaika na huduma ya maji safi na salama kupitia mradi wa maji wenye thamani ya Sh2.1 bilioni uliosainiwa kati ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini Maswa (Mauwasa) na mkandarasi Kampuni ya Zongii Contractors Ltd ya jijini Mwanza.
Mradi huo unalenga kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji iliyokuwa ikiwasumbua wananchi wa maeneo hayo kwa muda mrefu, hususan wanawake na watoto waliokuwa wakitembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo muhimu.
Akizungumza Mei 30,2026 katika kijiji cha Mwasita wakati wa kusainiwa kwa mkataba huo, Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano amemtaka mkandarasi kuhakikisha anatumia vifaa imara na vyenye viwango ili mradi huo uweze kudumu kwa muda mrefu na kutoa huduma kama serikali ilivyokusudia.
Amesema serikali haitavumilia vitendo vya wizi au ubadhirifu katika utekelezaji wa mradi huo na kuonya kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayehusika kuhujumu utekelezaji wake.
“Tunataka mradi huu uwe wa mfano kwa sababu wananchi wamekuwa wakisubiri huduma hii kwa muda mrefu. Hakikisheni mnatumia vifaa bora na kazi ifanyike kwa uaminifu mkubwa,” amesema.
Sehemu ya wananchi wakishuhudia utiaji saini wa mkataba kati ya MAUWASA na Kampuni ya Zongii katika kijiji cha Mwasita, wilayani Maswa, kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji wa Mwabayanda–Mwasita. Picha na Samwel Mwanga.
Amesema kuwa atahakikisha kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya watasimamia utekelezaji wa mradi huo hatua kwa hatua, ili kuhakikisha fedha zilizotengwa zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa, Poas Kilangi amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo ni sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma ya maji safi na salama maeneo ya vijijini na mijini.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kwa kipindi cha mwaka mmoja kutanufaisha zaidi ya wananchi 12,000 na utasaidia kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji katika wilaya hiyo na kuboresha maisha ya wananchi kwa ujumla.
“Mradi huu utahusisha ujenzi wa tenki la kuhifadhi na kusambaza maji kwenye mnara wenye urefu wa mita 12, lenye uwezo wa kuhifadhi lita 200,000 za maji,ulazaji wa wa bomba kwa umbali wa kilomita 12 pamoja na mabirika ya kunyweshea maji mifugo,” amesema.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Kampuni ya Zongii Contractors Ltd, Elpidius Kasiga amesema kuwa watakamilisha mradi huo mapema kwa kipindi cha miezi sita licha ya mkataba kuwataka kumaliza kwa kipindi cha mwaka mmoja ili wananchi waweze kupata huduma ya maji.
“Tunahitaji ushirikiano kwa wananchi kwa ajili ya kulinda vifaa na miundo mbinu ya maji tutakayojenga na ninaahidi kutoa kipaumbele cha ajira kwa vijana na wanawake wa vijiji vya Mwabayanda na Mwasita wakati wa utekelezaji wa mradi huu,” amesema.
Mkazi wa kijiji cha Mwasita Agnes John amesema kwa muda mrefu wananchi walikuwa wakitegemea maji ya kwenye mito na visima vya asili ambavyo si salama kwa matumizi ya binadamu.
“Tumekuwa tukipata shida sana hasa kipindi cha kiangazi. Wanawake tulikuwa tunaamka usiku kwenda kutafuta maji mbali, lakini sasa tuna matumaini makubwa,” amesema.
Kwa upande wake, Esther Pius wa kijiji cha Mwasita amesema ujio wa mradi huo utaongeza maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa vijiji hivyo.
“Ukipata maji karibu hata shughuli za kilimo na biashara zinaenda vizuri. Huu mradi utatusaidia sana wananchi wa kawaida,” amesema.
Naye Neema Masule mkazi wa kijiji cha Mwabayanda amesema watoto wengi walikuwa wakichelewa kwenda shule kutokana na kutumia muda mwingi kutafuta maji.
“Watoto wetu walikuwa wanateseka sana. Tunaamini sasa hali itabadilika na afya za wananchi zitakuwa bora zaidi,” amesema.