Dodoma. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amemwelekeza Waziri wa Tamisemi, kufanyia marekebisho sheria inayosimamia uchaguzi wa naibu meya na makamu wenyeviti wa halmashauri za wilaya na manispaa.

Dk Mwigulu amesema utaratibu wa kufanya uchaguzi wa viongozi hao kila mwaka umekuwa ukikwamisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa kuwa viongozi wengi hutumia muda mwingi kujiandaa kwa uchaguzi badala ya kuwahudumia wananchi.

Ametoa kauli hiyo leo Jumamosi, Mei 30, 2026, wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara wilayani Manyoni, mkoani Singida, baada ya kuzindua mradi wa maji wa miji 28 wenye thamani ya Sh28 bilioni.

Amesema mbali na changamoto ya uchaguzi wa kila mwaka, kumekuwepo na tabia ya baadhi ya viongozi na watendaji kutumia muda mwingi kufikiria nafasi za uongozi badala ya kutekeleza majukumu waliyopewa.

“Watu wana shida nyingi, lakini baadhi ya wenye dhamana wanawaza vyeo muda wote.

“Wanaunda makundi na kuendeleza ushabiki wa kisiasa kwa ajili ya uchaguzi unaofuata badala ya kutatua matatizo ya wananchi. Nimeagiza Waziri wa Tamisemi afanyie marekebisho sheria ya uchaguzi wa naibu meya na makamu wenyeviti wa halmashauri,” amesema Dk Mwigulu.

Amesema uchaguzi wa kila mwaka hauwapi viongozi hao nafasi ya kutosha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, hali hiyo pia imekuwa ikichochea makundi yenye masilahi binafsi ambayo huamini kuwa viongozi wanaowaunga mkono watakapochaguliwa wataendeleza maslahi yao.

Katika hatua nyingine, Dk Mwigulu amesema ataendelea kusimamia haki za wananchi na kupambana na vitendo vya ubadhirifu, rushwa na unyonyaji bila kuyumba mbele ya upinzani kutoka kwa watu wanaonufaika na mifumo isiyo sahihi.

Akitumia mfano wa simulizi la Mfalme Daudi na Goliati katika Biblia, amesema hatasita kukabiliana na makundi yoyote yanayojihusisha na vitendo vinavyowakandamiza wananchi.

“Walaghai, wezi na wanyang’anyi nitawashikisha adabu. Mimi sina nafasi ya kulea uzembe wala kuonea wananchi. Nayajua mahitaji ya Watanzania na changamoto wanazopitia kwa sababu nami nimepitia maisha hayo,” amesema.

Amesisitiza kuwa uzoefu wake serikalini umempa uelewa wa kina kuhusu changamoto zinazowakabili wananchi wa kawaida, hivyo ni wajibu wa kila mtendaji wa umma kuwajibika kikamilifu katika eneo lake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *