Mbeya. Watu watatu wamefariki dunia na wengine wanne kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha magari mawili katika Kijiji cha Mambi, Kata ya Kongolo, Tarafa ya Ilongo wilayani Mbarali mkoani Mbeya.
Ajali hiyo imetokea asubuhi ya leo Mei 30 katika barabara kuu ya Mbeya-Njombe ikihusisha lori iliyobeba mafuta kutoka Dar es Salaam kwenda mkoani Songwe na kuligonga basi Kampuni ya ABC Upper Class.
Hivi karibuni Mei 8 mwaka huu, watu watano walifariki dunia na wengine 28 kujeruhiwa baada ya basi la Kampuni ya Shabiby aina ya Youtong likiendeshwa na Michael Mbugi likitokea Dodoma kwenda Mbeya lilipata ajali katika eneo la Tanangozi, Kata ya Mseke mkoani Iringa, baada ya kugongana na lori la vinywaji aina ya FAU.
Picha ikionesha ajali iliyohusisha magari mawili basi ya kampuni ya ABC Upper Class na lori iliyotokea wilayani Mbarali mkoani Mbeya.
Katika ajali hiyo, derava wa basi na kondakta wake, pamoja na dereva wa roli walifariki dunia.
Akithibitisha ajali hiyo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishina Msaidizi Polisi (ACP), Wilbert Siwa amesema gari aina ya Volvop Kampuni ya Syenergy ikitokea Dar es Salaam kwenda Songwe lilihama upande wake na kuligonga gari kampuni ya ABC.
Amesema gari hilo likiendeshwa na dereva Mohamed Seif mkazi wa Dar es Salaam, aliendesha kwa uzembe na kuhama upande wake wa kushoto na kwenda kulia na kuligonga basi la kampuni ya ABC iliyokuwa ikitokea Mbeya kwenda Dar es Salaam.
Picha zikionesha ajali iliyohusisha magari mawili basi ya kampuni ya ABC Upper Class na lori iliyotokea wilayani Mbarali mkoani Mbeya.
“Waliofariki katika ajali hiyo ni Ased Asad ‘Tembo’ ambaye ni dereva wa basi, kondakta wa basi Letisia Bujabi na Mohamed Seif ‘Maurid’ ambaye ni dereva wa lori hilo, huku majeruhi akiwa ni Mariam Abdul,” amesema.
“Kati ya majeruhi hao wanne, watatu wametibiwa na kuruhusiwa kuondoka huku mmoja (Mariam) akiendelea na matibabu katika Hospitali ya Inyala na magari yote mawili yameharibika,” amesema Kamanda huyo.
Kamanda Siwa ameongeza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori kutokuwa makini barabarani na kuyapita magari mengine huku akitoa wito kwa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali.
Mmoja wa abiria aliyekuwa katika basi hilo, Charles Isack amesema hawakuwa katika mwendo wa haraka na huenda dereva wao hakujua kama kuna gari nyingine mbele yake hadi kuwagonga.
“Tulikuwa katika mwendo wa kawaida ukizingatia bado ilikuwa asubuhi nafikiri dereva wetu pia hakujua kwamba kuna lori mbele ili aweze kulikwepa, tunashukuru kwa ambao tumebaki salama,” amesema Isack.