
Moshi. Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi, Kilimanjaro imeondokana na utegemezi wa oksijeni baada ya kuanza kutumia mtambo wa kuzalisha hewa tiba ya oksijeni, na kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa wagonjwa.
Hatua hiyo imetajwa kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za uendeshaji na kuiwezesha kuokoa Sh126 milioni katika kipindi cha miezi sita.
Mradi huo wa kimkakati ulianza rasmi Novemba 25, 2024 kwa maandalizi ya eneo la usimikaji wa mtambo na ujenzi wa jengo, huku usimikaji wake ukikamilika Septemba 29, 2025.
Hayo yameelezwa leo Mei 30, 2026 na Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Abdilahi Issa, wakati wa ziara ya Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Kenani Kihongosi katika hospitali hiyo.
Dk Issa amesema hospitali ilikabidhiwa rasmi mtambo huo Novemba 17, 2025 na kuanza uzalishaji wa oksijeni Desemba 1, 2025, hali iliyoondoa utegemezi wa muda mrefu wa kununua mitungi ya oksijeni kutoka Dar es Salaam, Arusha na maeneo mengine.
Amesema hadi Mei 28, 2026, mtambo huo ulikuwa umezalisha mitungi 3,313 ya hewa tiba ya oksijeni, ikiwemo mikubwa 2,875 na midogo 438, kiasi kilichowezesha hospitali kujitosheleza kwa huduma hiyo na hata kuuza mitungi 186 kwa taasisi nyingine za afya.
“Kabla ya mtambo huu tulikuwa tunanunua oksijeni kutoka kwa wazabuni wa nje, jambo lililosababisha gharama kubwa za manunuzi, usafirishaji na uhifadhi wa mitungi. Sasa tunazalisha oksijeni yetu wenyewe na kuisambaza moja kwa moja kwenye vitengo vya hospitali,” amesema.
Kwa mujibu wa Dk Issa, hospitali ilikuwa ikitumia wastani wa Sh3.5 milioni kwa wiki kwa ajili ya ununuzi wa oksijeni, huku bajeti ya kati ya Sh100 milioni na Sh200 milioni kwa mwaka ikitengwa kwa matumizi hayo.
Amesema mtambo huo wenye thamani ya Dola za Marekani 843,217.04 sawa na Sh1.94 bilioni umeimarisha huduma katika vitengo vya Dharura (EMD), Wagonjwa Mahututi (ICU), Uchujaji Damu (Dialysis) pamoja na Afya ya Mama na Mtoto.
Awali, Kihongosi amesema Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mawenzi ni miongoni mwa taasisi kongwe za afya nchini, iliyoanza kutoa huduma mwaka 1920 kama zahanati ya askari wa kikoloni wa Kijerumani kabla ya kupandishwa hadhi kuwa kituo cha afya mwaka 1922, hospitali ya mkoa mwaka 1956 na hospitali ya rufaa mwaka 2010.
Kihongosi amesema amefurahishwa na maendeleo ya hospitali hiyo hususan utekelezaji wa mradi wa mtambo wa kuzalisha hewa tiba ya oksijeni uliowezeshwa na Serikali kwa lengo la kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Kihongosi, kabla ya uwekezaji huo hospitali ilikuwa ikikabiliwa na gharama kubwa za kununua na kusafirisha oksijeni kutoka Dar es Salaam, Arusha na maeneo mengine, jambo lililoathiri ufanisi wa utoaji wa huduma na kuwa mtambo huo umeongeza upatikanaji wa uhakika wa hewa tiba ya oksijeni, kuokoa maisha ya wagonjwa na kupunguza gharama za uendeshaji wa hospitali.