Njombe. Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka amesema viongozi wa dini wana wajibu wa kuihubiria jamii katika kutenda mema ili waweze kuwa na mwisho mzuri watakapoondoka duniani.

Katika hafla ya chakula iliyoandaliwa nyumbani kwake, yenye lengo la kuwapongeza viongozi wa Kanisa la Waadventist Wasabato Tanzania, ambao waliweka kambi ya mwezi mmoja kuhubiri neno la Mungu na kutoa huduma za kitabibu kwa wananchi mkoani humo.

Akizungumza wakati wa kuwakaribisha viongozi hao Nyanda za juu kusini na kaskazini waliofika katika hafla pamoja na waumini wao leo Mei 30, 2026, Mtaka amesema tukio la kambi ya maombezi ni kubwa na limekuwa likifuatiliwa na watu wengi kupitia vyombo mbalimbali vya habari vya ndani na nje ya nchi kwa lugha tofauti.

Amesema kupitia mkutano huo wa injili watu wamepata mafundisho mengi na shuhuda mbalimbali kutoka maeneo tofauti nchini, ikionyesha dhahiri kuwa mkutano huo umekuwa na tija kubwa kwa wananchi hasa mkoani Njombe.

Kwaya ya Wadventisti Wasabato Kurasini ikitumbuiza kwenye hafla iliyofanyika mkoani Njombe

Amesema hafla hiyo imefanyika ili kuwashukuru viongozi hao kwa kutoa huduma ya maombezi pamoja na ile ya matibabu bure kwa wananchi wa mkoa huo.

Amesema kufuatia hafla hiyo wakaona waalike kwaya za Wasabato za Kurasini, Magomeni na Galilaya ya Kigamboni ili kushiriki kufunga kambi ya maombezi.

“Lengo la kukutana hapa ni kushukuru zimekuwa siku 20 zenye baraka kubwa na tunahitimisha lakini sisi familia ya Njombe tumepata nafasi ya kuonana, tunasema tunashukuru,” amesema Mtaka

Askofu Kanisa la Wadventista Wasabato Tanzania Jimbo la Kusini, Joseph Mgwabi amesema kukutana kwenye hafla hiyo katika kilele cha mikutano mikubwa ya injili kumewafanya waondoke wakiwa wanafahamiana kupitia tukio hilo.

Mwenyekiti wa Kanisa la Wadventisti Wasabato Jimbo la Kaskazini, Mchungaji David Mpwani, amesema Mtaka ana mchango mkubwa katika kufanikisha mkutano huo wa injili kutokana na maamuzi yake ya kutaka mkutano kufanyika mkoani hapa.

“Katika kufanikisha ujio wetu hapa kuna mengi umeyafanikisha ambayo si vema kuyasema yote hapa, lakini hata kwa kitendo hiki cha kutualika hapa, kuandaa tukio kama hili ni tendo la ukarimu ambalo haliwezi kuelezeka katika lugha za kibinadamu,” amesema Mpwani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *