
Utafiti wa Benki ya Hifadhi ya Shirikisho ya New York unaonyesha kwamba karibu 10% ya kaya zinaripoti kutokula chakula kutokana na kupanda kwa gharama na matatizo ya kifedha.
Wamarekani wengi wanasumbuliwa na njaa sasa kuliko wakati wa kilele cha janga la COVID-19. Haya ni kwa mujibu wa utafiti mpya wa Benki ya Hifadhi ya Shirikisho ya New York, ambao unaashiria ongezeko kubwa la ukosefu wa usalama wa chakula unaosababishwa na shinikizo la gharama za maisha linaloongezeka.
Utafiti huo, uliochapishwa katika Liberty Street Economics na kwa mujibu wa Utafiti wa Matarajio ya Watumiaji wa benki hiyo, umebaini kuwa karibu 10% ya kaya ziliripoti kukosa milo kutokana na ukosefu wa chakula katika utafiti wa hivi karibuni wa Februari, ikiwa ni zaidi ya mara mbili ya 4% iliyorekodiwa mwaka wa 2020.
Ripoti hiyo inategemea mawimbi mengi ya utafiti kuanzia 2020 hadi Oktoba 2025 ili kutathmini mwenendo wa mashinikizo ya kifedha ya kaya na uhaba wa chakula na inaonyesha kwamba shinikizo limeongezeka katika miaka ya karibuni licha ya mwisho rasmi wa kipindi cha janga la Corona.
Kwa mujibu wa uchambuzi, karibu 16% ya waliohojiwa huko Marekani wamesema wamekuwa wakitegemea michango ya chakula, huku karibu 20% za kaya zinazopata chini ya $50,000, wakiripoti kuruka milo au kukosa chakula.
Benki ya Hifadhi ya Shirikisho ya New York imesema, hili ni “ongezeko kubwa la ukosefu wa usalama wa chakula,” hasa miongoni mwa kaya zenye kipato cha chini na zisizo na elimu ya kutosha, pamoja na familia zenye watoto wadogo.
Vilevile, uchambuzi uliofanywa na NPR umegundua kuwa viwango vya ukosefu wa usalama wa chakula mwaka 2025 vilikuwa vya juu kuliko kipindi cha kiangazi cha 2020, jambo linaloonesha zaidi kina cha mashinikizo ya kifedha yanaoendelea kwa familia nyingi za Marekani.
Ripoti hiyo inakuja huku kukiwa na shinikizo la mfumuko wa bei na gharama za juu za maisha, ikiwa ni pamoja na kupanda bei za mafuta. Kipindi cha utafiti huo kimetangulia ongezeko kubwa la bei za gesi mwishoni mwa Februari na Machi kutokana na vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran na kusimamishwa usafirishaji wa baharini katika Mlango-Bahari wa Hormuz, ambao umezidisha msongo wa mashinikizo katika kaya nyingi za Marekani.
Waendeshaji wa benki za chakula kote nchini Marekani wanasema wanashuhudia ongezeko la mahitaji huku kaya zikipambana kukabiliana na gharama kubwa za usafiri na maisha.