
Bunge la Iran linatarajiwa kupitia na kuidhinisha sheria inayorasimisha usimamizi na mamlaka ya Jamhuri ya Kiislamu juu ya Mlango-Bahari wa Hormuz.
Alireza Salimi, mjumbe wa Bodi ya Uongozi ya Bunge, amesema kwamba chombo hicho cha kutunga sheria “hivi karibuni” kitapasisha sheria ya usimamizi wa Iran katika Mlango-Bahari wa Hormuz.
Ameongeza kuwa maelezo yote yanayohusiana na mpango huo yataidhinishwa na kukamilishwa na Bunge.
Salimi amesisitiza kuwa Mlango-Bahari wa Hormuz uko katika maji ya eneo la pamoja la Iran na Oman, na kwa hivyo hakuna nchi nyingine itakayoruhusiwa kufanya maamuzi kuhusu njia hiyo ya majini.
“Hatutaruhusu Rais wa Marekani Donald Trump na wengine kuamua suala la Mlango-Bahari wa Hormuz; suala hili linatuhusu sisi,” amesema Salimi.
Mbunge huyo amesisitiza kwamba maamuzi kuhusu usimamiaji wa Mlango-Bahari wa Hormuz “sio ya kimkakati au ya muda mfupi” bali ni “ya uhakika na ya kudumu.”
Iran ilifunga Mlango-Bahari wa Hormuz kwa Marekani, Israel na washirika wao kufuatia uchokozi wao usio na sababu dhidi ya nchi hiyo.
Siku ya Ijumaa iliyopita pia Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi na mwenzake wa Oman, Badr bin Hamad Al Busaidi walijadili kadhia ya Mlango-Bahari wa Hormuz na usimamizi wake wa kisheria wa siku zijazo katika mazungumzo ya simu.
Mapema mwezi huu pia Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama wa Kitaifa na Sera za Kigeni ya Bunge la Iran, Ebrahim Azizi, alisema kwamba Tehran imebuni utaratibu mpya wa kudhibiti trafiki ya baharini kupitia “njia iliyoteuliwa” katika Mlango-Bahari wa Hormuz, ambayo inajumuisha kutoza ada za “huduma maalumu.”
Aliongeza kuwa mfumo mpya unaendana na mamlaka ya kitaifa ya Iran na utahakikisha usalama wa biashara ya kimataifa.