Waziri anayejiita wa usalama wa Israel, Itamar Ben-Gvir, amemtaka Waziri Mkuu wa utawaka huo katili, Benjamin Netanyahu, kusawazisha na ardhi vitongoji vya mji mkuu wa Lebanon, Beirut huku utawala huo ukizidisha mashambulizi yake dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu.

Katika video iliyochapishwa kwenye Instagram, Ben-Gvir alisema anapinga kusitisha mapigano na Lebanon na anahimiza mashambulizi makali zaidi kwenye vitongoji vya kusini mwa Beirut.

Akimhutubu Netanyahu moja kwa moja, Ben-Gvir amesema: “Waziri Mkuu mpendwa Benjamin Netanyahu, ninakupenda na ninakuthamini, lakini sasa ni wakati wa kusawazisha vitongoji vya Beiruti na ardhi.”

“Tunamshukuru [Rais wa Marekani Donald] Trump, na lazima tuseme asante kwa ushirikiano,” ameongeza waziri huyo mwenye msimamo mkali.

Katika hotuba iliyorushwa kwenye televisheni siku ya Jumamosi, Waziri Mkuu wa Lebanon, Nawaf Salam alisema Israel “inafuata sera ya kuteketeza ardhi” kwa “kuharibu miji na vijiji, na kuwalazimisha wakazi wake kwenda uhamishoni.”

Mapema wiki hii, jeshi la Israel lilizidisha mashambulizi dhidi ya Lebanon, huku Netanyahu akisema ameamuru jeshi la utawala huo vamizi kuzidisha mashambulizi ikiwa ni katika jitihada za kuvuruga makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo tayari yalikuwa dhaifu.

Kwa upande mwingine, harakati ya Muqawama ya Lebanon, Hizbullah imejibu mapigo kwa kufanya mashambulizi kadhaa kwenye maeneo ya kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu “kujibu ukiukwaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano”.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *