
Jumuiya ya Wachapishaji Habari Duniani imetangaza kwamba tuzo ya Kalamu ya Dhahabu ya Uhuru 2026 itatolewa kwa wapiga picha na wakurugenzi wa video kutoka Ukanda wa Gaza ulioharibiwa na vita.
Tuzo hiyo ya kifahari ya kimataifa hutolewa kwa ajili ya kuwaenzi wale waliorekodi mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na Israel, wakihatarisha maisha yao ili kuwaonyesha walimwengu ukweli wa mambo, wakati Israel inawazuia waandishi wa habari wa kigeni kuingia eneo la Ukanda wa Gaza.
Hafla ya tuzo hiyo ilifanyika katika mji wa pwani wa Marseille kusini mwa Ufaransa mnamo Juni 1, sanjari na Kongamano la 77 la Vyombo vya Habari vya Dunia.
Waandishi wa habari wa Palestina wanawakilisha wenzao jasiri katika uwanja huo, huku wapiga picha Mohammed Salem, Fatima Shbair na Mohammed al-Baba wakichaguliwa kupokea tuzo hiyo kwa niaba ya waandishi wenzao wa habari.
Baba, ambaye alitumia miezi saba kurekodi ukatili wa Israel huko Gaza kabla ya kuondoka katika eneo hilo, amesisitiza kwamba tuzo hii ina thamani kubwa ya kibinadamu na kitaaluma.
Tuzo hii inatolewa wakati ambapo Jumuiya ya Wachapishaji Habari Duniani imewataja waandishi wa habari wa Gaza kuwa “waathiriwa wa mzozo huo kama ambavyo ni maripota wa vita vya kandokando yao.”
Ripoti ya Shirika la Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka inaangazia athari kubwa kwa jamii ya waandishi wa habari wa Palestina, huku zaidi ya waandishi habari 260 wakiwa wameuawa kwa kupigwa risasi au kulipuliwa na jeshi la Israel tangu kuanza vita vya mauaji ya kimbari ya utawala huo dhidi ya watu wa Gaza, Oktoba 2023.