
KOCHA Mkuu wa Hausung FC ya Njombe, Selemani Kitunda Simota ‘Guardiola’ amesema sababu ya timu hiyo kufanya vibaya hadi sasa katika Ligi ya Championship ni kutokana na kukosa wachezaji wazoefu, jambo linalochangia kurudisha maendeleo yao.
Akizungumza na Mwanaspoti, Guardiola amesema wachezaji wengi waliopo katika kikosi hicho ni vijana na hawana uzoefu sana wa kupambana na timu nyingine, jambo ambalo ni changamoto inayosababisha kutokuwa na mwenendo mzuri tangu msimu umeanza.
“Wachezaji wengi ni waliopandisha timu daraja sasa kwa hali ya namna hiyo ni ngumu kushindana na wapinzani wengine ambao walifanya maboresho mazuri dirisha la usajili, kubaki kwetu Championship ni suala la miujiza,” amesema Guardiola.
Kitunda anayefananishwa na Kocha wa Manchester City ya England, Pep Guardiola katika karia yake ya soka amezichezea timu mbalimbali za Kikwajuni FC, Polisi Pemba na Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo ‘KMKM FC’ zote za visiwani, Zanzibar.
Licha ya kucheza Kikwajuni FC, Polisi Pemba na KMKM FC, ila, Kitunda amewahi pia kuzifundisha timu mbalimbali, zikiwemo, Tunduru Korosho, Stand United ‘Chama la Wana’, Cosmopolitan na mabingwa wa Ligi Kuu mwaka 1982, kikosi cha Pan Africans.
Hausung imepanda daraja msimu huu na kushiriki Ligi ya Championship baada ya kuongoza kundi A na pointi 25, ikiungana na mabingwa wa Ligi Daraja la Kwanza msimu wa 2024-2025, Gunners FC ya Dodoma, iliyoongoza pia kutoka kundi B na pointi 35.
Timu hiyo inayotumia Uwanja wa Amani uliopo Mkoa wa Njombe, katika mechi 27, ilizocheza imeshinda tatu tu, sare tatu na kupoteza 21, ikiwa mkiani mwa nafasi ya 16 na pointi tisa, huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 16 na kuruhusu 53.